Saturday, May 3, 2014

NADHARIA ZA MAANA

Habwe na Karanja (2007:204), Crystal (1987), Matinde (2012), Ogden na Richards (1923), wanakubaliana kuwa neno  maana lina fahiwa nyingi, linaweza kudokeza sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelekezo, ufafanuzi, kufaa na ukweli. Kutokana na ugumu uliopo katika kufafanua maana ya maana, wanaisimu wamefafanua aina kuu mbili za maana ambazo ni maana ya msingi na maana ya ziada. Utetezi wa nadharia hii umesababisha kuibuka kwa nadharia mbalimbali ambazo zinajaribu kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali, ambazo chimbuko lake ni wanaisimu, wanafalsafa, wanamantiki na wanasaikolojia.

Nadharia ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo fulani (Mdee na wenzake, 2011). Kwa msingi huo nadharia hubeba mawazo, dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au kwa lengo la kueleza hali fulani, chanzo, muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.

Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira na mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni. 

Nadharia za maana ni miongozo ambayo hutambulisha mbinu mbalimbali za kujifunza namna ya kufasiri maana katika lugha (Matinde, 2012:247). Katika kufafanua maana nadharia zinazohusika ni nadharia ya urejeleo, dhana au taswira, matumizi, uelekezi, masharti‒ukweli, kichocheo‒mwitikio, na vijenzi Semantiki.

Ufuatao ni ugumu unaojitokeza katika kufasili maana ya maana kwa kuzingatia nadharia za maana kama zinavyo pambanuliwa.

Nadharia ya urejeleo iliasisiwa na Ogden na Richards, wanafalsafa hawa wanadai kuwa maana hujitokeza pale palipo na kirejelewa chake (Lyons, 1981). Waasisi wa nadharia hii wanadai kuwa lazima kuwe na kirejelewa. Mfano mtu kipo kitu kinachorejelewa, waasisi hawa waliibuka na dhana ya pembe tatu ili kueleza nadharia yao kama inavyoonekana hapa chini.







                                        Dhana (fikra)
                                                         

              Umbo la isimu                          kirejelewa (kitaje)

Kuna umbo la isimu kama kitaja neno, misemo, kauli au sentensi na vitu hivi hufanya tujenge dhana akilini. Dhana hii ndiyo inatufanya tupate kirejelewa, kuna uhusiano imara kati ya umbo la isimu na dhana. Dhana na kirejelewa akilini hakuna uhusiano imara kati ya umbo la isimu na kirejelewa, kiunganisho kati ya neno na kirejelewa katika dunia halisi bali ni fikra tu (Matinde, 2012).

Ugumu unaojitokeza katika kueleza maana ya maana katika nadharia ya urejeleo ni kwamba si kila kinyambo au leksimu yenye maana ina kirejelewa chake (Austin, 1970). Ni dhahiri kuwa pamoja na kuwepo kwa maneno mengi yenye virejelewa vyake kuna baadhi ya maneno yasiyokuwa na virejelewa. Nomino dhahania hubeba maana fulani katika jamii ya watu. Kwa mfano Mungu, malaika, jini, shetani, njaa, upole, upepo, hasira na furaha ni vinyambo vyenye maana ijapokuwa havina kirejelewa kama nadharia inavyodai. Kukosekana kwa kirejelewa kunasababisha utata au ugumu katika kufasili maana kwa kuzingatia nadharia ya urejeleo.

Kielelezo 2

         Umbo la isimu↔ dhana ↔kitajwa
               ↓                ↓                   ↓
             Mungu        X            – mwenye kuumba ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake.
                  
Upepo             X            − hewa isiyotulia na aghalabu huenda kwa kasi.

Pia nadharia hii inapata ugumu wa kufasili maana ya maana kwa maneno yenye uhusiano wa kihomonimia ambapo kuna baadhi ya maneno yanayorejelea zaidi ya hali au kitu kimoja (Matinde, 2012:252). Kwa mfano    paa [+ondoa mamba ya samaki kwa kuparuza kwa kitu kama kisu]
   [+enda juu]
   [+chukua baadhi ya makaa ya moto weka mekoni]
  [+mnyama wa porini anayefanana na mbuzi aliye        mwembamba sana]


Kaa [+kipande cheusi cha kuni kilichochomwa na kuzimwa kabla ya kuwa majivu]
[+mnyama mdogo wa majini mwenye miguu sita au zaidi]
[+kuweka matako au makalio juu ya kiti]

Panda [+mgawanyiko katika kitu]
           [+pembe kubwa na ndefu iliyotobolewa tundu katika              ncha yake inayopigwa katika ngoma au kutoa
             taarifa]
           [+paji la uso]
           [+enda kuelekea juu ya kitu]
           [+weka mbegu au mche katika ya ardhi ili ikue]

Kutokana na mifano hiyo hapo juu ni dhahiri kuwa kwa kutumia nadharia hii ya urejeleo ni vigumu kufasili maana ya maana kwa kuwa neno paa, panda na kaa hurejelea fahiwa nyingi.

Nadharia ya urejeleo haifanyi kazi kwenye maneno yenye uhusiano wa kipolisemia (Holm na Karlgren, 1995:3). Polisemia ni maneno ambayo yana uhusiano kimaana, na mara nyingi maana ya maneno huwa imepanuka kadri ya mpito wa wakati. Mfano wa maneno kama vile;
Kichwa [+ cha binadamu]
              [+ kama kiongozi]
Jicho      [+ la sindano]
              [+la binadamu]
mguu     [+wa binadamu]
              [+wa gari]

Kutokana na mifano ya maneno hayo hapo juu, nadharia ya urejeleo haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kipolisemia. Kwa sababu waasisi wa nadharia ya urejeleo wanadai kuwa katika urejeleo lazima kuwe na kirejelewa kimoja na jina moja tu, lakini maneno yenye uhusiano wa kipolisemia huwa na kirejelewa zaidi ya kimoja ambavyo huweza kurejelea maana tofautitofauti.

Maneno kama vielezi, na vihusishi yanakosa maana katika nadharia hii (Filp, 2008:20). Kwa mujibu wa wanaurejeleo maana ya neno ni kitu kinachorejelewa na neno husika, kwa msingi huu maneno ni majina ambayo hutaja vitu. Aidha dhana hii inaonesha kuwa maneno yasiyokuwa nomino kama vile vielezi na vihusishi hayana maana, jambo ambalo halina ukweli. Hii ni kwa sababu lugha yoyote inajumuisha aina mbalimbali za maneno na si majina tu.

Nadharia hii haiwezi pia kufafanua maana katika kiwango cha sentensi, ambapo sentensi ni tungo inayojitosheleza kimaana, kimsingi huhusisha na mtendaji, neno sentensi haliwezi kufafanuliwa na kupata urejeo sentensi.kwa mfano (a) Mwalimu anafundisha darasani
(b) Juma anapika ugali
Katika sentensi hizi urejeleo wa maana ya sentensi nzima hauwezi kupatikana.


Aidha nadharia ya uelekezi ni dira ambayo waasisi wake wanadai kuwa, njia nzuri ya kufafanua maana ya kitu au dhana ni kusonta kwa kidole kile kinachorejelewa (uelekezi kwa kutumia kidole) (Matinde, 2012:252). Ni muhimu kuelewa  kuwa kalamu ni nini, na mbuzi nini na kuelewa kuwa umelenga kalamu nzima na mbuzi mzima na wala si sehemu tu ya kitu. Hivyo basi nadharia hii ya uelekezi inapata ugumu wa kufasili maana ya maana kama ifuatavyo;

Baadhi ya maneno katika lugha hayawezi kufafanuliwa kwa kusonta kidole ( uelekezi kwa kutumia kidole), mfano usingizi, urafi, njaa, hekima na busara. Kwani unaposonta kidole tumboni tunaweza kupata fahiwa mbalimbali kama vile njaa, shibe, ujauzito, minyoo na utumbo.

Pia nadharia hii ni ya kidhahania kwani huakisi tu kuwa anaye elekezwa anaufahamu au maarifa awali kuhusu kile kinachorejelewa. Mfano inatuwia vigumu kumfafanua ng’ombe kwa kusonta kidole kwa mtu asiyekuwa na maarifa ya awali ya ng’ombe kuwa anasifa zipi.

Aidha sababu za kiutamaduni huweza kuleta ugumu katika matumizi ya nadharia hii katika ufasiri na ufafanuzi wa kile kinachorejelewa. Mfano sehemu nyingi nchini Kenya neno mchele hurejelea uliopikwa na ambao haujapikwa, tofauti na Tanzania ambapo neno mchele hurejelea usiopikwa tu, na mchele uliopikwa huitwa wali. Hivyo ni vigumu kufafanua maana ya maana kwa kutumia nadharia hii ya uelekezi.

Nadharia vijenzi semantiki ni nadharia inayopambanua leksimu au vinyambo vilivyo katika kikoa kimoja cha maana kwa kutumia seti isiyo na ukomo (Baron, 1972). Kwa kigezo hiki sifa za leksimu hupambanuliwa kwa kutumia alama ya kujumlisha (+) inayodokeza uwepo wa sifa hiyo na alama ya kutoa (-) inayodokeza kutokuwepo kwa sifa tajwa. Aidha sifa bainifu za leksimu moja huitofautisha na leksimu nyingine.

Kutokana na matumizi ya mbinu ya uwili kinzani kutofaa katika leksimu ambavyo vijenzi vyake havibainishiki kwa urahisi, maana ya maana bado ni tata. Alama kinzani (+ na -) haviwezi kuwa na uzito katika aina zote za maneno kama vile vihusishi na vinganishi vinapotumiwa kufasili maana ya maneno husika. Kwa mfano ni rahisi kufasili neno mvulana kwa kutumia kijenzi MTU, MTU MZIMA na ME kwa kutumia alama + au lakini ni vigumu kubaini vijenzi semantiki katika kufasili kiunganishi kwa.  

Pia kutokuwepo kwa vigezo vya uteuzi wa vijenzi, kunatatiza fasili ya maana kwa kuzingatia nadharia ya vijenzi semantiki. Nadharia hii haiweki wazi sana kilichozingatiwa katika kuteua vijenzi husika wakati wa kufasili leksimu mbalimbali. Kwa mfano kijenzi ME kinatumiwa katika ufafanuzi wa leksimu zinazohusu binadamu na udugu. Jambo hili linatatiza na kuibua hisia zisizo na jibu la haraka kama kusahaulika kwa kijenzi KE, ni mfumo dume au la. Aidha matumizi ya vijenzi mlalo na mfuatano katika fasili za udugu hauzingatii umbali au ukaribu. Kwa mfano ndugu wa tumbo moja (kaka au dada) si lazima wafuatane kwa karibu.

Vile vile hakuna ukomo wa vijenzi katika fasili ya leksimu, pamoja na nadharia hii kufanikiwa kubainisha vikoa maana katika lugha, hakuna uthibiti wa idadi ya vijenzi vinavyotumika. Leksimu moja katika lugha inaweza kuwa na idadi tofauti ya vijenzi semantiki ukilinganisha na neno jingine katika lugha ile ile. Kwa mfano neno mvulana linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi [MTU], [MTU MZIMA] na [ME], wakati neno kaka linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi semantiki [ME], [MZAZI], [MLALO] na [MFUATANO]. Tofauti hii ya vijenzi semantiki kutoka neno moja na jingine inazua uvulivuli wa kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia ya vijenzi semantiki.

Aidha uwepo wa orodha ya vijenzi semantiki vya jumla vinavyotumiwa katika kufasili vinyambo vya lugha mahususi unakosa uthibitisho. Hii inatokana na ukweli kwamba kila lugha ina kanuni zake mahususi. Hivyo, ujumla unaosisitizwa na wanadharia ya vijenzi semantiki ni wa kutiliwa shaka kwani lugha inaweza kutofautiana na lugha nyingine katika vijenzi-semantiki kutokana na utamaduni wa jamii husika.


Nadharia ya dhana au taswira iliasisiwa na wataalumu wa isimu ambao ni Sapir na Desassure (Ogden na Richards, 1923). Ambapo msingi wake mkuu unaeleza kuwa maneno ya kiambo ni dhana au taswira inayoibuliwa na kiambo hicho akilini mwa mwanalugha wakati kiambo hicho kinapotumika. Kwa mujibu wa nadharia hii maana ya neno, kisemo na sentensi hujengeka akilini mwa msikilizaji au mzungumzaji. Kwa mfano tunaweza kuwa na NENODHANA. Nadharia ya dhana huhusisha moja kwa moja maana na wazo, taswira au hisi badala ya kuhusisha maana na kitu moja kwa moja. Pia husaidia kutoa majibu ya vinyambo visivyoweza kurejerewa kama vile: Mungu, shetani, upepo, njaa, usingizi, upendo na furaha, kwa kuwa nadharia ni wazo kuu linalomwongoza mtu ama jamii kutenda jambo fulani, ni dhahiri kuwa nadharia ya dhana humwongoza mwanalugha kuhusisha maana na wazo, taswira au hisi. Kutokana na upungufu wa nadharia hii upo utata au ugumu wa kufasili maana ya maana kwa sababu;

Dhana ya picha au taswira si bainifu na haiwezi kuchunguzika na kutabiri chochote. Huwezi kutabiri maana ya neno wala kufanya utafiti wa aina moja. Kwa sababu maana ya kiashiria hutokana na picha au taswira zinazojengeka akilini mwa mwanalugha. Hivyo maana ya maana inabaki kuwa telezi kwa kuwa kila kiashiria kinajengewa maana kulingana na picha iliyojengeka akilini mwa mwanalugha. Kwa mfano, kiashiria kiti kinaweza kujengewa picha tofauti akilini mwa mwanalugha kulingana na mazingira au uzoefu wa mwanalugha huyo. Kielelezo kifuatacho kinaonesha ni kwa namna gani picha ya kiti inaweza kuwa na maana mbalimbali kulingana na picha ya mwanalugha aliyoijenga akilini mwake.
Kiashiria                                        Taswira au picha
KITI                                              - kiti cha ofisini
                                                       - kiti cha kinyozi
                                                       - kiti cha umeme
Picha kama hizi zinajengwa na mwanalugha huku akiwa anafahamu kuwa kiti ni kifaa kilichotengenezwa kwa kutumia mbao, kwa ajili ya mtu mmoja kuketi, kina miguu minne, kina sehemu ya egemeo la nyuma. Ugumu wa kufasili maana ya maana unakuja pale mwanalugha anapokuwa na picha au taswira ya kiti chenye mguu mmoja na kile chenye miguu mitatu. Pia kiashiria nyumba kinaweza kuwa mfano wa kiashiria chenye kujengewa picha tofauti tofauti akilini mwa mwanalugha. Ikiwa nyumba ni jengo ambalo limekusudiwa kukaliwa na watu. Utata unakuja pale mtu anayejua kuwa banda ni nyumba ambayo hutumika kuwekea vitu au wanyama.

Aidha, picha za akilini ni dhahania ya kutosha kuweza kuwakilisha maana za nomino au vitenzi vya kawaida. Dhana anayoijenga mtu akilini mwake haiwezi kufumbata maana ya kitu halisi. Kwa mfano, mtu anaposikia neno mbuzi, dhana itakayojengwa inaweza kuwa dhana ya kiumbe mnyama, kiumbe hai, kifaa cha kukunia nazi, kiumbe mwenye miguu minne. Maana inayojengwa hutegemea zaidi ukomo wa fikra zake. Aidha utofauti katika uwezo wa kujenga dhana akilini juu ya leksimu fulani unapunguza maana ya kitu kinachojengewa dhana.

Hakuna picha ya jumla ya mguso katika nadharia ya dhana au taswira, kwani kila mwanalugha hujenga picha akilini mwake kulingana na imani yake, uzoefu wake, na mazingira yake (Holm na Karlgren, 1995:6). Katika majina au nomino dhahania mwanalugha hawezi kuvigusa viashiria ila huvijengea picha viashiria hivyo akilini mwake kama vile kiashiria shetani hakina mguso. Hakiwezi kuonekana wala kushikika bali mwanalugha hujenga picha akilini mwake kuwa kiashiria shetani kina maana ya kiumbe mwenye pembe ndefu, mbaya wa sura, kiumbe wa kutisha, tena mtoa roho za watu ambaye kwa hakika ni laghai lakini pia shetani kama kiumbe anaweza kujengewa picha na mwanalugha kuwa ni mtu yeyote mwenye matendo mabaya. Kutokana na ujengaji wa picha au dhana akilini mwa mwanalugha inakuwa vigumu kueleza maana ya maana kutokana na ujenzi tofauti wa picha katika akili ya mwanalugha.
  
Pia ugumu wa kueleza maana ya maana unakuja pale tu ambapo nadharia ya dhana inadai kwamba kila kinyambo kina husiana na taswira wakati si kila kinyambo kinahusiana na taswira (Holm na Karlgren, 1995:3). Kwa mfano, kinyambo kama vile ingawa, lakini na japokuwa havina taswira ambayo mwanalugha anaweza kuijenga akilini mwake. Hivyo basi kutokana na ugumu huu wa baadhi ya vinyambo kukosa taswira kunakuwa na utata wa kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia ya dhana au taswira na kuifanya maana ya maana kubaki kuwa dhana telezi tu.
 
Haiwezi kuelezea vinyambo viwili kuwa vyaweza kuwa visawe. Taswira au dhana inayojengwa akilini kuhusishwa na kinyambo kimoja tu haiwezi kukubalika kwani inaweza kuvitenga visawe kwani si kila dhana inawakilishwa na neno moja tu (Matinde 2012:256). Kwa mfano badala ya kusema nyati mwanalugha mwingine anaweza kusema mbogo, chumvi kuwa munyu, dagaa kuwa kauzu, tembo kuwa ndovu.  Uwepo wa visawe unadhihirisha udhaifu wa nadharia hii katika kufasili maana ya maana kwani taswira au picha ya akilini si kigezo toshelevu cha uchanganuzi na ufasiri wa maana. Hii ni kwa sababu kila mzawa wa lugha huwa na picha tofauti kuhusu maneno, vitu, dhana au hali mbalimbali.

Pia, nadharia hii haiwezi kuelezea maana ya sentensi au nahau, kwa kuwa maana ya kinyambo haipatikana katika leksimu tu na wala si utungo mrefu kama vile nahau na sentensi. Nahau ifuatayo inaweza kutumika kama mfano kuntu wa hoja hii. “amekula chumvi nyingi” katika hali ya kawaida ni vigumu mtu kujenga maana ya dhana hiyo kama hana uelewa wa wazo. Kwa maana hiyo dhana atakayoijenga itahusiana na chumvi moja kwa moja, wakati maana ya nahau hii ni kuishi miaka mingi.

Nadhria ya kichocheo-mwitikio iliasisiwa na wanasaikolojia Skinner na Watson, wao wanadai kuwa maana ya neno au dhana husika hufafanuliwa katika hatua tatu ambazo ni kichocheo, tamko na mwitiko (Holm na Karlgren, 1995:4). Hivyo nadharia hii inaeleza kuwa maana ya umbo la kiisimu linalotamkwa na msemaji hutokana na mwitiko wa msikilizaji. Kwa hiyo nadharia hii huchukulia kuwa maana ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Pia maana ya tamko huwa katika muundo wa kitendo –uneni kama inavyooneshwa hapa chini.
Kichocheo …→ (mwitiko…kichocheo) …→ mwitiko

Tamko     ……………… Jibu la msikilizaji.

Kwa mfano; Musa ameamua kuvuta sigara chumbani, kuna harufu nzito inayotokana na moshi wa sigara. Hali hii inamlazimu Juma kutoa tamko; fungua madirisha yote. John na Kulwa wakaitikia kwa kufungua madirisha na yule mvuta sigara akazima sigara yake. Hivyo basi katika hali hii kichocheo cha tamko la Juma ni harufu ya moshi wa sigara, kiitikio ni John na Kulwa kufungua madirisha na mvuta sigara kuzima sigara. Kwa hiyo maana ya usemi inabainishwa na mwitiko wa John, Kulwa na mvuta sigara.

Udhaifu wa nadharia hii ya kichocheo-mwitiko ni kwamba, kichocheo kimoja kinaweza kusababisha utokeaji wa viitikio viwili au zaidi. Kwa mfano mvua imeanza kunyesha, mama anawaamrisha watoto waingie ndani. Watoto wanaitikia kwa kukimbia kwenda ndani ya nyumba.
           Kichocheo……………………mvua
           Tamko………………….ingia ndani
           Kiitikio ……………….watoto kuingia ndani ya nyumba upesi.
Katika mfano wetu huu viitikio vinaweza kuwa; watoto kuchukua ndoo na sufuria na kuanza kuteka maji, kuingia ndani na kuchukua miavuli, kuingia ndani na kukoka moto (Matinde, 2012:259).

Maneno mengi katika lugha hayataji vitu vinavyoonekana, kwa hiyo basi maneno hayo hayawezi kusababisha mwitikio wa msikilizaji. Mfano wa maneno hayo ni kama vile njaa, busara, upendo, uchoyo na huruma (Alston, 1967). Hii ni kwa sababu maneno dhahania hayawezi kuelezwa kwa kutumia nadharia hii.

Pia wakati mwingine wanalugha hawaitiki maneno kwa vitu vinavyowakilisha maneno hayo (Holm na Karlgren, 1995:4). Hii ina maana kuwa kujenga maana ya kinyambo kwa kutumia nadharia ya kichocheo mwitiko inalazimisha upekee wa vinyambo au maneno husika. Ukweli ni kwamba wanajamii huitikia vitu vinavyowakilisha maneno hayo.

Aidha semi nyingi sana katika lugha hazidhibitiwi na kichocheo katika muktadha peke yake. Kwa mantiki hii nadharia ya kichocheo mwitiko inakosa mashiko kwani wakati mwingine mtu anaweza kuulizwa swali na asijibu au akajibu kinyume kabisa na swali. Kwa mfano ni kawaida kwa Mtanzania kusema nakuja wakati anaonekana anakwenda.

Nadharia ya masharti – ukweli husisitiza dhana ya ukweli katika ujasiri wa maana, hivi kwamba maana sharti iwe ya kweli na ukweli huo ubainishwe bayana. Nadharia hii iliasisiwa na wanamantiki na wanafalsafa, kisha ikafafanuliwa na wanaisimu.
Mfano (a) Ukweli wa kihistria
i/ Muungano wa Tanzania na Zanzibar 1964
           ii/ Rais wa kwanza wa Tanzania ni J. K.Nyerere
          (b) Ukweli wa maarifa ya kiulimwengu
Ukweli huu hutokana na uhalisia wa kiulimwengu ambao kila mwanajamii anakuwa nao. Mfano shairi huundwa na beti, mistari, vina na mizani au mwanamke hujifungua.
       
(a)ukweli wa kiisimu
Ukweli huu hubainishwa kupitia mfuatano wa maneno katika sentensi na usahihi wa mfuatano huo.
      i ) Hadija aliolewa na Kanyansa (sahihi)
      ii) Kanyansa aliolewa na Hadija ( si sahihi)

Nadharia hii hushughulikia sentensi arifu tu, kwa kuwa ndizo hutoa kauli ambazo zinaweza kuwa kweli au si kweli. Hivyo ni vigumu kubashiri maana ya sentensi swalifu na amrishi kwa maswali na amri haviwezi kubainisha ukweli au si kweli. Vilevile ni vigumu nadharia hii kutumiwa kubainisha ukweli au wigo wa sentensi tendezi, kwani sentensi tendezi hazielezi matukio. Kwa mfano; Ninakubali kuwa yeye si jambazi. Katika sentensi hiyo ni vigumu kuamini au kutoamini ukweli wa kauli hiyo. Sentensi moja au zaidi huweza kuibua seti nyingi za masharti ukweli hali ambayo huifanya nadharia hii kuwa na mzunguko usiokikomo katika ufasiri na ufafanuzi wa maana.

Nadharia hii hutegemea zaidi maarifa ya kiulimwengu imani, mielekeo na tajiriba pana kuhusu kila tungo. Sentensi inayodokeza maarifa ya kiulimwengu ni ya kijumla kuhusu taaluma mbalimbali kama vile; maji hayana rangi- itakuwa kweli endapo tu maji hayatakuwa na rangi. Hivyo basi ukweli huu ni wa kiulimwengu kwa sababu kila mwanajamii anakuwa nao.

Nadharia ya masharti-ukweli hujikita zaidi katika maswala ya taaluma ya mantiki na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana. Hii ni kwa sababu tu nadharia hii inajikita zaidi katika kujua maana ya neno. Kwa mfano nini maana ya kifo na ukweli ni nini. Hivyo basi kutokana na mifano hiyo hapo juu nadharia hii huenda mbele zaidi na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana.

Nadharia ya utendaji au matumizi ilianzishwa ili kutatua upungufu uliojitokeza katika nadharia zilizotangulia. Nadharia hii inasema kwamba si sahihi kuangalia maana ya neno au kisemo kuwa si kitu ambacho kinajitosheleza. Msisitizo upo wa maana ya neno hupatikana katika utumizi uliotumika, kwani neno halina maana moja. Mwasisi wa nadharia hii ni Ludwing Wittgenstein, yeye aliona nadharia hii itatoa upungufu ulijitokeza katika nadharia zilizopita (Matinde, 2012:260). Katika kitabu cha Philosophical Investigation (1963) anasema ni kosa kubwa kuangalia kama kitu au kiumbile kamili. Hivyo alipendekeza kuwa maana ya neno iangaliwe kwa kuzingatia muktadha wa neno au kisemo jinsi kilivyotumika. Kwa maana hiyo maana au kisemo ni matokeo au athari inayopatikana.

Neno moja huweza kuwa na maana nyingi kutokana na muktadha au kutokana na matumizi yake. Kwa kuangalia muktadha wa jamii kuna baadhi ya maneno ambayo huwa na maana katika jamii fulani. Kwa mfano matumizi ya tumsifu Yesu kristo huendana na muktadha wa ibada au waumini wawili hasa wa kikatoriki. Usemi huu utakapotumiwa msikitini utazua utata wa imani za kidini.

Pamoja na  ugumu uliopo katika kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali zilizojadiliwa na wataalamu wengi, kila nadharia ina ubora na mapungufu yake katika kufasili maana ya maana katika kiwango cha neno na sentensi. Kwa hiyo maaana ya maana inabaki kuwa dhana telezi kutokana na utata wa kufasili dhana hii. Ni vema tafiti mbalimbali ziendelee kufanyika ili kuziba pengo la  ugumu wa kufasili maana ya maana.

                                                   MAREJEO
Alston, W. P. (1967) Meaning The Encyclopedia of philosophy, vol 5 Macmillan  and  Free press,
                                PaulEdwards, Editor in Chief, (pp.233-241), imesomwa tarehe 11/04/2014 saa 22:00
                                kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Baron, J. (1972) Semantic Components and Conceptual development, Elsevier imesomwa tarehe 11/04/2014
                                saa 22:15 kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Bloomfield, W. L. P. (1983) Language, LondonNew york.

Filp, H (2008) What is Semantics, What is Meaning, imesomwa tarehe 11/04/2014, saa 20:00 kutoka
                                www.sciencedirect.com/science/article.

Habwe, J. na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.

Holm, P. and Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning and Different perspective on information System,
                                Stockholm University, Marburg.

Lyons, J. (1981) Language; Meaning and Context, Fontana Paperbacks.

Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,
                               Serengeti Education publishers (T) LTD, Mwanza.

Mdee, S. J. na wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21: Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne
                               Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi.

Sengo, T. S. Y.M (2009) Fasihi za Kinchi, The Regestered Trustees of Al Amin Education and Research
                               Academy, Dar es Salaam.

Wamitila, K. W, (2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia, Kenya Focus Publications LTD, Nairobi.




No comments: