Friday, April 18, 2014

VISIMA VYA SHAABAN ROBERT

VISIMA
VYA
SHAABAN ROBERT

Na nianze kwa salaamu, salamu ni yangu jadi,
Pokea zangu salamu, usitie ukaidi,
Nyote kwangu ni muhimu, hakuna aliyezidi,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Hapa nitapaanzia, pengine kuelekea,
Tega sikio sikia, akilini kuyatia,
Moja mbili naingia, tayari kukuambia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha kwanza kufikirika, kisa mwana mfalume,
Mkuu mwana kataka, si binti bali kidume,
Waganga wakaitika, kwa kasi kama umeme,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Wakatoka wa kusini, magharibi wakafika,
Hata wa kasikazini, kipenga kiliwafika,
Mashariki sikioni, ngoma zilitetemeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Uponyaji kwa kafara, baraza lilitamka,
Ujinga kweli hasara, nchi iliharibika,
Waganga waso busara, miti mifugo kufyeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shujaa Utubusara, akili alitumia,
Kuiondoa hasara, nchi ilokusudia,
Hakuyataka madhara, kama yaliyotokea,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha pili ni cha Adili, mgawo kisa kikuu,
Kisima chao ahali, na mambo yao makuu,
Wema kweli ni asali, twairamba wajukuu,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Dunia kamwe si mbaya, wala haina makucha,
Binadamu tu wabaya, twasemana kutwa kucha,
Wema hushinda ubaya, Adili hakuuacha,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Busara kubwa kichwani, haina katu faida,
Kama hauna moyoni, wema na njema ibada,
Utatoswa baharini, ndugu acha ya husuda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Adili kashinda vita, kwa kutenda yalo mema,
Wema kwako nauleta, uwe baba naye mama,
Tenda pasi na kusita, imara mja simama,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha tatu binti Saadi, wasifu chaelezea,
Hiki kweli ni samadi, kipandwacho kinamea,
Giza linapokuzidi, kuchwa kuna karibia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti aliuza vyungu, mjini akaingia,
Maisha yale machungu, binti alivumilia,
Alitaka cha uvungu, kuimba aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti alikuwa mwema, kwa watu wa rika zote,
Mema aliyoyachuma, yalifika nchi zote,
Siti kaacha alama, hakutenda kwa kitete,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maisha kweli matendo, nini mja umetenda?
Singizi zaole vundo, waloshinda wametenda,
Epuka kuwekwa kando, kapambane tayashinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Rangi haina nafasi, katika kufanikiwa,
Mshipi utie tasi, kijana hujachelewa,
Hakuna jambo jepesi, liwezalo kimbiliwa,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti hakuwa Mtanga, watu wote tambueni,
Siti alitangatanga, mwisho yuko vitabuni,
Siti alitoa mwanga, nyayoze tufuateni,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maji ya kisima hiki, matamu nakuambia,
Utamu haufichiki, Shabani katwandikia,
Jitenge na unafiki, heri itakufikia,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Nne ni maisha yake, humo ninaogelea,
Alitupenda wenzake, tawasifu katwachia,
Tuzifate nyayo zake, wema kuushangilia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kayamimina, Robert kasisitiza,
Alimpenda Amina, hata katika jeneza,
Alipenda wake wana, Shabani hakujikweza,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Alichapa zake kazi, kwa makini na stadi,
Aliheshimu wazazi, hakutenda ukaidi,
Aliwapenda wakazi, alitimiza ahadi,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Penzi bora katangaza, katika yake diwani,
Kisima chatuliwaza, mitungi kutwa vichwani,
Umpendaye  utamwaza, siku zote maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kitu azizi, mja hilo litambue,
Usiitende ajizi, mwenzio mtamkie,
Mambo uyaweke wazi, wabukuzi wabukue,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Kisima kusadikika, njiani alikichimba,
Kwa wema katualika, wema ni la kwetu shamba,
Wavua pweza huvuka, katika wao mwamba,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siku ya watenzi wote, shabani aliandika,
Bara visiwani kote, watenzi walizinduka,
Hawakuzicheza kete, siku wakaiitika,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

K’elelezo cha fasili, ni ubora wa Shabani,
Kimebaini vivuli, kweli ndoa ni kanuni,
Ameiandika kweli, fumbo kuu maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shabani taa angavu, nani asiyeijua,
Shabani mvumilivu, vitabu katwandikia,
Shabani bwana shupavu, popote aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Utubora mkulima, kilimo alihimiza,
Alirudi himahima, mjini alikubeza,
Imara alisimama, uchumi kaukweza,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Shaabani liandika, jitu jinga ni hasara,
Usiweke ushirika, hilo halina busara,
Zinduka dada kaka, badili zako fikra,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Nitatia umakini, visimavye  kuvilinda,
Sintotia ufitini, mbegu bora kuipanda,
Aliimba ufukweni, kiswahili kukilinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

                                                            Kapele harry, simu 0763891415/hkapele@gmail.com

No comments: