Friday, December 27, 2013

FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI, Na. Reuben.A


SWALI: FASIHI SIMULIZI YA KIBANTU INGEWEZA KUWA NI RASLIMALI MUHIMU 

fafihi simulizi ya kiswahili




KWA MAENDELEO YA JAMII. BAINISHA AMALI ZINAZO AKISIWA NA KABILA LA KIBANTU ZA TANZANIA NA VIPENGELE MUHIMU VYA UHUSIANO WAKE KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA JAMII KWA KUZINGATIA MUKTADHA MPANA WA UTANDAWAZI. MIFANO IJIKITE KATIKA KABILA LA WASAFWA NA WANYAKYUSA

Fasihi simulizi kama dhana, imeelezwa na wataalamu wengi kwa kutegemea nadharia na mitazamo mbalimbali , hata hivyo ni muhimu kufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika, mahali dhana hiyo inapotokea na hata kipindi au wakati husika. Hii ndio sababu tunapata fasili mbalimbali zinazorejea dhana ya fasihi simulizi kama ifuatavyo:

Ngure, A.(2003), anafasili fasihi simulizi kama sanaa itoayo maudhui yake kwa lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kutendwa. Kwa mijibu wa maana hii, Ngure anasisitiza kwa kusema fasihi ni namna ya utoaji wa maudhui kisanaa na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo ambayo huweza kutamkwa au kutendwa.

Mulokozi (1996:24) anasema, fasihi simulizi ni fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi, hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha (mazingira) fulani wa kijamii na kutawaliwa na mwingiliano wa fanani, hadhira, fani inayotendwa, tukio, mahali na wakati. Mulokozi anafafanua kwa kusema fasihi simulizi ni ile fasihi inayotendwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo ikiambatana na vitendo, swali ni kwamba fasihi simulizi inayowasilishwa kwa njia ya redio, tepurekoda pamoja na luninga sio fasihi simulizi?
Finnegan (1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalumu. Katika fasili hii Finnegan hajagusia mambo muhimu katika fasihi simulizi kama vile muktadha, namna ya uwasilishaji, uhifadhi na badala yake amejikita zaidi katika ubunifu alionao msanii anayeiumba fasihi husika.  

Balisidya (1983) anafasili fasihi simulizi kama aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuiumba, kuiwasilisha na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake. Fasili hii ina mapungufu kwani haijafafanua juu ya ubunifu alionao msanii katika kuikamilisha, na pia katika suala la uwasilishaji tunaweza kujiuliza kwamba je, fasihi simulizi lazima iwasilishwe kwa njia ya mdomo tu?
Hivyo basi, kutokana na fasili zote hapo juu tunaweza kufasili fasihi simulizi kuwa ni kazi ya sanaa inayotumia mazungumzo ya ana kwa ana ikihusisha utendaji na njia nyingine za mawasiliano kama vile tepurekoda, redio, luninga na vinginevyo ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Kuna tanzu nyingi za fasihi simulizi kutokana na wataalamu tofauti kuwa na mawazo tofauti tofauti, tanzu hizo zimewekwa katika makundi au tanzu kuu nne ambazo ni hadithi, semi, maigizo na ushairi.

TUKI (2004) wanafasili amali kuwa ni matendo, kazi na mazoea, hivyo kwa maelezo hayo amali za jamii ni jumla ya mazoea, kazi mbalimbali na matendo yote yanayofanyika katika jamii husika kama vile mila na desturi, utamaduni, dini, siasa na uchumi.
www.wikipedia.org/wiki, wanafasili amali za jamii kama tawi la isimu ambalo huchunguza uhusiano kati ya lugha na jamii, aidha inajihusisha na athali yoyote ya jamii kama vile desturi za watu, matazamio na muktadha katika nyanja za lugha na namna inavyotumika.
Hivyo, amali za jamii huhusisha tamaduni, mila, desturi, dini, siasa na uchumi na haya yote sharti yahifadhiwe katika uasili wake ambapo hutunzwa, huhifadhiwa, kulindwa na kuendelezwa na fasihi simulizi.
Matumizi ya utandawazi yalianzia miaka ya tisini yakimaanisha kukifanya kitu kuwa katika kiwango cha kimataifa na kukifanya kuwa wazi na kufanywa na watu wa aina yoyote duniani (www.wikipedia.org/wiki/isimu).
Kutokana na fasili hii, utandawazi unaweza kuelezwa kama njia ambayo wenyeji au taifa hufanya mambo kuwa ya kimataifa na unahusu suala zima la uchumi, biashara, teknolojia, siasa na utamaduni.
Wasafwa na Wanyakyusa ni miongoni mwa makabila ya kibantu yanayopatikana nchini Tanzania mkoani Mbeya.

Kabila la Wasafwa hupatikana katika wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, jamii hii inajishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji. Shughuli hizi ndizo zinazofanya amali zao zitofautiane na amali za jamii nyingine.
Kabila la wanyakyusa hupatikana katika wilaya za Rungwe na Kyela katika mkoa wa Mbeya, jamii ya wanyakyusa hufanya shughuli mbazo hutofautiana kulingana na sehemu wanakotoka (yaani mazingira). Wanyakyusa wa Rungwe hujishughulisha na kilimo na ufugaji na wale wa Kyela hujishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ingawa makabila haya hupatikana katika wilaya husika yaani Wasafwa kwa wilaya ya Mbeya na Wanyakyusa wilaya ya Rungwe na Kyela, shughuli za utafutaji mali zimesababisha jamii ya Wanyakyusa na Wasafwa wapatikane sehemu nyingine pia za nchi ya Tanzania.
Amali mbalimbali zinazopatikana katika makabila ya kibantu ni pamoja na mila na desturi, utamaduni, dini (imani), siasa na uchumi.

Utamaduni ni jumla ya mambo yote yanayobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo yake (Mwambusye, 2013). Katika fasili hii mambo yanayozungumziwa ni ndoa, uzazi, malezi, marika, mafunzo mbalimbali ya mazingira na shughuli zingine kama jando, ngoma na imani katika Mungu, miungu, mashetani na mizimu, vyakula, mavazi, mapambo, salamu na lugha.
Utamaduni ni mojawapo ya nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii yoyote ile kama amali mojawapo ya jamii, tamaduni zilikuwa sharti zibaki katika uasili wake katika vipengele vya muktadha, wahusika, maudhui, hadhira na fanani.

Suala la ndoa katika kabila la wasafwa waliohusika kumfundisha mwali ni shangazi na bibi ambao hasa walikuwa ndio fanani, mwali huyo alifundishwa namna ya kuishi katika ndoa pamoja na matumizi mazuri ya chakula katika familia, kwa mfano binti alifundishwa kupika chakula ambacho kingetosheleza mahitaji ya mumewe na familia yake kwa ujumla bila kubakiza na kukitupa. Katika shughuli hii mwali ndiye aliyekuwa hadhira na ukweni ndio palikuwa mahali pa kutendea na maudhui yalikuwa ni mafunzo kuhusu maisha ya ndoa na fanani walikuwa bibi na shangazi wa mwali, katika kipindi hicho mafunzo hayo yalimfundisha mwali namna ya kuishi na jamii inayomzunguka na mafunzo yote yalifikishwa kwa njia ya misemo, nyimbo na hadithi. Mfano wa nyimbo zilizokuwa zikiimbwa wakati wa mafunzo hayo ni kama vile:
                                         “Wamala yashi ingano
                                           yaleta bana yao
                                           yenye ubaba ni mama
                                           bayinzilile mwigomba”.
Wimbo huu ulimfundisha mwali kutokumaliza chakula ndani kwa ajili ya matumizi ya baadaye na kwa ajili ya wageni.

Kutokana na maendeleo ya utandawazi amali hii imepoteza uasili wake kutokana na kuathiriwa katika uwasilishaji wake, fanani yake, mahali pa kutendea na hata maudhui yake yaani mafunzo hayo katika muktadha wa utandawazi huitwa “Kitchen party” au sherehe ya jikoni (tafsiri yetu) ambayo hufanyika kwenye kumbi na fanani huwa mtu yeyote sio wale wa asili na maudhui pia yamebadilika kwani yaliyofundishwa kipindi katika kipindi kile sio yanayofundishwa leo. Hivyo amali hii imepoteza thamani yake ya kuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii.

Kimsingi katika ndoa za kinyakyusa wazazi ndio waliohusika kuwachagulia wenzi wa ndoa vijana wao, suala la utoaji wa mahari ilikuwa ni sehemu ya amali ya jamii kwa kabila la Kinyakyusa. Ili kuhakikisha usalama wa binti wa kinyakyusa bibi au shangazi waliwachunguza mabinti zao mara kwa mara mpaka siku ya ndoa, mchakato huo ulizua misemo mingi kwa mfano mzazi angeweza kumwonya binti yake ajitunze kwa kusema “Api kujoba pa kijinja” yaani heshima na mambo yako yatathibitika penye migomba.  “Pa kijinja” palikuwa ni mahali ambapo binti alipelekwa kwa uchunguzi ili kuthibitisha ubikra wake hivyo kitendo cha kumchunguza kiliitwa “Ukosya” yaani kuoshwa. Endapo binti akigundulika kuwa alishaingiliwa kimwili ilisemwa kuwa “inguku jiligilwe” yaani kuku ameliwa, hii ilisababisha binti kutolewa mahari ndogo yaani ng’ombe wachache ikilinganishwa na binti ambaye alikutwa salama yaani hajaingiliwa na wanaume yaani aliyekutwa ni bikira ambaye mahari yake ilikuwa ni kubwa. Kutokana na umuhimu huo, mabinti walilazimika kujitunza mpaka siku ya ndoa,  hali iliyosababisha mahari kuwa kubwa na heshima kwa familia husika na fahari kwa ukoo wa mwanaume.
Kwa upande wa jamii, hali hii ilisaidia wanawake kutokuchezewa na kutozaa watoto nje ya ndoa yaani “isigwana”, kwa hali hiyo uchumi wa wazazi wa binti uliongezeka pamoja na heshima  ya binti na jamii kwa ujumla.

Kutokana na utandawazi, mfumo wa elimu kuwapeleka watoto shule na mwingiliano wa tamaduni umesababisha wanyakyusa kuoana na makabila mengine,  hivyo  kusababisha amali hii kuathiriwa na utandawazi kwa kuwa hakuna tena utaratibu wa kuwakagua mabinti yaani “Ukosya”,  pia utaratibu wa kutoa mahari nao umebadilika kwani mahari ya kutoa ng’ombe imekuwa ikithaminishwa na fedha taslimu.
Hivyo basi, katika kipindi hiki baadhi ya wazazi wamekosa mahari ambazo zingewasaidia kuendesha shughuli zao za maendeleo kutokana na watoto wao kujioza wenyewe na kusababisha mahali kuwa kidogo na hivyo kuifanya amali hii kama kipengele muhimu cha fasihi simulizi kupungukiwa thamani ya kuwa rasilimali muhimu katika maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Tambiko ni utekelezaji wa ada maalumu ili kutuliza mizimu, koma au pepo, sadaka edaha, kafara, mviga, miiko (TUKI, 2004). Hivyo tambiko ni sadaka itolewayo kwa mwenyezi Mungu au miungu kwa lengo la kuomba au kumshukru kwa mambo mbalimbali yanayoikabili jamii. Tambiko katika jamii ya wasafwa ilihusisha matukio mbalimbali katika jamii kama vile magonjwa, njaa, ukame, mashambulizi ya wanyama au maadui ambavyo viliaminiwa kutokana na kuwaudhi mizimu au miungu.  Unyeshaji wa mvua kwa wakati na kiasi cha kutosha ulikuwa ni muhimu sana wakati ukame ulipotokea. Kiongozi mkuu huongoza kundi la wazee kwenda “Iganjo” yaani mahali pa kutambikia wakiwa na pombe ndani ya vibuyu vitano au sita pamoja na kuku mweusi. Siku maalumu hutangawa kwenda kuomba mvua hivyo hakuna mwanajamii anayeruhusiwa kufanya kazi yoyote. Mwene ndiye kiongozi wa ibada kwa kusihi mizimu, mfano “uposhele inguku ini, tuhanzaje hunzi hwilwepei invula itonye”, maana yake “Pokea kuku huyu tunataka nchini kuwe kweupe akiomba mvua inyeshe”.
Baada ya hapo wazee humchoma kuku akiwa na manyoya yake mpaka aive na humla na kunywa pombe. Ibada ziliweza pia kuuliza neno gumu na kushukru kwa mambo mazuri waliyoyapata. (http://www.safarilands.org/docs/jamii-ya-wasangu-tanzania.pdf).
Kwa upande wa kabila la wanyakyusa kulikuwa na tambiko kwa miungu kupitia mizimu kwa madhumuni mbalimbali na hasa walifanya hivyo kwa ajili ya kushukru endapo mwaka mzima hakukuwa na balaa lolote na kuomba msaada kama kuna tukio mfano baa la njaa, magonjwa, ukame ili kutokomeza tatizo hilo. Siku ya tambiko la kuomba mvua ilikuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuwasha moto hasa nyakati za asubuhi hadi pale “Kyungu” (Kiongozi wa matambiko) atakapowasha moto mkubwa kando ya kibanda kidogo maarufu kama “Moto ufya” hii ilikuwa ni kama ishara ya kutoa salaamu za maombi ya mvua kwa mizimu. Waliamini kuwa moto huo ukizimika muda mfupi baada ya kuwashwa basi ombi lao limekataliwa na shughuli za kuomba mvua hubatilishwa hadi siku nyingine.
Katika kufanya hivyo maeneo yaliyohusika kufanyia matambiko yaliitwa “Isyeto/Masyeto, wahusika katika shughuli hiyo walikuwa wazee maalumu, vifaa walivyotumia kutambikia ni pamoja na vibuyu, vyungu, pombe, ulezi, kuku mweusi, pesa. Ng’ombe alichinjwa kwa mwaka mara moja kwenye maeneo hayo ya masyeto kwa kuunganisha na pombe ambapo watu walitumia huko. Mavazi yaliyotumika yalikuwa ni ya kawaida. Katika kutoa sadaka zilitolewa pesa (senti) kila baada ya muda fulani na pombe ambayo kiasi fulani iliachwa kwenye kibuyu, ilikuwa ni marufuku akina mama kutafuta kuni ndani ya isyeto, katika kila isyeto kulikuwa na chifu anayehusika. Katika utambikaji pia kulikuwa na hadhira ambayo ilikuwa ni ya kitaswira yaani mizimu, fanani walikuwa ni wale wazee waliokuwa wanatambika.
Tangu utandawazi umekuwa ukishika kasi kila uchao, dini za kigeni kama Ukristo na Uislamu vimethoofisha sana utambikaji katika “Maganjo na Masyeto”, hii inatokana na watu kuomba mahitaji yao tata katika makanisa na misikiti. Matatizo mengi ya jamii yamekuwa yakielezwa kisayansi na kupatiwa ufumbuzi wa kisayansi, maingiliano ya dini za asili na hizi za kigeni huleta mtafaruku katika jamii na kupunguza mshikamano ndani ya jamii, mfano siku za matambiko, wanajamii hukatazwa wasifanye kazi yoyote ambapo kwa nyakati hizi za utandawazi watu wenye imani tofauti na matambiko huendelea na utaratibu wao kulingana na kile mmoja anavyoamini, hali ambayo huleta pia mtafaruku na migongano katika jamii ambapo pia husababisha kuharibu umoja na mshikamano wa jamii.
Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii (TUKI, 2004). Katika makabila ya kibantu uongozi katika jamii ulikuwa unapatikana kwa kurithishwa ndani ya ukoo, chifu katika eneo au jamii husika pamoja na viongozi walikuwa wanarithishwa madaraka kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya ukoo fulani, kiongozi kabla ya kustaafu alikuwa anamuandaa mtu mmoja katika ukoo wake ili atakapostaafu au kufariki atumie nafasi yake kuuendeleza ukoo. Viongozi katika makabila ya kibantu walikuwa na mamlaka ya kusema lolote katika jamii na kutekelezwa, mfano waliweza kutoa adhabu kwa mtu yeyote yule ambaye alikiuka kaida au taratibu za jamii husika.
Kwa mfano kabila la wasafwa kulikuwa na machifu wengi na kila chifu alikuwa na watu wake wa kumsaidia katika utawala wake hasa wazee wa kimila (Mafumu). Kwa kawaida chifu alichaguliwa kutokana na busara aliyokuwa nayo, uchaguzi haukufuata urithishwaji wa mtoto mkubwa tu, bali ilitazamwa busara aliyokuwa nayo mtoto huyo.
Aliyevunja sheria alipewa adhabu ya kutubu na baadaye kulipa ng’ombe mmoja kwa wazee (Mafumu). Adhabu hii ilikuwa na lengo la kuifanya jamii iweze kuishi katika mwenendo mwema na kuwepo kwa maadili katika jamii hiyo ya wasafwa.
            Ufuatao ni mfumo mzima wa utawala ulivyokuwa katika kabila la wasafwa:
MWENE
                                                         
FUMU MKUU
                                                                                                           
MAFUMU WAKUU
                                                                                                                   
MAFUMU WADOGO          
                                                  

RAIA

Kuingia na kushamiri kwa utandawazi katika makabila ya kibantu kumeharibu mfumo mzima wa uongozi au utawala ambapo kwa sasa viongozi wanapatikana kwa utaratibu wa kiserikali ambao ulitokana na tamko la serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo mwaka 1963 ambapo alifuta rasmi utawala wa kichifu nchini Tanzania.
Baada ya kufutwa kwa mfumo huu pamekuwepo na mfumo wa vyama mbalimbali vya siasa ambavyo ndio vimekuwa vikigombea uongozi katika ngazi mbalimbali ambapo vimekuwa vikisababisha machafuko ndani ya jamii na kusababisha utengano ndani ya jamii moja ambapo yote haya ni matokeo ya utandawazi.
Uchumi ni mfumo na mapato na matumizi ya watu katika nchi (TUKI, 2004:422). Kwa mujibu wa tafsiri hii uchumi ni mali iliyopatikana kutokana na amali za nchi au watu ambapo hujitengenezea mfumo wao wa mapato na matumizi.
Suala la uchumi katika makabila ya kibantu halikutofautiana katika mifumo ya uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi na uwindaji kwa kutaja mifano michache. Jamii zilifanya kazi kwa kushirikiana na kugawana mapato kwa usawa. Suala la uvivu lilipigwa vita, hivyo kila mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya kazi alitakiwa awajibike ipasavyo. Shughuli hizi zilienda sanjali na vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi kama vile nyimbo, semi na majigambo.
Tukirejea kabila la wanyakyusa kulikuwa na mitindo mbalimbali ya kulima, mkulima mmoja mmoja au kwa kushirikiana katika shughuli nzima ya kulima yaani (Ndimya), ambapo wanakikundi walilima kwa zamu katika shamba la kila mmoja aliyeshiriki katika ushirikiano huu, hivyo walikuwa wakilimiana kwa zamu mpaka mashamba yote yanamalizika. Ingawa wanyakyusa walifanya baadhi ya kazi zao kwa ushirikiano na umoja hawakuwa na jadi ya kuimba wakati wa kufanya kazi zao, badala yake wakati wa mapumziko waliimba nyimbo mbalimbali za maonyo, mafumbo au matukio yaliyokuwa yanatokea katika jamii.


 Mfano wa wimbo ulioimbwa baada ya kazi ni:
                                      “Kiongozi:    Kungwengwelela jumo jwene, jumo fiki fyakwegelaga
                                            wote:        Kungwengwelela jumo jwene, jumo fiki fyakwegelaga”.
Maana yake ni:  “Umempendelea mke mmoja huyo mwingine kitu gani kilikuolea
                              au nani alikuolea?”.
Kwa mfumo huu wa maisha katika jamii za kinyakyusa nyakati za mapumziko baada ya kazi zilikuwa ni nyakati za burudani na kubadilishana mawazo.
Wanyakyusa walihifadhi mazao yao katika ghala zilizojulikana kwa jina la “Mitenene” ambazo zilijengwa kwa matete na kusiribwa kwa kinyesi cha ng’ombe. Pia waliweza kuhifadhi mazao darini ambapo palikuwa ni usawa na mafiga, mazao hayo yaliyohifadhiwa usawa wa mafiga yaliwekwa kwa ajili ya mbegu katika msimu wa kilimo uliofuata.
Baada ya utandawazi kushamiri utaratibu wa kulima umebadilika sana kiutendaji, vifaa vya kutendea na hata namna ya kufanya shughuli nzima ya kilimo, mpaka sasa baadhi ya wakulima walio na uwezo mzuri kiuchumi wanatumia matrekta na plau (Jembe la kukokotwa na wanyama na hasa ng’ombe), wakati huo huo wakulima walio wengi bado wanatumia jembe la mkono ambapo pia wapo wanaolima wenyewe na wengine wanaajiri vibarua kwa ujira wa kutwa au kutegemea na vipimo vya shamba. Kutokana na ubinafsi huo hakuna tena ushirikiano hatimaye kutokomeza matumizi ya nyimbo, semi pamoja na majigambo ambapo hivi vipengele vilisaidia kuleta umoja na mshikamano katika kazi. Pia uhifadhi wa mazao umebadilika sana ambapo kwa sasa nafaka huhifadhiwa kwa kutumia kemikali za kisasa na kuwekwa kwenye maghala ya kisasa pamoja na kutumia mbegu zilizoandaliwa (kisayansi), kisasa zaidi. 

Uhusiano ni hali ya kuwa na fungaman, uhusiano unaweza kuwa mbaya au mzuri (TUKI, 2004:427). Kutokana na maana hii uhusiano ni sehemu ya amali za jamii kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya maendeleo katika jamii. Wabantu hutunza uhusiano mzuri baina ya familia, ukoo na jamii kwa ujumla ili kutimiza adhima husika. Mahusiano katika jamii hujidhihirisha katika utani baina ya mtu na mtu, ukoo na ukoo au kabila na kabila. Hali kadhalika salaamu, sherehe, misiba au starehe mbalimbali zilikuwa ni ishara ya mahusiano mazuri katika jamii.
Wanyakyusa wamegawanyika katika makundi makuu mawili kulingana na hali ya kijiografia, kuna wale wanaoishi bondeni yaani “Ntebela” hususani pwani ya ziwa Nyasa wenyewe huita “Nyanja” kwa maana ya bahari na wengine huishi milimani. Mgawanyo huo wa kijiografia umesababisha tofauti kubwa kiuchumi. Wanyakyusa wa bondeni ambayo ni wilaya ya Kyela wanajishughulisha na kilimo cha mpunga pamoja na mazao mengine wakati hawa wanyakyusa wa milimani hujishughulisha zaidi na kilimo cha ndizi na aina nyingine ya mazao yaliyo katika mfumo wa mizizi iliwayo. Hata hivyo kutokana na mahusiano mazuri kati yao waliweza kubadilishana bidhaa, mara nyingi wale wa milimani walibeba magimbi, ndizi na hata mahindi ili kubadilishana na mpunga au samaki hali iliyozua utani na nyimbo kati yao. Wanyakyusa wa bondeni walikuwa wanaimba nyimbo kama:
                       “Kiongozi  :  Bisile aba mwamba aba ngata inywamu
                              wote    :  Bisile aba mwamba aba ngata inywamu
                         Kiongozi   : Sokamo mu mphulo gwe kapimba ugwe
                              wote     : Sokamo mu mphulo gwe kapimba ugwe”.
Maana yake ni;     “ Wamekuja watu wa milima
                                 wenye nzinga kubwa
                                 ewe kajitu kafupi ondoka uwanjani”.
“Nzinga kubwa” ilitumiwa na wanyakyusa wa milimani ili kupunguza msuguano kichwani kutokana na uzito wa mizigo waliyoibeba kichwani. Mabadilishano ya biashara yalionesha uhusiano mzuri na kujenga undugu kati yao. Pia misemo ya utani kama vile  “Aba ngulya gwene” ulikuwa ni msemo uliomaanisha kwamba watu wa milima ambao wanaweza kula wali bila mboga. 
Katika kabila la Wanyakyusa na Wasafwa wana namna moja katika kushirikiana wakati wa misiba na matatizo mbalimbali kwa mfano, ukitokea msiba katika familia fulani kwenye jamii, jamii nzima huhusika katika msiba ule na kushirikiana katika shughuli zote za msiba huo. Wanaume na wanawake wa jamii nzima waliwajibika kushinda na kulala mahali palipotokea msiba na kila mmoja katika jamii huweza kuchangia chakula, kuni na vifaa vingine vilivyotumika katika shughuli nzima ya mazishi kama vile majembe, makoleo, mkeka na ng’ombe, hii ilikuwa ni kulingana na uzito wa msiba uliokuwa umetokea. Mbolezi ziliimbwa wakati wote wa msiba ambapo waghani walikuwa wakitaja sifa na mema ya marehemu au ukoo wa marehemu, waombolezaji wengine waliimba na kupita sehemu mbalimbali za makazi yao wakiimba na kuchangishana nafaka kwa ajili ya msiba, kwa mfano katika kabila la Wasafwa walikuwa wanaimba nyimbo kama hizi:
                                       “Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile      
                                        Kiongozi:     Ndio maana ×2
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile
                                        Kiongozi:     (Hutaja jina la marehemu au ukoo wake)
                                        Waitikiaji:   Ndio maana twinzile”.
Wimbo huu hutumika kuonyesha uhusiano mzuri kati ya jamii na ndugu pamoja na jamaa waliofiwa, wimbo una maana kuwa (Tumekuja kwa sababu tunaushiriano na nyie).
Kwa upande wa kabila la Wanyakyusa waliimba hivi:
                                       “Kiongozi:   Twalimenye naloli           
                                        Waitikiaji:  Twalimenye naloli
                                         Kiongozi:   Ukete abhandu bikulila
                                         Waitikiaji: Ukete abhandu bikulila
                                         Kiongozi:  Keta tukwenda tukulila
                                         Waitikiaji: Keta tukwenda tukulila”
Wimbo huu ulikuwa na maana kwamba kulikuwa na uhusiano mzuri kwa kusema:
                                       “Kiongozi:  Tulimjua sana       
                                        Waitikiaji: Tulimjua sana
                                        Kiongozi:   Ona watu wanavyolia
                                        Waitikiaji:  Ona watu wanavyolia
                                        Kiongozi:   Tazama tunatembea tukilia
                                        Waitikiaji:  Tazama tunatembea tukilia”.
Kutokana na utandawazi kuingia katika jamii hizi fasihi simulizi iliyotumika kama amali ya mahusiano imepoteza uasili wake katika kuihifadhi, kuwasilishwa, muktadha wake pamoja na maudhui. Katika kipindi hiki cha utandawazi nyimbo kama hizi za mbolezi zimerekodiwa katika kanda na zinaweza kuimbwa popote na wakati wowote bila kuzingatia muktadha na katika hali yoyote. Kutokana na athari hizo za utandawazi uhusiano katika jamii umedhoofika, kwa mfano mtu anaweza kununua kanda na kwenda kusikiliza nyumbani, hivyo kwa sasa hata nyimbo hizi kwenye misiba huwa zinawasilishwa kwa kutumia kanda za muziki na hivyo kupoteza uhalisia wake.

Jando na unyago ni sehemu ya malezi inayolenga kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake ya kuwa mwanaume au mwanamke ili jinsia imjenge badala ya kumvuruga. Mara nyingi wavulana huwa wanaongelea sri zao zinazowahusu wao katika makuzi yao na huwa hawataki mtoto wa kike kuzijua hali kadhalika kwa upande wa mtoto wa kike nao huwa wanamafunzo yao ambapo nao huwa hawapendi mambo wanayojifunza yajulikane kwa watoto wa kiume, mafunzo haya yaliweza kutolewa na watu wazima ambao ndio walitegemewa zaidi na jamii katika kutoa elimu ya jinsia.
Katika jamii za kibantu zilikuwa na kawaida ya kuongelea mafunzo hayo ya siri na wazee hasa babu na bibi ndio walihusika sana katika kutoa mafunzo hayo, kulikuwa na mafundisho rasmi ambayo yalikuwa na umuhimu wa kujua mapema ukweli hasa kuhusu maumbile ya binadamu. Kadri mtoto anavyozidi kukua ndivyo alivyohitaji kujifahamu kijinsia ili aweze kukomaa na hatimaye kukabiliana na shughuli mbalimbali za kijamii.

Katika kabila la Wanyakyusa walizingatia malezi ya vijana na ilikuwa ni mwiko kwa mtoto wa kinyakyusa kudeka, mama aliweza kula na watoto wa kiume chini ya miaka kumi pamoja na wale wa kike ambao walikuwa bado hawajaolewa, lengo kubwa ilikuwa ni kuwafundisha kula kwa adabu na kuheshimiana. Kwa upande wa mtoto wa kiume aliruhusiwa kukaa na mama yake akiwa na umri chini ya miaka kumi, baada ya umri huo hakuruhusiwa kukaa tena na mama yake bali aliambatana na wanaume kwa lengo la kujifunza kazi. Mgawanyo wa kazi ulizingatia umri na jinsi kwa kuwa zamani watoto wengi hawakuwa na fursa za kusoma, hivyo walipata elimu (mafunzo) kutoka kwa wazazi wao. Watoto walipofikisha umri wa miaka kumi na moja au kumi na mbili waliweza kukusanywa kutoka familia tofauti na kupelekwa mbali na wazazi wao ili kujifunza maisha na kujitegemea na hivyo kuweza kuanzisha vijiji vipya kwa kujenga nyumba kisha kuanzisha familia.
Wakati wa utoaji wa mafunzo hayo semi na nyimbo mbalimbali zilitumika na zilitolewa na wazee, kwa mfano:
                                           “ Ukukoma ingunguni”
             Tafsiri yake ni;        “Kuua kunguni” 
Msemo huu ulilenga kuelimisha watoto na kuwakomaza kuwa kuendelea kuishi kwenye nyumba ya wazazi pamoja nao na hali wakiwa wamefikia umri wa kujitegemea sio vizuri, hivyo walisisitizwa zaidi kujitegemea. (Mwambusye, 2012:23).
                                              “Ukukula kitalikitali”
             Tafsiri yake ni;        “ Kukua haraharaka lakini bila umbile na akili au hekima”.
Katika msemo huu walimaanisha zaidi kuwa mwili unakua upesi kuliko akili yaani ukuaji wa mwili hauendi sambamba na ukuaji wa akili ( Mwambusye, 2012:27).
Kutokana na mafunzo haya ya kukaa pamoja, vijana waliweza kujifunza majukumu mbalimbali na malezi ya jamii zao kwa ajili ya maendeleo ya pamoja na kuhimiza ushirikiano, kuheshimiana na kuthaminiana na hatimiye kuishi kama ndugu na jamii moja na hapo ndipo  Wanyakyusa wanapo sema:
                                            “Nkamu ju mundu”
                 Tafsiri yake ni:   “Undugu ni kufaana na sio kufanana”.
Kutokana na kushamiri kwa utandawazi, mfumo huu wa maisha umeathiriwa kwa sababu muda mwingi watoto wanakuwa shuleni na wanapofikia hatua ya kuhitimu elimu ya msingi huwa katika umri wa miaka kumi na tatu hadi kumi na sita na baada ya hapo wengine hubaki kijijini na wengi huweza kuhamia mijini.
Pamoja na hayo, hata kule vijijini hakuna tena ardhi ya kutosha kuanzisha vijiji vipya kama ilivyokuwa zamani na hii imesababisha iwe vigumu kupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo au malezi ya kijamii.
Kwa upande wa kabila la Wasafwa, mtoto alipewa elimu kwa vitendo ambapo elimu ya kwanza kabisa kwa mtoto wa kisafwa ni elimu ya kilimo, mtoto wa kiume na wa kike akifikia umri wa miaka mitano na kuendelea alifundishwa kuwa jembe ndio kila kitu, jembe ndio maisha yake, aliweza kupewa sehemu ndogo ya shamba kwa ajili ya kulima mahindi ya kuchoma, alitengenezewa jembe dogo la mpini mfupi kadri ya kiganja chake cha mkono, hivyo alifundishwa namna ya kuwasaidia wazazi wake. Mtoto wa kiume pia alifundishwa elimu nyingine na ilitolewa kulingana na kazi aliyopendelea kuifanya atakapokuwa mkubwa, mfano alifundishwa kujenga nyumba, kuchonga mizinga ya nyuki, kukamua maziwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Pia alifundishwa namna ya kuishi na mke. Kwa upande wa mtoto wa kike naye hakuwekwa mbali na mafunzo ya kumuimarisha zaidi atakapokuwa mkubwa ambapo alifundishwa kupika, kusafisha vyombo na nyumba pamoja na namna ya kuishi na mume pamoja na namna ya kulea watoto.
Hakukuwa na elimu ya marika, bali watoto wa jinsi zote waliweza kula pamoja, kucheza na kulala pamoja na watoto wengine katika jamii. Wakati wa kula, kama mtoto amesimama wima ikiwa wengine wamekaa aliambiwa aende nje amwite “Mwimilila” yaani aliyesimama, basi mtoto huyo ataita kwa sauti akiwa hajui kama anajiita yeye mwenyewe. Kwa upande wa maonyo vilitumika vitendawili kama “Inzili nu mwene” yaani sina mfalme, ambapo waitikiaji walijibu “Ulundyelele” kwa maana ya utelezi wakilenga kufafanua kuwa utelezi hauchagui mtu unaweza kumdondosha mfalme, tajiri hata masikini. Katika maisha ya sasa kitendawili hiki kingeweza kutumika kuonya watu wawe makini na tabia zao maana kuna magonjwa hatari yasiyochagua wa kubagua kama vile “Ukosefu wa Kinga Mwilini” (UKIMWI).
Kutokana na maendeleo ya utandawazi katika harakati za kupambana na maisha jamii ya Kisafwa imetawanyika na kujikita zaidi katika shughuli za watu wa makabila mengine kama vile biashara, ulinzi na hata shughuli za udereva. Ni vigumu kwa vijana wa sasa wa kisafwa kuelekezwa kuwa shughuli kuu katika kabila lao (kisafwa) ni kilimo na wakaelewa, hii inatokana na kuwa wengi wao wamesoma na hivyo kuona kuwa kukimbilia mjini na kuendelea na shughuli zingine kama biashara, kazi za ofisini tofauti na zile za jamii yao ni ufahari na hivyo kuendelea kuishi mijini na kudharau vijijini pamoja na shughuli za kilimo na hivyo kuona shughuli hiyo imepitwa na wakati.
Afya ni kuwa na hali nzuri ya mwili bila ya maradhi, uzima, siha (TUKI, 1981). Kwa ujumla afya ni hali ya kutunza mazingira kwa lengo la kumtunza binadamu asipatwe na maradhi yoyote ya kimwili ikijumuisha utunzaji wa vyanzo vya maji, masuala ya tiba, uzazi wa mpango na upatikanaji wa chakula bora. Jamii mbalimbali za kibantu zimekuwa zikitunza afya zao katika nyanja mbalimbali kama vile masuala ya tiba, maji, uzazi wa mpango na chakula bora kwa ajili ya maendeleo mbalimbali katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na mengineyo.
Katika makabila ya kibantu afya ilionekana kama ndio msingi wa maisha yao. Pia afya mbovu ilionekana kama kichocheo hasi cha maendeleo, ili jamii iepukane na maradhi hayo ilitumia tiba mbalimbali za asili, mfano kwa upande wa wanyakyusya walizingatia sana utunzaji wa vyanzo vya maji ambapo maji hayo yalitumika kwa ajili ya kupikia na kunywa, maji ya kunywa yalitokea katika chanzo chake kutoka kwenye mwinuko wa chanzo hicho na yalitiririka kupitia kifaa maalumu kilichijulikana kama “Lyubhubhu”,ambalo ni ganda la mgomba au bomba lenye uwazi mkubwa. Sehemu hiyo haikuruhusiwa mtu yeyote kuoga wala kufua na kufanya shughuli zingine zaidi ya kuchota maji tu, ilifanyika hivyo ili kutunza maji na vyanzo vyake, hivyo basi kuna sehemu zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuoga na kufulia ambapo zilikuwa mbali na zile za kuchota maji. Tiba za dawa za asili zilitumika kwa kuponya au kuzuia magonjwa yaliyojitokeza katika jamii ya kinyakyusa, kulikuwa na dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali kwa mfano “Pupwe” ni dawa ya kutibu tumbo, “Kibangula” ni dawa ya mafua, “Mingongobhele nsemwasemwa” hii ilitibu tumbo na kisukari. Pia kulikuwa na dawa ambazo ziliandaliwa na watu maarufu, hizi zilinyunyizwa kwenye mlango wa kila nyumba ili kuondoa balaa au kuzuia balaa kama magonjwa. Kitendo cha kunyunyiza kilijulikana kama “Kumisa” yaani kutoa balaa.
Wanyakyusa pia walitumia uzazi wa mpango kwa kutumia njia mbalimbali za asili ambazo hazikuwa na madhara yoyote katika miili yao, mfano wanawake walivaa dawa kiunoni ili kuzuia mimba na kuepuka kuzaa watoto wa kufuatana kwa mfululizo na kwa muda mfupi. Njia nyingine mwanamke (mzazi) alipelekwa kwa wakwe mpaka mtoto atakapokuwa na umri mkubwa  kiasi cha kumuwezesha tena mama mzazi akipata ujauzito mwingine isilete madhara katika malezi ya mtoto aliyepo. Njia hizi zote zilisaidia kupata idadi ya watoto wanaotakiwa au idadi iliyopangwa na familia husika, pia kuipa familia nafasi ya kulea mtoto aliyezaliwa.
Kulingana na utandawazi, tiba na kinga hufanyika kwa kutumia dawa za kutibu na kukinga magonjwa mbalimbali kama vile panado, septrini, kinga za kifaduro, polio, surua na mengine mengi, kwa upande wa uzazi wa mpango kumekuwepo na vidonge vya majira, vitanzi, sindano za kuzuia mimba pamoja na mipira ya kiume na kike. (Kondomu).
Kwa upande wa kabila la wasafwa, usafi wa nyumba, mwili ulitiliwa mkazo na kuwa na umuhimu mkubwa hasa kwa wanawake. Nyumba zao zilisilibwa kwa udongo wa rangi mbalimbali na kuchorwa michoro ya urembo tofauti tofauti. Mavazi yao ambayo yalikuwa ni ngozi za mbuzi zilizolainishwa kwa mafuta ya ng’ombe au mafuta ya nyonyo yalitunzwa kwa uangalifu. Kabila hili la wasafwa kama walivyo wanyakyusa walioga ndani ya vijito ambavyo huzunguka makazi yao kwani wasafwa huweza kuweka makazi yao karibu na vijito. Jamii ilikemea uchafu wa mwili kwa kutumia mafumbo pamoja na nyimbo mbalimbali, kwa mfano moja ya nyimbo zilizotumiwa kuhimiza utunzaji na usafi wa mwili kwa kuoga ni pamoja na:
                             “Uyogaje  uyogaje × 2
                             uyogaje hyena muzina uyogaje
                             Ihwili isabuni ya sumuni uyogage”.
Maana yake ni:  “Uwe unaoga, uwe unaoga
                             mama mtoto uwe unaoga
                             sasa kuna sabuni ya thumuni”.      
Suala la maji, katika jamii ya kisafwa ilitunza vyanzo vya maji, hasa yanayotumika kupikia na kunywa. Ilizuiliwa kunywesha mifugo au kukanyaga penye chanzo cha maji, maji mengi hutiririka kutoka milimani ambapo wasafwa huita “Inzalala” kwa maana ya maji yanayotiririka.
Kutokana na maendeleo ya utandawazi  siku hizi wasafwa hutumia maji ya bomba, tiba za kisasa na kusababisha dawa za asili kukosa umaarufu na umuhimu. Hivyo dawa za kisasa zina madhara makubwa tofauti na zile za asili ambazo zilikuwa ni za uhakika na zilisababisha watu wa jamii hii kuweza kuishi muda mrefu bila matatizo.
Kukua kwa sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu sana katika kuleta maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha utandawazi. Kutokana na mabadiliko haya, fasihi simulizi kama kazi ya kisanaa iliyojaa ufundi na ubunifu ndani yake haina budi kuendana na mabadiliko hayo maana hata mfumo wa maisha hubadilikabadilika katika jamii kulingana na maendeleo yanavyozidi kuimarika na kujitokeza. Hivyo pamoja na mabadiliko hayo si vyema kupuuza fasihi simulizi kwani yenyewe ndiyo fasihi kongwe na ndiyo iliyoibua fasihi andishi baada ya kugundulika kwa maandishi kwani fasihi hata kabla ya utandawazi ilikuwa na mchango mkubwa sana katika kuimarisha amali za jamii.











MAREJEO
Balisidya, M. L, (1983), Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi, kutoka kwa Mulika namba 19 (1987),
                                     Taasisi ya Uchunguzi  wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mwanbusye, D (2012), Lugha, Utamaduni na Fasihi simulizi ya Kinyakyusa, Dar es Salaam.
Ngure, A (2003), Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari, Nairobi, Phoenix Publishers Ltd.

Finnegan, R. (1970), Oral Literature in Africa, OpenBook Publishers, Cambridge.
TUKI, (1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Nairobi, Oxford University Press Ltd.

TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

www.wikipedia.org/wiki , 24/10/2013, 10:30 jioni.

www.wikipedia.org/wiki/isimu, 26/10/2013, 04:20 asubuhi.


www.habarileo.com.tz/index/makala-wanyakyusa,  27/10/2013, 03:30 asubuhi.

http://sw:wikipedia.org/wiki/maelezoyajinsia,  26/10/2013, 04:00 asubuhi.


FASIHI YA KISWAHILI


 FASIHI YA KISWAHILI

SWALI:  Je, kuna umviringo wowote katika fasihi ya mwafrika? Kama upo ni katika maeneo yapi? Rejea ujumi katika fasihi mifano yako ijikite Katika mila na desturi za wasafwa na Wanyakyusa.                                                                                       

DONDOO

          UTANGULIZI
Ø      Historia fupi ya Wanyakyusa na Wasafwa.
Ø      Dhana ya umviringo katika Fasihi simulizi.

  KIINI
Ø      Maeneo yanayothibitisha uwepo wa umviringo katika fasihi simulizi ya Wasafwa na Wanyakyusa.


        HITIMISHO
       
        MAREJEO                                                                                                                                                                                            










Wanyakyusa ni kabila linalopatikana nyanda za juu kusini magharibi mwa Tanzania tangu karne ya 10. Walitokea nchini Malawi kusini mwa ziwa Nyasa wakijulikana kama Wangonde. Kutokana na wenyeji waliowakuta (Wasafwa na Wanyamwanga) kuwaita Wanyasa jina la kabila lao lilibadilka. Waliamua kuboresha jina la kabila lao (Wanyasa) kwa kuchopeka herufi za kiongozi wao wa kidini (Kyungu) na kuwa Wanyakyusa (waumini kutoka Nyasa). Kuja kwao katika maeneo ya kabila la Wasafwa naWanyamwanga kulisababisha kutoelewana nao kwa sababu ya majigambo yao. Hata hivyo, tofauti zao zilimalizika kwa sababu ya kuungana dhidi ya biashara ya utumwa na Wangoni ambao waliwavamia wakazi wa mkoa wa Mbeya. Mpaka sasa Wanyakyusa wamechangamana sana na Wasafwa, Wanyamwanga na makabila mbalimbali ya Tanzania kutokana na shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutawala.  (www.habarileo.co.tz/index.php.makala/14765-wanyakyusa)

Aidha, Wasafwa ni wenyeji hasa wa mkoa wa Mbeya mjini na makabila mengine ni wahamiaji tu kutoka sehemu mbalimbali. Aidha, kutokana na Wahehe kupigwa sana na Wasangu wakisaidiwa na Wajerumani ambao walipigwa kibabe na katika maeneo ya Lugalo Iringa, ilisababisha Wasafwa wengi kukimbilia maeneo ya milimani. Jambo hili lilisababisha Wasafwa kuwa washamba na wachafu pia. Wasafwa wamegawanyika katika makundi mbalimbali kutegemea na sehemu wanazoishi na ndiyo maana kuna wasafwa wa Ilomba, Mbalizi na maeneo mengine. Kuongea kwao hutofautiana, wengine huongea kwa kuvuta lakini wengine kuharakisha lakini wanaelewana wote ni wamoja.  

Mviringo ni dhana inayoturudisha palepale, dhana hii tunaiona katika saa, siku, miezi, miaka na karne (Kezilahabi, 2002:165). Hivyo, umvirngo katika fasihi simulizi ya Mwafrika ni hali ya kujirudiarudia kwa tendo au namna ya nyanja za maisha, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Umviringo huu huenda sanjari na ujumi katika kazi za fasihi simulizi.

Katika eneo la utawala au uongozi umviringo unajidhihirisha katika upatikanaji wa viongozi kwa njia ya kurithishwa. Kurithishwa huku hutokea ndani ya ukoo wa mtawala. Kwa mfano utawala katika jamii ya Wasafwa ulikuwa kwa muundo wa kichifu. Familia za kichifu ziliogopwwa sana kiuchawi, na Wasafwa zamani walikuwa na imani ya uchawi sana. Pia, kulikuwa na waganga wa miti shamba wa uhakika. Zamani hizo ambapo chifu Mwanshinga mhamiaji kutoka Ukinga alipofika maeneo ya Wasafwa yeye ndiye aliyewasha moto kwa mara ya kwanza Usafwani. Pia alikuja na mbegu katika nywele zake ambazo hakuwahi kuzikata tangu azaliwe. Kutokana na maajabu hayo akatoroshwa na baba yake na kuhamia Usafwani na ndicho chanzo cha ukoo wa Mwanshinga.
          “Umwene umwinza wuwula wakupapwa ishimwene”

            “Chifu mzuri ni yule anayezaliwa kichifu”

Kwa hiyo, katika kuendeleza uongozi kwa Wasafwa ilibidi mrithi wa chifu atoke ndani ya familia ya kichifu na awe amezaliwa kichifu, mfano azaliwe akiwa ameota meno.


Vilevile simulizi za Wanyakyusa zinasisitiza utawala wa mfumo dume. Mwanaume ndiye kichwa cha familia na ndiye mwenye maamuzi katika familia.
     “Wanyakyusa wameshawahi kuwa na kiongozi mwanamke anayefaahamika
       kwa jina la Nyanseba. Inasemekana kuwa kiongozi huyo alijaribu kuweka
       utawala wa mfumo jike, lakini hakufanikiwa kwa kuwa alipinduliwa na
       wasaidizi wake ambao waliweka dola la mfumo wa utawala wa kifalme” (habarileo.co.tz)
Kwa maana hiyo umviringo katika uongozi kwa pande za makabila yote mawili unajidhihirisha kwa kitendo cha kurithishana majukumu kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Dhana ya wakati katika fasihi simulizi inaonesha umviringo na ujumi katika fasihi. Tunaiona katika saa, siku na karne. Mfano katika kabila la Wanyakyusa suala la wakati linatumika katika uvunaji wa mazao (mfunjo) kwa kila mwaka. Kwa mfano mwezi wa pili, tatu na nne ni kipindi cha mavuno ya mahindi ambacho kila mwaka kinajirudia. Kuanzia mwezi wa saba na wa nane ni kipindi cha mavuno ya maharage ambapo kipindi hiki hujirudia kwa kila mwaka. Hivyo dhana ya wakati ilikuwa inatumika kwa mtindo huo na inajidhihirisha kuwa ni mviringo kwa kuwa kila mwaka vipindi hivi hujirudiarudia.

Aidha, kumteua mchumba ni eneo mojawapo linaloonekana kuwepo kwa umviringo. Tamaduni za Kiafrika zinasisitiza kuoa au kuolewa na mtu wa kabila au dini moja. Kwa hiyo basi utamaduni huu upo hata kwa makabila ya Wanykyusa na Wasafwa kwani vijana husisitizwa kuoa au kuolewa miongoni mwa makabila yao wenyewe. Pia, hata wachumba huweza kuchaguliwa na wazazi wao lakini huteuliwa miongoni mwa makabila yao yaani Wanyakyusa au Wasafwa. Malengo ya kufanya hivi ni kulinda utamaduni na kuzuia magonjwa ya kurithishwa.
        “Tamaduni tofauti zimeangalia namana ya kutafuta wachumba au kuoa au
          kuolewa. Baadhi ya jamii uchaguzi wa wachumba hufanywa na wazazi hii
          inaweza kufanyika hata kabla ya kuzaliwa kwa mtoto” (Mbiti, 1971:135).

Pia, majina katika kabila la Wanyakyusa na Wasafwa huwa na desturi ya kurithishwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Imani yao ni kwamba mtu wa makamo jina lake hupewa mtoto mchanga azaliwaye kwa madhumuni ya kwamba tabia alizonazo mtu huyo wa makamo ambazo kwa mategemeo ya wengi ni zile nzuri hurithiwa na mtoto mchanga aliyezaliwa. Kwa mfano kama jina la ukoo ni Mwakalindile mtumiaji wa jina hilo hurithishwa kwa wajukuu wa kiume ambapo atabakia kuitwa Mwakalindile wakati mtoto wa kike atachukua au atarithi jina la bibi yake. 

Kifo na mazishi ni matukio ambayo yalikuwepo tangu zamani. Kiutamaduni wasafwa walimwogesha marehemu na kumkalisha kwenye kiti kabla ya kucheza ngoma ya msibani. Iwapo mtoto wa kwanza katika familia amefariki maiti huzikwa kwa babu mzaa mama, mtotowa pili akifariki huzikwa kwa babu mzaa baba, mtoto watatu na kuendelea ndio mali ya wazazi husika hivyo ilikuwa ni lazima kuzaa watoto zaidi ya watatu ilifamilia changa ipate mtoto wao.
                                               
           Mfano wa kaburi la Wasafwa likiwa katika umbo la duara ndani ya kaburi la pembe nne.

Sambamba na mzishi haya kufuata mila na desturi za maumbo ya makaburi, kabila la Wasafya hutumia kakavu (tarumbeta) kutoa taarifa kwa wanajamii ili waweze kujua kuwa kuna msiba kijijini.
                        
                 Mfano wa picha ya kakavu (tarumbeta) itumikayo kutoa taarifa ya msiba ikiwa

                 begani kwa mtu wa pili kutoka kulia.

Tukio hili lilijulisha jamii nzima kuhudhuria msiba nyumbani kwa marehemu ambapo marehemu alizikwa nyuma ya nyumba.
                                              
                                Mfano wa picha ya mazishi yanayofanyika nyuma ya nyumba  

Pia, Wanyakyusa wanadesturi ya kumwogesha marehemu kabla ya kumzika. Uwepo wa vipengele vinavyofanana hadi leo kunadokeza umviringo katika Fasihi simulisi zao.

Kwa upande wa kuzika Wanyakyusa walifanya ibada za kimila zikiambatana na matumizi ya unyuso nguo za kufunika maiti. Jambo hili linafanyika hadi leo na nguo hizo ni maarufu kwa jina la sanda.     
       “Marehemu walifungwa nguo iliyotengenezwa kwa magome ya miti
         Inayojulikana kwa jina la unyuso. Nguo hiyo ilitumika kumfunika
         marehemu mithili ya sanda kisha aliwekwa kwenye shimo la duara
         maarufu kwa jina la itago” (www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa).
Maumbo ya mashimo ya kuzikia kwa Wanyakyusa yanadokeza umviringo katika fasihi simulizi japo siku hizi taratibu hizi zinadorora siku hadi siku.

Kipengele cha imani na dini nacho kinagusia umviringo katika Fasihi simulizi ya Wanyakyusa na Wasafwa. Kwa asili watu hawa walikuwa na dini na imani zao za asili walisali katika miti mikubwa, mito na makaburini kama njia ya kutatua matatizo yaliyowasonga. Kuingia kwa wamisionari wa kwanza mnamo mwaka 1892 wakiongozwa na Merensky na Nauhans wakiwa na madhehebu ya misheni ya Berlin kulianza kuwabadilisha imani zao hata kabla ya kuja wamisionari wa Morovian (www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa).

Hata hivyo, wabantu hawa wanapokubwa na matatizo makubwa kama magonjwa, vifo na magonjwa mengine ambayo hushindikana kutatuliwa kanisani huamua kwenda kwa waganga wa jadi (Tembels, 1959:13). Pia Wasafwa na Wanyakyusa wa sasa bado wanaamini waganga wa jadi licha ya kuokoka. Hili linajidhihilisha wazi kwa jinsi kipindi cha Dr.Mlingolingo kinavyopata wapenzi wengi katika radio Generation FM. Mlingolingo hupokea simu za watu wengi hasa waishio mkoa wa Mbeya licha ya kuwepo kwa makanisa mengi. Dodoso za mganga huyu kwa njia ya simu hudokeza jinsi watu hawa walivyoshindikana katika maombi kanisani huamua kutaka msaada kutoka kwake. Aidha maeneo waliko na majina yao yanadokeza kuwa wapenzi wa kipindi hiki ni Wanyakyusa na Wasafwa hata waliobatizwa na kuokoka.

Vilevile kipengele cha ngoma za Wanyakyusa na Wasafwa kinaonesha ujumi wa duara. Jambo hili linadhihirishwa na jinsi ngoma zao zilivyo na zinavyochezwa. Wanyakyusa wanacheza ngoma za asili ambazo hujulikana Kama Ipenenga na Miparano. Mara nyingi Ipenenga huchezwa na wazee au machifu wa ukoo na huvalia vizuri na kucheza kwa umakini. Miparano huchezwa katika kufurahia mavuno yao. Jambo la msingi hapa ni mkao wao na vifaa wanavyotumia wakati wa mchezo ambavyo hutengenezewa dhana ya mduara. Wachezaji hushika mkongojo na kucheza kwaduara (www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa).

Kwa upande wa Wasafwa kuna ngoma zao zinazoitwa Mbeta, Ndingala, Mwadede na Bidubidu. Ngoma hizi mara nyingi zilichezwa wakati wa mavuno na mara chache wakati wa msiba (mwengulo) wa watu maarufu. Hata hivyo, zimepungua kasi kutokana na mwingiliano wa tamaduni na dhana kuwa kuchezwa kwake katika mwengulo kunazidisha haja ya kulogana ili watu wapate kula na kunywa. Jinsi wanavyocheza na vifaa wanavyotumia hudhihirisha mduara katika ngoma. Mwashinga (2012) anasema:
        “mguuni kunavaliwa njuga za chuma za duara (INSAHALA) ambazo
         zinagonganishwa kwa kufuata mlio wa pembe zinazokuwa zinapigwa
          na wanaume na kuleta mziki mzuri. Pembe hizo ndiyo jina lenyewe
          la ngoma yaani MBETA.”  

Mila ya utani imeenea sana kwa Waafrika. Watu wanavyokutana hutanina kwa maneno na vitendo huku wakizingatia masharti yanayotawala uhusiano wa utani huo. Waafrika hutaniana baina ya mtu mmoja na mwingine au kabila moja na kabila jingine. Kwa mfano Wanyakyusa wanataniana baina ya babu na mjukuu wake, bibi na mjukuu wake, pia mashemeji. Aidha, Wanyakyusa huweza kutaniana na Wahehe huku masharti ya uhusiano wa utani yakizingatiwa. Utani huu hujirudiarudia kwa kurithishwa katika jamii zao. Hivyo kufanya ujumi wa mviringo katika fasihi simulizi ya Kiafrika.

Desturi ya kula chakula kwa waafrika inatetea ujumi katika mviringo. Waafrika huwa na mila na desturi za kula chakula kwa kuzunguka mahali palipo na chombo cha chakula. Mfano kabila la Wanyakyusa ambao hula chakula chao maarufu msibani (kande) kwa kuweka katika sinia na watu wanalizunguka wakila kwa kutumia majani ya mgomba ambayo huitwa ndundu. Pia, hunawa maji katika chombo kimoja, baba huanza na watoto wa kiume hufuata. Baadaye mama hufuatiwa na watoto wa kike. Watu hula chakula kwa kutumia chombo kiitwacho lwangabya (sinia). Tendo lile la kunawa hujirudia tena kuanzia baba, mtoto wa kiume, mama na baadaye watoto wa kike. Hivyo basi kujirudia kwa tendo hilo la kunawa kabla ya kula chakula na namna ya ukaaji wakati wa kula kunadhihirisha umviringo wa fasihi simulizi ya Mwaafrika.

Aidha, Wasafwa katika desturi ya kula hutumia baadhi ya vyombo kama vile chungu kikubwa (usuyi). Chungu hiki hutumika kutekea na kutunzia maji na kuwekea pombe pia. Ungo (uveto) uliotengenezwa kwa majani na kamba za porini zinazoufanya uwe imara zaidi. Vifaa hivi hutumika kulia chakula na umbo lake huwa la mviringo na kusadifu ujumi wa mviringo katika fasihi ya Kiafrika.

Maumbo ya vitu katika fasihi ya kiafrika yanadhihirisha uwepo wa umviringo. Kutokana na umbo hilo la mviringo jamii za kiafrika ziliamini kuwa umbo hilo ni zuri. Kwa kuangalia jamii za Kinyakyusa na Kisafwa kuna vitu vyao vingi ambavyo vina umbo la mviringo. Kwa upande wa jamii ya Wanyakyusa kuna vifaa vyao vingi vya umbo la duara kama:
Kiswahili                         Kinyakyusa                                    Matumizi
       Ungo                                uluseko                                             kupepetea
       Chungu                            Syala/videko                                     kutunzia nafaka na kupikia
       Kigoda                             ikikota                                              kukalia
       Kibuyu                             ulupale                                             kutunzia maziwa
       Jiwe la kusagia                 ukwala                                             kusagia nafaka nafaka
       Kata                                 ingata                                              kujitwishia mzigo na kukalishia
                                                                                                        vyungu vya nafaka


                                           
                        Mfano wa picha ya kigoda katika kabila la Wanyakyusa (ikikota) 

                                                              
                                    Mfano wa picha ya chungu (ndeko) kwa kabila la Wanyakyusa    

Aidha vitu vyenye umbo la mviringo hupatikana pia katika jamii ya Wasafwa ambapo baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:
Kiswahili                   Kisafwa                       matumizi                                                     
      Chungu                    usayi                              kutunzia na kutekea maji na kuwekea pombe
      Ungo                        uveto                             kupepetea                                                             
      Kikapu                     ishitundu                       kuwekea vitu mbalimbali                                         
      Kikombe                  upandi                           kunywa maji au pombe

Hata nyumba za kale za Wanyakyusa zilikuwa za mduara ambapo chifu alijengewa (isyenge) na nyumba za wake zilijegwa pembeni kuzunguka nyumba ya chifu. Pia kwa upande wa Wasafwa nao walikuwa na nyumba zao ambazo ziliitwa isonze ambazo pia zilijegwa kwa umbo la duara.
                                                               
Mfano wa picha ya    msonge (insyenge) kwa Wanyakyusa, (insonze) kwa Wasafwa

Vitu vyote hapo juu kwa makabila yote vina umbo la umviringo na viliandaliwa kwa umbo hilo kwa kuwa ndilo umbo lililoaminiwa na waafrika kuwa ni zuri.

Aidha umviringo katika kazi za fasihi za Kiafrika inaonekana pia katika nyimbo mbalimbali ambazo zinaweza kuimbwa msibani au kwenye sherehe mfano harusi na ngoma. Katika kutekeleza utanzu huu wa fasihi umviringo hujidhihilisha kwa kuwa nyimbo hizo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mfano katika kabila la Wanyakyusa mara nyingi sehemu za sherehe huimbwa wimbo ufuatao:
       “lelelele amba
        Ujo tubhapele umwana
         Amba lelelele…amba
         Mungu nkomagha
         Amba lelelele…amba
         Mungu mfyundagha
         Amba lelele…amba

Tafsiri yake.
           Mtoto huyo tumewapa
           Ambaa…lelele
            Msimpige
           Ambaa…lelele
           Msimfinye
           Ambaa.lelele

Umviringo pia hujidhihirisha kwa upande wa nyimbo za Wasafwa. Mavazi yao huonekana hadi wakati huu kutokana na baadhi ya Wasafwa kuendeleza tamaduni hizo kwa mfano; kuvaa kitambaa kilichorembwa shanga (Igoyi), mguuni kuvaliwa njuga za chuma za duara (Insahala), kupuliza pembe (Mbeta).

Kuna vifaa mbalimbali vinavyotumika katika kufanya matambiko kwa kabila la Wanyakyusa ambapo hufanyika kama kuna tatizo limetokea kama vile njaa, ukame na magonjwa. Mfano wa vifaa hivyo ni pamoja na vibuyu (kata), moto, ndizi na pombe. Jamii ya Wanyakyusa ilitumia moto kama kifaa cha tambiko katika kuomba Mungu wao. Moto huu ulikokwa na chifu wakati wa kutambika na mara baada ya majibu mazuri ya maombi yao, walichukua moto huo na kurudi nao kijijini. Huko uliandaliwa moto mwingine nyumbani kwa chifu ambao ulitumiwa na wanakijiji wote kuwasha moto huo kama ishara ya kufurahia kutii maombi waliyojibiwa na miungu wao. Umviringo unaozungumziwa hapa ni moto unapozungushwa toka nyumba moja hadi nyingine.

Sambamba na hilo matumizi ya vibuyu (kata) vilivyotumika kunywea pombe wakati wa tambiko vilikuwa na umbo la duara na hata wakati wa kunywa pombe hizo walikaa mkao wa duara. Kwa upande wa Wasafwa ibada za matambiko zilifanyika kuendana na tukio lililoikumba jamii hiyo. Mfano wa matukio hayo ni njaa, ukame na magonjwa katika jamii. Kuhusu suala la ukame chifu (mwene) wa Wasafwa aliwaita wafuasi wake kujadili namna ya kulitatua tatizo hilo, wakati mwingine kulikuwako na watu waliosadika kwamba walitumiwa na mizimu kuleta taarifa juu ya jamii fulani.
       “mzimu (izimu) ni watu ambao walikufa ambao inasadikika kwamba
          nafsi zao zinarudi kwa kupitia mwili au ufahamu wa mtu mwingine
          na kutoa ujumbe kwa ndugu zao ambao wako hai bado” (Mwasinga, 2011:20)

Katika suala hili umviringo unajidhihirisha pale ambapo nafsi ya mtu aliyekufa kurudi kwa aliye hai.

Usimuliaji wa hadidhi upo katika hali ya umviringo hasa katika maeneo mbalimbali. Hadidhi hurithiwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine, hasa kutoka kwa watu wakubwa kwenda kwa watoto. Pia eneo la hadithi na mtindo wa ukaaji ni wa mviringo kwani hadithi husimuliwa wakati wa jioni wakiwa wameuzunguka moto kwa umbo la duara jambo hili hufanyika ili kumsaidia kila mtoto kushiriki katika usimulizi wa hadithi hizo. Mfano hadithi ya Kinyakyusa huadithiwa kama ifuatavyo:
“Kapango kapango:
Ijolo alipo bhabha jumo alinumwana unyambala bho akulile kafikile  akabhlilo ka kwegha, bhabha ghwake alimbulile ukuti atikulondighwa ukwegha kutali,(ikikolokyapanja)ghwegheghe unyakyusa,lelo umwene akanile ukwegha unyakyusa abhukile ikikolo kyapanja, bhoafikile munjila alimwaghile undindwana jumo bhalina mama ghwake pasi pa mpiki pakaja pa myabho.Alinganile nukulonda ukumwegha,bho alalusisye ifyuma, mama jula atile ungasosya ufyuma nafimo loli kumpimba mpaka kumyenu. Loli bhobhafikile munjila undindwana jula akanile ukusuluka alyandile ukwimba”
             “ Ghwali nyeghile kumyitu x2
              ikisu kya kutukuju kumyetu kula kula x2”
Pitasi unyambala jula alambalele nu ndindwana jula pa nyuma ngimba akalimundu lyali setano. Lyali ngoghile nukwega ubhula bhwake, undumyana jula alinkwenda nu kufwa.

Tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili;
Hadith hadithi:
Hapo zamani za kale palikuwepo na baba mmoja aliyekuwa na mtoto wa kiume. Alipofikia umri wa kuoa baba yake alimwonya kuwa sheria ya Kinyakyusa hairuhusu kuoa nje ya kabila lao lakini yeye alikataa akaondoka kwenda nje ya kabila lake. Alipofika njiani alimkuta binti mmoja na mama yake wakiwa chini ya mti nyumbani kwao. Akampenda yule binti na kuridhia kumuoa. Alipouliza kuhusu mahali yule mama akasema asitoe kitu chochote ila kumbeba hadi nyumbani kwake. Lakini walipofika nyumbani yule binti alikataa kushuka na kuanza kuimba.
      “ulinitoa kwetu x2
        Kaniweke kwangu mji wa Tukuyu, kule kwetu kule x2
Kijana yule baadaye aliamua kulala huku binti akiwa mgongoni. Kumbe hakuwa binti bali ni jini likamuua kwa kumtoa utumbo na ikawa mwisho wa maisha ya yule kijana.

Pia michezo ya watoto hudhihirisha ujumi katika umviringo wa fasihi simulizi ya Mwafrika. Watoto hucheza michezo mbalimbali kifamilia au kwa kukutana na makundi ya familia nyingine. Mfano mzuri ni mchezo ujulikanao kama Azyungule katika kabila la Wasafa, wachezaji hucheza kwa duara. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kwa mahojiano tuliyoyafanya na mzee wa Kisafwa Ndele Mengo anayepatikana katika kijiji cha Nzenga kitongoji cha Mbogo, mara nyingi michezo hii hufanyika usiku. Watoto hukusanyika kabla ya chakula cha usiku na kuimba nyimbo mbalimbali huku wakizungukazunguka. Mambo haya yamekuwa yakifanyika tangu zamani hadi sasa. Kwa hiyo umviringo katika fasihi simulizi ya kisafwa inajidhihirisha katika mduara unaotokeza katika michezo yao.
                                            

Kwa upande wa wanyakyusa kuna michezo mbalimbali ya watoto. Watoto hucheza michezo hiyo hasa wanapokuwa hawanashughuli za kufanya.baadhi ya michezo hiyo ni “salo” (mdako) na “kubhasabhasa” au “kudumbadumba”. Namna na vifaa wanavyochezea hudokeza umviringo kwani mashimo ya kuchezea huwa ya duara. Pia, michezo hii bado infanyika hadi leo. Mahojiano yaliyofanyika wakati wa kukusanya data yalidokeza kuwa watoto hucheza mdako kwa kushindana ili kujua ni nani anayeweza kupangua kete huku akidaka nyingine.

Aidha, michezo hii inakuza fikra za watoto na uwezo wa kutenda mambo mengi kwa wakati mmoja.Michezo hii bado ipo hadi sasa hasa kijijini japo kuna michezo mingine inapungua umaarufu kutokana na maingiliano ya tamaduni na utandawazi.

Kwa upande wa Wasafwa elimu ya jando na unyago ilitolewa kwa watoto wa kiume na wa kike. Binti wa Kisafwa baada ya kuvunja ungo aliwekewa ndani peke yake. Ilikuwa ishara inayoonesha kuwa binti akiwa katika siku zake haruhusiwi kupika wala kushiriki na mwenzake katika kazi yoyote ile. Mafunzo yaliyotolewa unyagoni ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii, mfano kuchota maji, kutafuta kuni porini na kulima. Ila tohara kwa Wasafwa haikuwepo. Hivyo suala hili la jando na unyago linaendelea katika baadhi yakoo na familia chache ambazo ndizo zinazoendelea na suala hili. Pia kwa upande wa kijana wa Kisafwa mara tu baada ya kubalehe naye huanza kupewa mafunzo ya jando. Akiwa mafunzoni alifundishwa namna ya kujitengemea kama vile kujijengea kinyumba chache (invanza), kuanza kwenda kwenye magita na huko ndiko anaweza akapata mchumba. Suala la tohara kwa kijana wa Kisafwa halikuwepo, lakini baada ya kuanza kujichanganya na makabila mbalimbali limeenea sana kwa watu wote. Hivyo basi kuwepo kwa jando na unyago kunadhihirisha kabisa uwepo wa umviringo wa fasihi simulizi ya Mwafrika.   

Suala la matumizi ya lugha katika fasihi za kiafrika ndani yake kuna umviringo ingawa kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia jamii hulazimika kubuni misamiati mipya ili kukidhi mahitaji yao na kuendeleza mawasiliano. Hata hivyo kuna baadhi ya vipengele vya lugha bado vinaendelea kuwa hai hadi sasa, mfano wa vipengele hivyo kwa upande wa wanyakyusa ni;
Vitendawili, mfano i . Inguku jangu jitelile mmifwa (ikinanasi)
                                    Tafsili yake : kuku wangu katagia mibani    (nanasi)
                     Mfano ii. Kunokununu pakati pakali na kuno kununu (isuba)
                                    Tafsili yake : huku kutamu katikati pachungu na mwisho patamu (jua)

Nahau ni kauli zilizojengwa kwa kutumia maneno ya kawaida lakini zinatoa maana isiyo ya kawaida. Mfano i. kinyakyusa:    ali mumbabhu
                              Kiswahili:       yuko kwenye kuni                                                                                                                                                                                  
Maana yake   yuko kwenye siku zake/ yuko mwezini                                                             
              Mfano ii. Kinyakyusa:  Ali na masusu pammilo
                              Kiwsahili:      Ana mavi ya kuku kooni
Maana yake ni binti mdogo asiyeelewa kitu.

Methali nazo huonesha wazi umviringo kwa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine, mfano wa methali ni;
              i. Kinyakyusa: Imbwele ndukama
                 Kiswahili    : Inzi kwenye maziwa
                 Maana yake: Mtu kuingilia jambo lisilomuhusu
              ii.kinyakyusa : Ingongobe jangu nduluka jikukolela bho bhukali
                 Kiswahili    : Jogoo wangu anawika kabla ya wakati
Maana yake ni kusherehekea kabla ya mafanikio.

Aidha kwa upande wa Wasafwa kumekuwa na umviringo katika matumizi ya lugha kwa kuendelea kutumia baadhi ya vipengele japokuwa kuna mabadiliko na maboresho kwa baadhi ya vipengele vya lugha. Mfano wa vipengele vya lugha ambavyo vina umviringo ni; vitendawili, nahau, misemo na methali. Mfano wa misemo Kisafwa: hwasha hwalenga (kumekucha)
                                               Nkulembela zitonela enyau (ukizubaa wajanja watachukua nafasi)
Kwa kuchunguza vipengele vyote vya lugha vilivyofafanuliwa hapo juu ni wazi kuwa umviringo unapatikana kwani kizazi kipya hupata tanzu hizo kwa kurithishwa kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
 
Umviringo katika fasihi za kiafrika hujionesha pia katika maleba/mavazi yanayotumika katika utambaji wa baadhi ya tanzu za fasihi simulizi. Ukweli wa jambo hili unajibainisha kwa kutumia kabila la Wanyakyusa na Wasafwa. Kwa upande wa Wanyakyusa kwa kawaida katika uchezaji wa ngoma kuna vifaa kama vile; njuga, mkia wa fisi, mkwiju, filimbi, kaptura na shati jeupe, ngoma za asili.

Aidha kwa upande wa kabila la kisafwa kuna matumizi ya maleba pia ambayo nao huyatumia katika uchezaji wa ngoma. Mfano wa malena hayo ni: njuga, malimba, filimbi na ngoma. Hivyo katika eneo hili umviringo unajitokeza kwa kuwa vifaa hivyo bado vinatumika hadi sasa ingawa kumekuwa na maboresho kidogo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa mfano badala ya kutumia ngoma za asili kwa sasa huweza kutengeneza muziki kwa kutumia kinakilishi na nyimbo nazo hurekodiwa kwenye vinasa sauti na kanda.

Kupambana na mfumo dume nako hudokeza umviringo katika fasihi simulizi za Wasafwa na Wanyakyusa. Kihistoria, Wanyakyusa wamekuwa wakipambana na mfumo dume tangu zamani hasa kupitia kipengele cha majina. Watoto wa kiume hurithi majina ya upande wa ma mfumo mama ilihali watoto wa kike hurithi majina ya upande wa baba zao. Simulizi zinamtaja mwanamke ( Nyaseba) aliyewahi kujaribu kuweka mfumo jike, suala hili bado linajitokeza hadi leo japo limekuwa changamani. Siku hizi wanawake wa Kinyakyusa na Kisafwa wanapambana na mfumo dume kupitia asasi mbalimbali zinazotetea wanawake nchini na ulimwenguni kwa ujumla. Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Habarileo gwiji la habari linataja juhudi hizi:
                    ……… wanawake wa kinyakyusa wanaungana na wanawake
                    ulimwenguni kote kukabiliana na changamoto ykubwa ya mfumo
                    dume na kujenga mfumo unaozingatia haki na usawa hasa katika
                    upatikanaji wa elimu, haki ya kumiliki ardhi, mali na kushika
                    nafasi za kutoa maamuzi.(www.habarileo.co.tz/index.php/makala/14765-wanyakyusa)


Kwa kuhitimisha, suala la umviringo katika fasihi simulizi ya kiafrika huweza kujitokeza katika makabila mbalimbali ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Hivyo basi si makabila ya Wasafwa na Wanyakyusa tu ambapo umviringo huweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali. Haa hivyo, kutokana na kuingia kwa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia suala hili la umviringo limeanza kupungua siku hadi siku.    


 

















MAREJEO
Kezilahabi , E.(2002), Makala ya Nadharia ya Fasihi Simulizi na Maendeleo katika Sayansi na
                                     Teknolojia, TUKI, Dar es salaam.

Mbiti, J. S. (1971), African Religions and philosophy, Heinemann Educational Book Ltd, Nairobi.

Msokile, M. (1992), Misingi ya Hadithi Fupi, Dar es Salaam University Press, Dar es Salaam.

Mwanshinga, S. P. (2012), Wajue Wasafwa Kutoka Mbeya.

Ngure, A. (2006), Fasihi Simulizi Kwa Shule Za Sekondari, Phoenex publishers Ltd, Nairobi.

Tembles, P. (1954), BantuPhilosophy, Presence Afrcaine Kutoka
                        www.aequtoria.be/temples/BiblioDetemplesEnglish.html. 16.10.2013 saa 15:00

                                                     

www.safarilands.org/docs/jamii-ya -wasangu-tanzania.pdf.20/10/2013 saa16:30.