Wednesday, June 19, 2013

LUMBA KISWAHILI

Uwanjani najitupa, Kiswahili kukilumba,
Talumba bila ya pupa, na ulimi kuuramba,
Kiswahili sio kapa, nawajuzeni washamba,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Kiswahili lugha yangu, tangazo nalitangaza,
Kwayo nitafungwa pingu, hadharani nawajuza,
Piga  kwa vyenu virungu, Kiswahili natangaza,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Nyumbani nitaanzia, TEKU lugha twabukua,
Twasoma fonolojia, mofoloji sintaksia,
Twajua  semantikia, isimu kuyogelea,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Kiswahili kubukua, sio njia kupotea,
Mwanga wake twaujua, gizani unatutoa,
Sokoni tutaingia, mataifa kutujua,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru,
Lugha hii ni mwanana, tumia pasi ushuru,
Mwana kaa danadana, Kiswahili ndio nuru,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Kaka dada sikieni, vyeti leo mwapokea,
Lakini jama jueni, ujuzi ni kutumia,
Si kuutia kapuni, kabatini kufungia,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Kiswahili kuenea, ni wazawa kutumia,
Kenya Uganda ingia, Rwanda Burundi vamia,
Acha bwana kusinzia, dunia soko huria,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Wahenga wanazo semi, hunena pasipo soni,
Lugha hukuza uchumi, tena hukausha kuni,
Huzirainisha ndimi, sogani na kutanoni,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Mwana utazame mwezi, usitazame kidole,
Akisemacho mzazi, tambua kaona mbele,
Maisha kama jahazi, chambua kama mchele,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

Mpira uko kambani, wanalugha shangilia,
Za kigeni zi pembeni, ushindi zashuhudia,
Kiswahili ki damuni, popote nitatumia,
Lumba Kiswahili mwana, huu ni wako uhuru.

                                                                                                       Ushauri zaidi:  hkapele@gmail.com
                                                                                                          0763-891415

No comments: