SWALI: FASIHI SIMULIZI YA
KIBANTU INGEWEZA KUWA NI RASLIMALI MUHIMU
fafihi simulizi ya kiswahili
KWA MAENDELEO YA JAMII. BAINISHA
AMALI ZINAZO AKISIWA NA KABILA LA KIBANTU ZA TANZANIA NA VIPENGELE MUHIMU VYA
UHUSIANO WAKE KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA JAMII KWA KUZINGATIA MUKTADHA MPANA
WA UTANDAWAZI. MIFANO IJIKITE KATIKA KABILA LA WASAFWA NA WANYAKYUSA
Fasihi
simulizi kama dhana, imeelezwa na wataalamu wengi kwa kutegemea nadharia na
mitazamo mbalimbali , hata hivyo ni muhimu kufahamu ya kwamba maana inayopewa
dhana au kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu
wanaohusika, mahali dhana hiyo inapotokea na hata kipindi au wakati husika. Hii
ndio sababu tunapata fasili mbalimbali zinazorejea dhana ya fasihi simulizi
kama ifuatavyo:
Ngure,
A.(2003), anafasili fasihi simulizi kama sanaa itoayo maudhui yake kwa lugha ya
maneno ambayo hutamkwa ama kutendwa. Kwa mijibu wa maana hii, Ngure anasisitiza
kwa kusema fasihi ni namna ya utoaji wa maudhui kisanaa na kuwasilishwa kwa
njia ya mdomo ambayo huweza kutamkwa au kutendwa.
Mulokozi
(1996:24) anasema, fasihi simulizi ni fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani
na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia
maandishi, hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha (mazingira)
fulani wa kijamii na kutawaliwa na mwingiliano wa fanani, hadhira, fani
inayotendwa, tukio, mahali na wakati. Mulokozi anafafanua kwa kusema fasihi
simulizi ni ile fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa
njia ya mdomo ikiambatana na vitendo, swali ni kwamba fasihi simulizi
inayowasilishwa kwa njia ya redio, tepurekoda pamoja na luninga sio fasihi
simulizi?
Finnegan
(1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye
huiumba kwa maneno katika tukio maalumu. Katika fasili hii Finnegan hajagusia
mambo muhimu katika fasihi simulizi kama vile muktadha, namna ya uwasilishaji,
uhifadhi na badala yake amejikita zaidi katika ubunifu alionao msanii
anayeiumba fasihi husika.
Balisidya
(1983) anafasili fasihi simulizi kama aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo
katika kuiumba, kuiwasilisha na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
Fasili hii ina mapungufu kwani haijafafanua juu ya ubunifu alionao msanii katika
kuikamilisha, na pia katika suala la uwasilishaji tunaweza kujiuliza kwamba je,
fasihi simulizi lazima iwasilishwe kwa njia ya mdomo tu?
Hivyo
basi, kutokana na fasili zote hapo juu tunaweza kufasili fasihi simulizi kuwa
ni kazi ya sanaa inayotumia mazungumzo ya ana kwa ana ikihusisha utendaji na
njia nyingine za mawasiliano kama vile tepurekoda, redio, luninga na vinginevyo
ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Kuna
tanzu nyingi za fasihi simulizi kutokana na wataalamu tofauti kuwa na mawazo
tofauti tofauti, tanzu hizo zimewekwa katika makundi au tanzu kuu nne ambazo ni
hadithi, semi, maigizo na ushairi.
TUKI
(2004) wanafasili amali kuwa ni matendo, kazi na mazoea, hivyo kwa maelezo hayo
amali za jamii ni jumla ya mazoea, kazi mbalimbali na matendo yote yanayofanyika
katika jamii husika kama vile mila na desturi, utamaduni, dini, siasa na
uchumi.
www.wikipedia.org/wiki,
wanafasili amali za jamii kama tawi la isimu ambalo huchunguza uhusiano kati ya
lugha na jamii, aidha inajihusisha na athali yoyote ya jamii kama vile desturi
za watu, matazamio na muktadha katika nyanja za lugha na namna inavyotumika.
Hivyo,
amali za jamii huhusisha tamaduni, mila, desturi, dini, siasa na uchumi na haya
yote sharti yahifadhiwe katika uasili wake ambapo hutunzwa, huhifadhiwa, kulindwa
na kuendelezwa na fasihi simulizi.
Matumizi
ya utandawazi yalianzia miaka ya tisini yakimaanisha kukifanya kitu kuwa katika
kiwango cha kimataifa na kukifanya kuwa wazi na kufanywa na watu wa aina yoyote
duniani (www.wikipedia.org/wiki/isimu).
Kutokana
na fasili hii, utandawazi unaweza kuelezwa kama njia ambayo wenyeji au taifa
hufanya mambo kuwa ya kimataifa na unahusu suala zima la uchumi, biashara, teknolojia,
siasa na utamaduni.
Wasafwa
na Wanyakyusa ni miongoni mwa makabila ya kibantu yanayopatikana nchini
Tanzania mkoani Mbeya.
Kabila
la Wasafwa hupatikana katika wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, jamii hii
inajishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji. Shughuli hizi ndizo zinazofanya
amali zao zitofautiane na amali za jamii nyingine.
Kabila
la wanyakyusa hupatikana katika wilaya za Rungwe na Kyela katika mkoa wa Mbeya,
jamii ya wanyakyusa hufanya shughuli mbazo hutofautiana kulingana na sehemu
wanakotoka (yaani mazingira). Wanyakyusa wa Rungwe hujishughulisha na kilimo na
ufugaji na wale wa Kyela hujishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi.
Ingawa
makabila haya hupatikana katika wilaya husika yaani Wasafwa kwa wilaya ya Mbeya
na Wanyakyusa wilaya ya Rungwe na Kyela, shughuli za utafutaji mali
zimesababisha jamii ya Wanyakyusa na Wasafwa wapatikane sehemu nyingine pia za
nchi ya Tanzania.
Amali
mbalimbali zinazopatikana katika makabila ya kibantu ni pamoja na mila na
desturi, utamaduni, dini (imani), siasa na uchumi.
Utamaduni
ni jumla ya mambo yote yanayobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo
yake (Mwambusye, 2013). Katika fasili hii mambo yanayozungumziwa ni ndoa, uzazi,
malezi, marika, mafunzo mbalimbali ya mazingira na shughuli zingine kama jando,
ngoma na imani katika Mungu, miungu, mashetani na mizimu, vyakula, mavazi,
mapambo, salamu na lugha.
Utamaduni
ni mojawapo ya nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii yoyote ile kama amali
mojawapo ya jamii, tamaduni zilikuwa sharti zibaki katika uasili wake katika
vipengele vya muktadha, wahusika, maudhui, hadhira na fanani.
Suala
la ndoa katika kabila la wasafwa waliohusika kumfundisha mwali ni shangazi na
bibi ambao hasa walikuwa ndio fanani, mwali huyo alifundishwa namna ya kuishi
katika ndoa pamoja na matumizi mazuri ya chakula katika familia, kwa mfano
binti alifundishwa kupika chakula ambacho kingetosheleza mahitaji ya mumewe na
familia yake kwa ujumla bila kubakiza na kukitupa. Katika shughuli hii mwali
ndiye aliyekuwa hadhira na ukweni ndio palikuwa mahali pa kutendea na maudhui
yalikuwa ni mafunzo kuhusu maisha ya ndoa na fanani walikuwa bibi na shangazi
wa mwali, katika kipindi hicho mafunzo hayo yalimfundisha mwali namna ya kuishi
na jamii inayomzunguka na mafunzo yote yalifikishwa kwa njia ya misemo, nyimbo
na hadithi. Mfano wa nyimbo zilizokuwa zikiimbwa wakati wa mafunzo hayo ni kama
vile:
“Wamala yashi
ingano
yaleta bana yao
yenye ubaba ni mama
bayinzilile mwigomba”.
Wimbo
huu ulimfundisha mwali kutokumaliza chakula ndani kwa ajili ya matumizi ya
baadaye na kwa ajili ya wageni.
Kutokana
na maendeleo ya utandawazi amali hii imepoteza uasili wake kutokana na
kuathiriwa katika uwasilishaji wake, fanani yake, mahali pa kutendea na hata
maudhui yake yaani mafunzo hayo katika muktadha wa utandawazi huitwa “Kitchen
party” au sherehe ya jikoni (tafsiri yetu) ambayo hufanyika kwenye kumbi na
fanani huwa mtu yeyote sio wale wa asili na maudhui pia yamebadilika kwani
yaliyofundishwa kipindi katika kipindi kile sio yanayofundishwa leo. Hivyo
amali hii imepoteza thamani yake ya kuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya
jamii.
Kimsingi
katika ndoa za kinyakyusa wazazi ndio waliohusika kuwachagulia wenzi wa ndoa
vijana wao, suala la utoaji wa mahari ilikuwa ni sehemu ya amali ya jamii kwa
kabila la Kinyakyusa. Ili kuhakikisha usalama wa binti wa kinyakyusa bibi au
shangazi waliwachunguza mabinti zao mara kwa mara mpaka siku ya ndoa, mchakato
huo ulizua misemo mingi kwa mfano mzazi angeweza kumwonya binti yake ajitunze
kwa kusema “Api kujoba pa kijinja” yaani heshima na mambo yako yatathibitika
penye migomba. “Pa kijinja” palikuwa ni
mahali ambapo binti alipelekwa kwa uchunguzi ili kuthibitisha ubikra wake hivyo
kitendo cha kumchunguza kiliitwa “Ukosya” yaani kuoshwa. Endapo binti
akigundulika kuwa alishaingiliwa kimwili ilisemwa kuwa “inguku jiligilwe” yaani
kuku ameliwa, hii ilisababisha binti kutolewa mahari ndogo yaani ng’ombe
wachache ikilinganishwa na binti ambaye alikutwa salama yaani hajaingiliwa na
wanaume yaani aliyekutwa ni bikira ambaye mahari yake ilikuwa ni kubwa.
Kutokana na umuhimu huo, mabinti walilazimika kujitunza mpaka siku ya
ndoa, hali iliyosababisha mahari kuwa
kubwa na heshima kwa familia husika na fahari kwa ukoo wa mwanaume.
Kwa
upande wa jamii, hali hii ilisaidia wanawake kutokuchezewa na kutozaa watoto nje
ya ndoa yaani “isigwana”, kwa hali hiyo uchumi wa wazazi wa binti uliongezeka
pamoja na heshima ya binti na jamii kwa
ujumla.
Kutokana
na utandawazi, mfumo wa elimu kuwapeleka watoto shule na mwingiliano wa
tamaduni umesababisha wanyakyusa kuoana na makabila mengine, hivyo kusababisha amali hii kuathiriwa na utandawazi
kwa kuwa hakuna tena utaratibu wa kuwakagua mabinti yaani “Ukosya”, pia utaratibu wa kutoa mahari nao umebadilika
kwani mahari ya kutoa ng’ombe imekuwa ikithaminishwa na fedha taslimu.
Hivyo
basi, katika kipindi hiki baadhi ya wazazi wamekosa mahari ambazo zingewasaidia
kuendesha shughuli zao za maendeleo kutokana na watoto wao kujioza wenyewe na
kusababisha mahali kuwa kidogo na hivyo kuifanya amali hii kama kipengele
muhimu cha fasihi simulizi kupungukiwa thamani ya kuwa rasilimali muhimu katika
maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Tambiko
ni utekelezaji wa ada maalumu ili kutuliza mizimu, koma au pepo, sadaka edaha,
kafara, mviga, miiko (TUKI, 2004). Hivyo tambiko ni sadaka itolewayo kwa
mwenyezi Mungu au miungu kwa lengo la kuomba au kumshukru kwa mambo mbalimbali
yanayoikabili jamii. Tambiko katika jamii ya wasafwa ilihusisha matukio
mbalimbali katika jamii kama vile magonjwa, njaa, ukame, mashambulizi ya
wanyama au maadui ambavyo viliaminiwa kutokana na kuwaudhi mizimu au
miungu. Unyeshaji wa mvua kwa wakati na
kiasi cha kutosha ulikuwa ni muhimu sana wakati ukame ulipotokea. Kiongozi mkuu
huongoza kundi la wazee kwenda “Iganjo” yaani mahali pa kutambikia wakiwa na
pombe ndani ya vibuyu vitano au sita pamoja na kuku mweusi. Siku maalumu
hutangawa kwenda kuomba mvua hivyo hakuna mwanajamii anayeruhusiwa kufanya kazi
yoyote. Mwene ndiye kiongozi wa ibada kwa kusihi mizimu, mfano “uposhele inguku
ini, tuhanzaje hunzi hwilwepei invula itonye”, maana yake “Pokea kuku huyu
tunataka nchini kuwe kweupe akiomba mvua inyeshe”.
Baada
ya hapo wazee humchoma kuku akiwa na manyoya yake mpaka aive na humla na kunywa
pombe. Ibada ziliweza pia kuuliza neno gumu na kushukru kwa mambo mazuri
waliyoyapata. (http://www.safarilands.org/docs/jamii-ya-wasangu-tanzania.pdf).
Kwa
upande wa kabila la wanyakyusa kulikuwa na tambiko kwa miungu kupitia mizimu
kwa madhumuni mbalimbali na hasa walifanya hivyo kwa ajili ya kushukru endapo
mwaka mzima hakukuwa na balaa lolote na kuomba msaada kama kuna tukio mfano baa
la njaa, magonjwa, ukame ili kutokomeza tatizo hilo. Siku ya tambiko la kuomba
mvua ilikuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuwasha moto hasa nyakati za asubuhi
hadi pale “Kyungu” (Kiongozi wa matambiko) atakapowasha moto mkubwa kando ya
kibanda kidogo maarufu kama “Moto ufya” hii ilikuwa ni kama ishara ya kutoa
salaamu za maombi ya mvua kwa mizimu. Waliamini kuwa moto huo ukizimika muda mfupi
baada ya kuwashwa basi ombi lao limekataliwa na shughuli za kuomba mvua
hubatilishwa hadi siku nyingine.
Katika
kufanya hivyo maeneo yaliyohusika kufanyia matambiko yaliitwa “Isyeto/Masyeto,
wahusika katika shughuli hiyo walikuwa wazee maalumu, vifaa walivyotumia
kutambikia ni pamoja na vibuyu, vyungu, pombe, ulezi, kuku mweusi, pesa.
Ng’ombe alichinjwa kwa mwaka mara moja kwenye maeneo hayo ya masyeto kwa
kuunganisha na pombe ambapo watu walitumia huko. Mavazi yaliyotumika yalikuwa
ni ya kawaida. Katika kutoa sadaka zilitolewa pesa (senti) kila baada ya muda
fulani na pombe ambayo kiasi fulani iliachwa kwenye kibuyu, ilikuwa ni marufuku
akina mama kutafuta kuni ndani ya isyeto, katika kila isyeto kulikuwa na chifu
anayehusika. Katika utambikaji pia kulikuwa na hadhira ambayo ilikuwa ni ya
kitaswira yaani mizimu, fanani walikuwa ni wale wazee waliokuwa wanatambika.
Tangu
utandawazi umekuwa ukishika kasi kila uchao, dini za kigeni kama Ukristo na
Uislamu vimethoofisha sana utambikaji katika “Maganjo na Masyeto”, hii
inatokana na watu kuomba mahitaji yao tata katika makanisa na misikiti.
Matatizo mengi ya jamii yamekuwa yakielezwa kisayansi na kupatiwa ufumbuzi wa
kisayansi, maingiliano ya dini za asili na hizi za kigeni huleta mtafaruku
katika jamii na kupunguza mshikamano ndani ya jamii, mfano siku za matambiko,
wanajamii hukatazwa wasifanye kazi yoyote ambapo kwa nyakati hizi za utandawazi
watu wenye imani tofauti na matambiko huendelea na utaratibu wao kulingana na
kile mmoja anavyoamini, hali ambayo huleta pia mtafaruku na migongano katika
jamii ambapo pia husababisha kuharibu umoja na mshikamano wa jamii.
Siasa
ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha
uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii (TUKI, 2004). Katika
makabila ya kibantu uongozi katika jamii ulikuwa unapatikana kwa kurithishwa
ndani ya ukoo, chifu katika eneo au jamii husika pamoja na viongozi walikuwa
wanarithishwa madaraka kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya ukoo fulani,
kiongozi kabla ya kustaafu alikuwa anamuandaa mtu mmoja katika ukoo wake ili
atakapostaafu au kufariki atumie nafasi yake kuuendeleza ukoo. Viongozi katika
makabila ya kibantu walikuwa na mamlaka ya kusema lolote katika jamii na
kutekelezwa, mfano waliweza kutoa adhabu kwa mtu yeyote yule ambaye alikiuka
kaida au taratibu za jamii husika.
Kwa
mfano kabila la wasafwa kulikuwa na machifu wengi na kila chifu alikuwa na watu
wake wa kumsaidia katika utawala wake hasa wazee wa kimila (Mafumu). Kwa
kawaida chifu alichaguliwa kutokana na busara aliyokuwa nayo, uchaguzi
haukufuata urithishwaji wa mtoto mkubwa tu, bali ilitazamwa busara aliyokuwa
nayo mtoto huyo.
Aliyevunja
sheria alipewa adhabu ya kutubu na baadaye kulipa ng’ombe mmoja kwa wazee
(Mafumu). Adhabu hii ilikuwa na lengo la kuifanya jamii iweze kuishi katika
mwenendo mwema na kuwepo kwa maadili katika jamii hiyo ya wasafwa.
Ufuatao ni mfumo mzima wa utawala
ulivyokuwa katika kabila la wasafwa:
MWENE
|
FUMU
MKUU
|
MAFUMU
WAKUU
|
MAFUMU
WADOGO
|
RAIA
|
Kuingia
na kushamiri kwa utandawazi katika makabila ya kibantu kumeharibu mfumo mzima
wa uongozi au utawala ambapo kwa sasa viongozi wanapatikana kwa utaratibu wa
kiserikali ambao ulitokana na tamko la serikali ya awamu ya kwanza chini ya
uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo mwaka 1963 ambapo alifuta
rasmi utawala wa kichifu nchini Tanzania.
Baada
ya kufutwa kwa mfumo huu pamekuwepo na mfumo wa vyama mbalimbali vya siasa
ambavyo ndio vimekuwa vikigombea uongozi katika ngazi mbalimbali ambapo vimekuwa
vikisababisha machafuko ndani ya jamii na kusababisha utengano ndani ya jamii
moja ambapo yote haya ni matokeo ya utandawazi.
Uchumi
ni mfumo na mapato na matumizi ya watu katika nchi (TUKI, 2004:422). Kwa mujibu
wa tafsiri hii uchumi ni mali iliyopatikana kutokana na amali za nchi au watu
ambapo hujitengenezea mfumo wao wa mapato na matumizi.
Suala
la uchumi katika makabila ya kibantu halikutofautiana katika mifumo ya
uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi na uwindaji kwa kutaja mifano
michache. Jamii zilifanya kazi kwa kushirikiana na kugawana mapato kwa usawa.
Suala la uvivu lilipigwa vita, hivyo kila mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya
kazi alitakiwa awajibike ipasavyo. Shughuli hizi zilienda sanjali na vipengele
mbalimbali vya fasihi simulizi kama vile nyimbo, semi na majigambo.
Tukirejea
kabila la wanyakyusa kulikuwa na mitindo mbalimbali ya kulima, mkulima mmoja
mmoja au kwa kushirikiana katika shughuli nzima ya kulima yaani (Ndimya),
ambapo wanakikundi walilima kwa zamu katika shamba la kila mmoja aliyeshiriki
katika ushirikiano huu, hivyo walikuwa wakilimiana kwa zamu mpaka mashamba yote
yanamalizika. Ingawa wanyakyusa walifanya baadhi ya kazi zao kwa ushirikiano na
umoja hawakuwa na jadi ya kuimba wakati wa kufanya kazi zao, badala yake wakati
wa mapumziko waliimba nyimbo mbalimbali za maonyo, mafumbo au matukio
yaliyokuwa yanatokea katika jamii.
Mfano wa wimbo ulioimbwa baada ya kazi ni:
“Kiongozi: Kungwengwelela jumo jwene, jumo fiki
fyakwegelaga
wote: Kungwengwelela
jumo jwene, jumo fiki fyakwegelaga”.
Maana yake
ni: “Umempendelea mke mmoja huyo
mwingine kitu gani kilikuolea
au nani
alikuolea?”.
Kwa
mfumo huu wa maisha katika jamii za kinyakyusa nyakati za mapumziko baada ya
kazi zilikuwa ni nyakati za burudani na kubadilishana mawazo.
Wanyakyusa
walihifadhi mazao yao katika ghala zilizojulikana kwa jina la “Mitenene” ambazo
zilijengwa kwa matete na kusiribwa kwa kinyesi cha ng’ombe. Pia waliweza
kuhifadhi mazao darini ambapo palikuwa ni usawa na mafiga, mazao hayo
yaliyohifadhiwa usawa wa mafiga yaliwekwa kwa ajili ya mbegu katika msimu wa kilimo
uliofuata.
Baada
ya utandawazi kushamiri utaratibu wa kulima umebadilika sana kiutendaji, vifaa
vya kutendea na hata namna ya kufanya shughuli nzima ya kilimo, mpaka sasa
baadhi ya wakulima walio na uwezo mzuri kiuchumi wanatumia matrekta na plau (Jembe
la kukokotwa na wanyama na hasa ng’ombe), wakati huo huo wakulima walio wengi
bado wanatumia jembe la mkono ambapo pia wapo wanaolima wenyewe na wengine
wanaajiri vibarua kwa ujira wa kutwa au kutegemea na vipimo vya shamba.
Kutokana na ubinafsi huo hakuna tena ushirikiano hatimaye kutokomeza matumizi
ya nyimbo, semi pamoja na majigambo ambapo hivi vipengele vilisaidia kuleta
umoja na mshikamano katika kazi. Pia uhifadhi wa mazao umebadilika sana ambapo kwa
sasa nafaka huhifadhiwa kwa kutumia kemikali za kisasa na kuwekwa kwenye
maghala ya kisasa pamoja na kutumia mbegu zilizoandaliwa (kisayansi), kisasa
zaidi.
Uhusiano
ni hali ya kuwa na fungaman, uhusiano unaweza kuwa mbaya au mzuri (TUKI,
2004:427). Kutokana na maana hii uhusiano ni sehemu ya amali za jamii kwa kuwa
ni nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii. Wabantu hutunza uhusiano mzuri
baina ya familia, ukoo na jamii kwa ujumla ili kutimiza adhima husika.
Mahusiano katika jamii hujidhihirisha katika utani baina ya mtu na mtu, ukoo na
ukoo au kabila na kabila. Hali kadhalika salaamu, sherehe, misiba au starehe
mbalimbali zilikuwa ni ishara ya mahusiano mazuri katika jamii.
Wanyakyusa
wamegawanyika katika makundi makuu mawili kulingana na hali ya kijiografia,
kuna wale wanaoishi bondeni yaani “Ntebela” hususani pwani ya ziwa Nyasa
wenyewe huita “Nyanja” kwa maana ya bahari na wengine huishi milimani. Mgawanyo
huo wa kijiografia umesababisha tofauti kubwa kiuchumi. Wanyakyusa wa bondeni
ambayo ni wilaya ya Kyela wanajishughulisha na kilimo cha mpunga pamoja na
mazao mengine wakati hawa wanyakyusa wa milimani hujishughulisha zaidi na
kilimo cha ndizi na aina nyingine ya mazao yaliyo katika mfumo wa mizizi
iliwayo. Hata hivyo kutokana na mahusiano mazuri kati yao waliweza
kubadilishana bidhaa, mara nyingi wale wa milimani walibeba magimbi, ndizi na
hata mahindi ili kubadilishana na mpunga au samaki hali iliyozua utani na
nyimbo kati yao. Wanyakyusa wa bondeni walikuwa wanaimba nyimbo kama:
“Kiongozi
: Bisile aba mwamba aba ngata
inywamu
wote : Bisile aba mwamba aba ngata inywamu
Kiongozi
: Sokamo mu mphulo gwe kapimba ugwe
wote
: Sokamo mu mphulo gwe kapimba
ugwe”.
Maana yake
ni; “ Wamekuja watu wa milima
wenye nzinga kubwa
ewe kajitu kafupi ondoka uwanjani”.
“Nzinga
kubwa” ilitumiwa na wanyakyusa wa milimani ili kupunguza msuguano kichwani
kutokana na uzito wa mizigo waliyoibeba kichwani. Mabadilishano ya biashara
yalionesha uhusiano mzuri na kujenga undugu kati yao. Pia misemo ya utani kama
vile “Aba ngulya gwene” ulikuwa ni msemo
uliomaanisha kwamba watu wa milima ambao wanaweza kula wali bila mboga.
Katika
kabila la Wanyakyusa na Wasafwa wana namna moja katika kushirikiana wakati wa
misiba na matatizo mbalimbali kwa mfano, ukitokea msiba katika familia fulani
kwenye jamii, jamii nzima huhusika katika msiba ule na kushirikiana katika
shughuli zote za msiba huo. Wanaume na wanawake wa jamii nzima waliwajibika
kushinda na kulala mahali palipotokea msiba na kila mmoja katika jamii huweza
kuchangia chakula, kuni na vifaa vingine vilivyotumika katika shughuli nzima ya
mazishi kama vile majembe, makoleo, mkeka na ng’ombe, hii ilikuwa ni kulingana
na uzito wa msiba uliokuwa umetokea. Mbolezi ziliimbwa wakati wote wa msiba
ambapo waghani walikuwa wakitaja sifa na mema ya marehemu au ukoo wa marehemu,
waombolezaji wengine waliimba na kupita sehemu mbalimbali za makazi yao
wakiimba na kuchangishana nafaka kwa ajili ya msiba, kwa mfano katika kabila la
Wasafwa walikuwa wanaimba nyimbo kama hizi:
“Kiongozi: Ndio maana ×2
Waitikiaji:
Ndio maana twinzile
Kiongozi:
Ndio maana ×2
Waitikiaji:
Ndio maana twinzile
Kiongozi:
(Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
Waitikiaji:
Ndio maana twinzile”.
Wimbo
huu hutumika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya jamii na ndugu pamoja na jamaa
waliofiwa, wimbo una maana kuwa (Tumekuja kwa sababu tunaushiriano na nyie).
Kwa
upande wa kabila la Wanyakyusa waliimba hivi:
Waitikiaji: Twalimenye naloli
Kiongozi: Ukete abhandu bikulila
Waitikiaji: Ukete abhandu bikulila
Kiongozi: Keta tukwenda tukulila
Waitikiaji:
Keta tukwenda tukulila”
Wimbo
huu ulikuwa na maana kwamba kulikuwa na uhusiano mzuri kwa kusema:
Waitikiaji: Tulimjua sana
Kiongozi: Ona watu wanavyolia
Waitikiaji: Ona watu wanavyolia
Kiongozi: Tazama tunatembea
tukilia
Waitikiaji: Tazama tunatembea tukilia”.
Kutokana
na utandawazi kuingia katika jamii hizi fasihi simulizi iliyotumika kama amali
ya mahusiano imepoteza uasili wake katika kuihifadhi, kuwasilishwa, muktadha
wake pamoja na maudhui. Katika kipindi hiki cha utandawazi nyimbo kama hizi za
mbolezi zimerekodiwa katika kanda na zinaweza kuimbwa popote na wakati wowote
bila kuzingatia muktadha na katika hali yoyote. Kutokana na athari hizo za
utandawazi uhusiano katika jamii umedhoofika, kwa mfano mtu anaweza kununua
kanda na kwenda kusikiliza nyumbani, hivyo kwa sasa hata nyimbo hizi kwenye
misiba huwa zinawasilishwa kwa kutumia kanda za muziki na hivyo kupoteza
uhalisia wake.
Jando
na unyago ni sehemu ya malezi inayolenga kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake
ya kuwa mwanaume au mwanamke ili jinsia imjenge badala ya kumvuruga. Mara
nyingi wavulana huwa wanaongelea sri zao zinazowahusu wao katika makuzi yao na
huwa hawataki mtoto wa kike kuzijua hali kadhalika kwa upande wa mtoto wa kike
nao huwa wanamafunzo yao ambapo nao huwa hawapendi mambo wanayojifunza
yajulikane kwa watoto wa kiume, mafunzo haya yaliweza kutolewa na watu wazima
ambao ndio walitegemewa zaidi na jamii katika kutoa elimu ya jinsia.
Katika
jamii za kibantu zilikuwa na kawaida ya kuongelea mafunzo hayo ya siri na wazee
hasa babu na bibi ndio walihusika sana katika kutoa mafunzo hayo, kulikuwa na
mafundisho rasmi ambayo yalikuwa na umuhimu wa kujua mapema ukweli hasa kuhusu
maumbile ya binadamu. Kadri mtoto anavyozidi kukua ndivyo alivyohitaji
kujifahamu kijinsia ili aweze kukomaa na hatimaye kukabiliana na shughuli
mbalimbali za kijamii.
Katika
kabila la Wanyakyusa walizingatia malezi ya vijana na ilikuwa ni mwiko kwa mtoto
wa kinyakyusa kudeka, mama aliweza kula na watoto wa kiume chini ya miaka kumi
pamoja na wale wa kike ambao walikuwa bado hawajaolewa, lengo kubwa ilikuwa ni
kuwafundisha kula kwa adabu na kuheshimiana. Kwa upande wa mtoto wa kiume
aliruhusiwa kukaa na mama yake akiwa na umri chini ya miaka kumi, baada ya umri
huo hakuruhusiwa kukaa tena na mama yake bali aliambatana na wanaume kwa lengo
la kujifunza kazi. Mgawanyo wa kazi ulizingatia umri na jinsi kwa kuwa zamani watoto
wengi hawakuwa na fursa za kusoma, hivyo walipata elimu (mafunzo) kutoka kwa
wazazi wao. Watoto walipofikisha umri wa miaka kumi na moja au kumi na mbili
waliweza kukusanywa kutoka familia tofauti na kupelekwa mbali na wazazi wao ili
kujifunza maisha na kujitegemea na hivyo kuweza kuanzisha vijiji vipya kwa
kujenga nyumba kisha kuanzisha familia.
Wakati
wa utoaji wa mafunzo hayo semi na nyimbo mbalimbali zilitumika na zilitolewa na
wazee, kwa mfano:
“
Ukukoma ingunguni”
Tafsiri yake ni; “Kuua
kunguni”
Msemo
huu ulilenga kuelimisha watoto na kuwakomaza kuwa kuendelea kuishi kwenye
nyumba ya wazazi pamoja nao na hali wakiwa wamefikia umri wa kujitegemea sio
vizuri, hivyo walisisitizwa zaidi kujitegemea. (Mwambusye, 2012:23).
“Ukukula kitalikitali”
Tafsiri yake ni; “
Kukua haraharaka lakini bila umbile na akili au hekima”.
Katika
msemo huu walimaanisha zaidi kuwa mwili unakua upesi kuliko akili yaani ukuaji
wa mwili hauendi sambamba na ukuaji wa akili ( Mwambusye, 2012:27).
Kutokana
na mafunzo haya ya kukaa pamoja, vijana waliweza kujifunza majukumu mbalimbali
na malezi ya jamii zao kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na kuhimiza ushirikiano,
kuheshimiana na kuthaminiana na hatimiye kuishi kama ndugu na jamii moja na hapo
ndipo Wanyakyusa wanapo sema:
“Nkamu ju mundu”
Tafsiri yake ni: “Undugu ni kufaana na sio kufanana”.
Kutokana
na kushamiri kwa utandawazi, mfumo huu wa maisha umeathiriwa kwa sababu muda
mwingi watoto wanakuwa shuleni na wanapofikia hatua ya kuhitimu elimu ya msingi
huwa katika umri wa miaka kumi na tatu hadi kumi na sita na baada ya hapo
wengine hubaki kijijini na wengi huweza kuhamia mijini.
Pamoja
na hayo, hata kule vijijini hakuna tena ardhi ya kutosha kuanzisha vijiji vipya
kama ilivyokuwa zamani na hii imesababisha iwe vigumu kupata nafasi ya
kuhudhuria mafunzo au malezi ya kijamii.
Kwa
upande wa kabila la Wasafwa, mtoto alipewa elimu kwa vitendo ambapo elimu ya
kwanza kabisa kwa mtoto wa kisafwa ni elimu ya kilimo, mtoto wa kiume na wa
kike akifikia umri wa miaka mitano na kuendelea alifundishwa kuwa jembe ndio
kila kitu, jembe ndio maisha yake, aliweza kupewa sehemu ndogo ya shamba kwa
ajili ya kulima mahindi ya kuchoma, alitengenezewa jembe dogo la mpini mfupi kadri
ya kiganja chake cha mkono, hivyo alifundishwa namna ya kuwasaidia wazazi wake.
Mtoto wa kiume pia alifundishwa elimu nyingine na ilitolewa kulingana na kazi
aliyopendelea kuifanya atakapokuwa mkubwa, mfano alifundishwa kujenga nyumba,
kuchonga mizinga ya nyuki, kukamua maziwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Pia
alifundishwa namna ya kuishi na mke. Kwa upande wa mtoto wa kike naye hakuwekwa
mbali na mafunzo ya kumuimarisha zaidi atakapokuwa mkubwa ambapo alifundishwa
kupika, kusafisha vyombo na nyumba pamoja na namna ya kuishi na mume pamoja na
namna ya kulea watoto.
Hakukuwa
na elimu ya marika, bali watoto wa jinsi zote waliweza kula pamoja, kucheza na
kulala pamoja na watoto wengine katika jamii. Wakati wa kula, kama mtoto
amesimama wima ikiwa wengine wamekaa aliambiwa aende nje amwite “Mwimilila”
yaani aliyesimama, basi mtoto huyo ataita kwa sauti akiwa hajui kama anajiita
yeye mwenyewe. Kwa upande wa maonyo vilitumika vitendawili kama “Inzili nu
mwene” yaani sina mfalme, ambapo waitikiaji walijibu “Ulundyelele” kwa maana ya
utelezi wakilenga kufafanua kuwa utelezi hauchagui mtu unaweza kumdondosha
mfalme, tajiri hata masikini. Katika maisha ya sasa kitendawili hiki kingeweza
kutumika kuonya watu wawe makini na tabia zao maana kuna magonjwa hatari
yasiyochagua wa kubagua kama vile “Ukosefu wa Kinga Mwilini” (UKIMWI).
Kutokana
na maendeleo ya utandawazi katika harakati za kupambana na maisha jamii ya
Kisafwa imetawanyika na kujikita zaidi katika shughuli za watu wa makabila
mengine kama vile biashara, ulinzi na hata shughuli za udereva. Ni vigumu kwa
vijana wa sasa wa kisafwa kuelekezwa kuwa shughuli kuu katika kabila lao
(kisafwa) ni kilimo na wakaelewa, hii inatokana na kuwa wengi wao wamesoma na
hivyo kuona kuwa kukimbilia mjini na kuendelea na shughuli zingine kama
biashara, kazi za ofisini tofauti na zile za jamii yao ni ufahari na hivyo
kuendelea kuishi mijini na kudharau vijijini pamoja na shughuli za kilimo na
hivyo kuona shughuli hiyo imepitwa na wakati.
Afya
ni kuwa na hali nzuri ya mwili bila ya maradhi, uzima, siha (TUKI, 1981). Kwa
ujumla afya ni hali ya kutunza mazingira kwa lengo la kumtunza binadamu
asipatwe na maradhi yoyote ya kimwili ikijumuisha utunzaji wa vyanzo vya maji,
masuala ya tiba, uzazi wa mpango na upatikanaji wa chakula bora. Jamii
mbalimbali za kibantu zimekuwa zikitunza afya zao katika nyanja mbalimbali kama
vile masuala ya tiba, maji, uzazi wa mpango na chakula bora kwa ajili ya
maendeleo mbalimbali katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na
mengineyo.
Katika
makabila ya kibantu afya ilionekana kama ndio msingi wa maisha yao. Pia afya
mbovu ilionekana kama kichocheo hasi cha maendeleo, ili jamii iepukane na
maradhi hayo ilitumia tiba mbalimbali za asili, mfano kwa upande wa wanyakyusya
walizingatia sana utunzaji wa vyanzo vya maji ambapo maji hayo yalitumika kwa
ajili ya kupikia na kunywa, maji ya kunywa yalitokea katika chanzo chake kutoka
kwenye mwinuko wa chanzo hicho na yalitiririka kupitia kifaa maalumu
kilichijulikana kama “Lyubhubhu”,ambalo ni ganda la mgomba au bomba lenye uwazi
mkubwa. Sehemu hiyo haikuruhusiwa mtu yeyote kuoga wala kufua na kufanya
shughuli zingine zaidi ya kuchota maji tu, ilifanyika hivyo ili kutunza maji na
vyanzo vyake, hivyo basi kuna sehemu zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuoga
na kufulia ambapo zilikuwa mbali na zile za kuchota maji. Tiba za dawa za asili
zilitumika kwa kuponya au kuzuia magonjwa yaliyojitokeza katika jamii ya
kinyakyusa, kulikuwa na dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali kwa mfano “Pupwe” ni
dawa ya kutibu tumbo, “Kibangula” ni dawa ya mafua, “Mingongobhele nsemwasemwa”
hii ilitibu tumbo na kisukari. Pia kulikuwa na dawa ambazo ziliandaliwa na watu
maarufu, hizi zilinyunyizwa kwenye mlango wa kila nyumba ili kuondoa balaa au
kuzuia balaa kama magonjwa. Kitendo cha kunyunyiza kilijulikana kama “Kumisa”
yaani kutoa balaa.
Wanyakyusa
pia walitumia uzazi wa mpango kwa kutumia njia mbalimbali za asili ambazo
hazikuwa na madhara yoyote katika miili yao, mfano wanawake walivaa dawa
kiunoni ili kuzuia mimba na kuepuka kuzaa watoto wa kufuatana kwa mfululizo na
kwa muda mfupi. Njia nyingine mwanamke (mzazi) alipelekwa kwa wakwe mpaka mtoto
atakapokuwa na umri mkubwa kiasi cha
kumuwezesha tena mama mzazi akipata ujauzito mwingine isilete madhara katika
malezi ya mtoto aliyepo. Njia hizi zote zilisaidia kupata idadi ya watoto
wanaotakiwa au idadi iliyopangwa na familia husika, pia kuipa familia nafasi ya
kulea mtoto aliyezaliwa.
Kulingana
na utandawazi, tiba na kinga hufanyika kwa kutumia dawa za kutibu na kukinga
magonjwa mbalimbali kama vile panado, septrini, kinga za kifaduro, polio, surua
na mengine mengi, kwa upande wa uzazi wa mpango kumekuwepo na vidonge vya
majira, vitanzi, sindano za kuzuia mimba pamoja na mipira ya kiume na kike.
(Kondomu).
Kwa
upande wa kabila la wasafwa, usafi wa nyumba, mwili ulitiliwa mkazo na kuwa na
umuhimu mkubwa hasa kwa wanawake. Nyumba zao zilisilibwa kwa udongo wa rangi
mbalimbali na kuchorwa michoro ya urembo tofauti tofauti. Mavazi yao ambayo
yalikuwa ni ngozi za mbuzi zilizolainishwa kwa mafuta ya ng’ombe au mafuta ya
nyonyo yalitunzwa kwa uangalifu. Kabila hili la wasafwa kama walivyo wanyakyusa
walioga ndani ya vijito ambavyo huzunguka makazi yao kwani wasafwa huweza
kuweka makazi yao karibu na vijito. Jamii ilikemea uchafu wa mwili kwa kutumia
mafumbo pamoja na nyimbo mbalimbali, kwa mfano moja ya nyimbo zilizotumiwa
kuhimiza utunzaji na usafi wa mwili kwa kuoga ni pamoja na:
“Uyogaje uyogaje × 2
uyogaje hyena
muzina uyogaje
Ihwili isabuni ya sumuni uyogage”.
Maana yake
ni: “Uwe unaoga, uwe unaoga
mama mtoto uwe
unaoga
sasa kuna sabuni
ya thumuni”.
Suala
la maji, katika jamii ya kisafwa ilitunza vyanzo vya maji, hasa yanayotumika
kupikia na kunywa. Ilizuiliwa kunywesha mifugo au kukanyaga penye chanzo cha
maji, maji mengi hutiririka kutoka milimani ambapo wasafwa huita “Inzalala” kwa
maana ya maji yanayotiririka.
Kutokana
na maendeleo ya utandawazi siku hizi wasafwa
hutumia maji ya bomba, tiba za kisasa na kusababisha dawa za asili kukosa
umaarufu na umuhimu. Hivyo dawa za kisasa zina madhara makubwa tofauti na zile
za asili ambazo zilikuwa ni za uhakika na zilisababisha watu wa jamii hii
kuweza kuishi muda mrefu bila matatizo.
Kukua
kwa sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo katika nyanja
za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia
yamesababisha utandawazi. Kutokana na mabadiliko haya, fasihi simulizi kama
kazi ya kisanaa iliyojaa ufundi na ubunifu ndani yake haina budi kuendana na
mabadiliko hayo maana hata mfumo wa maisha hubadilikabadilika katika jamii
kulingana na maendeleo yanavyozidi kuimarika na kujitokeza. Hivyo pamoja na
mabadiliko hayo si vyema kupuuza fasihi simulizi kwani yenyewe ndiyo fasihi
kongwe na ndiyo iliyoibua fasihi andishi baada ya kugundulika kwa maandishi
kwani fasihi hata kabla ya utandawazi ilikuwa na mchango mkubwa sana katika
kuimarisha amali za jamii.
MAREJEO
Balisidya, M. L, (1983), Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi, kutoka
kwa Mulika namba 19 (1987),
Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar
es Salaam.
Mulokozi, M.M (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es Salaam, Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania.
Mwanbusye, D (2012), Lugha, Utamaduni na Fasihi simulizi ya Kinyakyusa,
Dar es Salaam.
Ngure, A (2003), Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari, Nairobi, Phoenix Publishers
Ltd.
Finnegan, R. (1970), Oral Literature in Africa, OpenBook Publishers, Cambridge.
TUKI, (1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Nairobi, Oxford University Press Ltd.
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam, Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili.
2 comments:
adhima ni nini
Nilichanganyikiwa na kuhuzunika mume wangu alipoomba talaka. Kisha nikawasiliana na Dk DAWN, baada ya kuona ushuhuda mwingi wa jinsi Dk DAWN alivyosaidia watu wengi kurejesha amani katika ndoa na uhusiano wao,
Pia niliona jinsi alivyotibu magonjwa mbalimbali na kusaidia watu wachache kutibu ugumba, niliamua kuwasiliana naye kwa msaada,
Aliahidi kusaidia wakati baada ya kumueleza kila kitu, nilimpa kila alichouliza na akafanya kazi yake, sasa mume wangu ananipenda sana na ananitendea kwa Matunzo. Nyumba yangu ni ya amani na imejaa furaha, shukrani zote kwa Dk DAWN,
Wasiliana naye ikiwa una tatizo lolote kwa sasa. Yeye ni WhatsApp: +2349046229159
Barua pepe: dawnacuna314@gmail.com
Post a Comment