Sunday, May 18, 2014

KONGAMANO LA KENYA - 2014

    TANGAZO!!!

CHAMA CHA WANAFUNZI WA KISWAHILI VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI
                                        (CHAWAKAMA)

KINAPENDA KUWATANGAZIA WANACHAMA NA WADAU WOTE WA KISWAHILI KUWA:

KONGAMANO LA KUMI (10) LA KIMATAIFA LA KISWAHILI NA MKUTANO MKUU LINATARAJIWA KUFANYIKA NCHINI KENYA TAREHE 21/08/2014 – 24/08/2014.

KUHUSU NCHI - KENYA

KUHUSU CHUO - LAIPIKIA

KUHUSU TAREHE - 25/08/2014 HADI 27/08/2014

KUHUSU SIKU YA KUWASILI- 24/08/2014

KUHUSU GHARAMA ZA KONGAMANO

·         MALAZI KWA SIKU NNE - TSH 12,000
·         CHAKULA -TSH 24,000
·         FULANA -TSH 15,000
·         CHETI CHA USHIRIKI -TSH 4,000
JUMLA YA GHARAMA = TSH 55,000

GHARAMA ZOTE HAPO JUU ZIKABIDHIWE KWA KIONGOZI WA TAWI KABLA YA 20/07/2014.

KUHUSU NAULI: KILA MSHIRIKI ATAJITEGEMEA KWANI MAZINGIRA YA MWANZO WA SAFARI YATATEGEMEA NA MSHIRIKI ANAKOSOMA AMA ANAKOISHI. ILA MCHANGANUO WA NAULI NI KAMA IFUATAVYO:

WASHIRIKI WATAKAOANZIA SAFARI DAR ES SALAAM, MOROGORO WANATAKIWA KUANDA TSH 134,000 KWENDA NA KURUDI, AMBAPO WASHIRIKI TOKA MBEYA WATATAKIWA KUUNGANA NA WASHIRIKI TOKA DAR ES SALAAM, MOROGORO, IRINGA, DODOMA, NA MIKOA JIRANI. KWA WASHIRIKI WA MWANZA TSH.114000 WAO WATATAKIWA KUPITIA MPAKA WA UGANDA HIVYO SI MUHIMU KWAO KUPITIA DAR ES SALAAM. Arusha tsh.54000 kwenda na kurudi.

KUHUSU HATI YA KUSAFIRIA (PASIPOTI)

KILA MWANACHAMA ANATAKIWA KUWA NA HATI YA KUSAFIRIA KATI YA HIZI:
Ø  HATI NDOGO (PASIPOTI NDOGO) TSH. 10,000
Ø  HATI KUBWA YA KUSAFIRIA (PASIPOTI KUBWA) TSH.50,000
KILA MMOJA ATALAZIMIKA KUFIKA OFISI ZA UHAMIAJI ZILIZO KARIBU NA MAKAZI YAKE ILI KUKAMLISHA MCHAKATO WA HUO.



           KAULI MBIU YA KONGAMANO NI
“KISWAHILI MALIGHAFI YA UMOJA WA AFRIKA MASHARIKI”

Kauli mbiu hii inalenga kuhimiza umoja na utangamano wa nchi za Afrika Mashariki.Lugha ya Kiswahili ina mchango mkubwa sana katika kuleta utangamano,umoja na mshikamano mwema baina ya nchi za Afrika Mashariki.Kando na mchango wa  Biashara,Michezo na Elimu.Swali ni je,Lugha ya Kiswahili ina mchango wowote katika mchakato wa kuimarisha na kukuza vipengele hivi vitatu; umoja,utangamano na mshikamano.

MADA ZA KONGAMANO

1.   Kiswahili ni lugha mwafaka ya umoja wa Afrika mashariki.
2.   Nafasi ya lugha ya Kiswahili katika tamaduni za nchi za Afrika Mashariki.
3.   Kiingereza au Kiswahili? Katika mwamko mpya wa Afrika Mashariki huru.
4.   Kiswahili na michakato ya kisiasa katika nchi za Afrika mashariki.
5.   Nafasi ya Kiswahili katika sanaa ya kisasa (Karne ya ishirini na moja).
6.   Mchango wa lugha ya Kiswahili katika upanuaji na uendelezaji wa elimu
      ya juu Afrika Mashariki.
7.   Kiswahili na uimarishaji wa usalama katika ubia Afrika mashariki.
8.   Changamoto za kisiasa,kiuchumi na kiusalama katika lugha ya Kiswahili,
9.   Ubunifu na talanta katika uzalishaji wa kazi mufti ya fasihi ya Kiswahili
                        Lugha ya Kongamano:

Lugha rasmi ya Kongamano ni Kiswahili. Makala yaliyoandikwa kwa Kiingereza yatakubaliwa tu iwapo hapana budi.wajumbe wanashauriwa kuanda makala yao katika lugha ya kiswahili
Ikisiri: Ikisiri za kati ya maneno 200-300 zitumwe kabla ya tarehe 30 Mei 2014 kwa Mratibu wa Kamati ya Maandalizi kupitia barua meme kwenye anwani ifuatayo:Billysakwa@gmail.com,AU Mhariri
Mkuu godwinalex664@yahoo.com (+255718252853) au kwa katibu mkuu wa chawakama Afrika mashariki Ahamadi Jumbe. Chawakama.am@gmail.com.
Makala: Makala kamili ya ikisiri zitakazokubaliwa yatumwe kwa Mratibu kwa baruameme kufikia tarehe 30 Juni 2014 kupitia anwani ifuatayo: Billysakwa@gmail.com
Ili kupata nafasi ya kuwasilisha makala uliyoandaa ni lazima.mjumbe atume ikisiri na hatimaye makala kamili ya mada aliyoandaa.Makala haya yatachapishwa katika chapisho la makala la kongamano kabla ya tarehe 15 Julai 2014 .utaratibu na mpangilio wa uwasilishaji utatolewa tarehe 30 Julai 2014.



                         “KISWAHILI MALIGHAFI YA UMOJA WA AFRIKA MASHARIKI











Saturday, May 3, 2014

NADHARIA ZA MAANA

Habwe na Karanja (2007:204), Crystal (1987), Matinde (2012), Ogden na Richards (1923), wanakubaliana kuwa neno  maana lina fahiwa nyingi, linaweza kudokeza sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelekezo, ufafanuzi, kufaa na ukweli. Kutokana na ugumu uliopo katika kufafanua maana ya maana, wanaisimu wamefafanua aina kuu mbili za maana ambazo ni maana ya msingi na maana ya ziada. Utetezi wa nadharia hii umesababisha kuibuka kwa nadharia mbalimbali ambazo zinajaribu kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali, ambazo chimbuko lake ni wanaisimu, wanafalsafa, wanamantiki na wanasaikolojia.

Nadharia ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo fulani (Mdee na wenzake, 2011). Kwa msingi huo nadharia hubeba mawazo, dhana au maelezo yatolewayo kwa nia au kwa lengo la kueleza hali fulani, chanzo, muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.

Sengo (2009:1) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani. Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira na mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni. 

Nadharia za maana ni miongozo ambayo hutambulisha mbinu mbalimbali za kujifunza namna ya kufasiri maana katika lugha (Matinde, 2012:247). Katika kufafanua maana nadharia zinazohusika ni nadharia ya urejeleo, dhana au taswira, matumizi, uelekezi, masharti‒ukweli, kichocheo‒mwitikio, na vijenzi Semantiki.

Ufuatao ni ugumu unaojitokeza katika kufasili maana ya maana kwa kuzingatia nadharia za maana kama zinavyo pambanuliwa.

Nadharia ya urejeleo iliasisiwa na Ogden na Richards, wanafalsafa hawa wanadai kuwa maana hujitokeza pale palipo na kirejelewa chake (Lyons, 1981). Waasisi wa nadharia hii wanadai kuwa lazima kuwe na kirejelewa. Mfano mtu kipo kitu kinachorejelewa, waasisi hawa waliibuka na dhana ya pembe tatu ili kueleza nadharia yao kama inavyoonekana hapa chini.







                                        Dhana (fikra)
                                                         

              Umbo la isimu                          kirejelewa (kitaje)

Kuna umbo la isimu kama kitaja neno, misemo, kauli au sentensi na vitu hivi hufanya tujenge dhana akilini. Dhana hii ndiyo inatufanya tupate kirejelewa, kuna uhusiano imara kati ya umbo la isimu na dhana. Dhana na kirejelewa akilini hakuna uhusiano imara kati ya umbo la isimu na kirejelewa, kiunganisho kati ya neno na kirejelewa katika dunia halisi bali ni fikra tu (Matinde, 2012).

Ugumu unaojitokeza katika kueleza maana ya maana katika nadharia ya urejeleo ni kwamba si kila kinyambo au leksimu yenye maana ina kirejelewa chake (Austin, 1970). Ni dhahiri kuwa pamoja na kuwepo kwa maneno mengi yenye virejelewa vyake kuna baadhi ya maneno yasiyokuwa na virejelewa. Nomino dhahania hubeba maana fulani katika jamii ya watu. Kwa mfano Mungu, malaika, jini, shetani, njaa, upole, upepo, hasira na furaha ni vinyambo vyenye maana ijapokuwa havina kirejelewa kama nadharia inavyodai. Kukosekana kwa kirejelewa kunasababisha utata au ugumu katika kufasili maana kwa kuzingatia nadharia ya urejeleo.

Kielelezo 2

         Umbo la isimu↔ dhana ↔kitajwa
               ↓                ↓                   ↓
             Mungu        X            – mwenye kuumba ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake.
                  
Upepo             X            − hewa isiyotulia na aghalabu huenda kwa kasi.

Pia nadharia hii inapata ugumu wa kufasili maana ya maana kwa maneno yenye uhusiano wa kihomonimia ambapo kuna baadhi ya maneno yanayorejelea zaidi ya hali au kitu kimoja (Matinde, 2012:252). Kwa mfano    paa [+ondoa mamba ya samaki kwa kuparuza kwa kitu kama kisu]
   [+enda juu]
   [+chukua baadhi ya makaa ya moto weka mekoni]
  [+mnyama wa porini anayefanana na mbuzi aliye        mwembamba sana]


Kaa [+kipande cheusi cha kuni kilichochomwa na kuzimwa kabla ya kuwa majivu]
[+mnyama mdogo wa majini mwenye miguu sita au zaidi]
[+kuweka matako au makalio juu ya kiti]

Panda [+mgawanyiko katika kitu]
           [+pembe kubwa na ndefu iliyotobolewa tundu katika              ncha yake inayopigwa katika ngoma au kutoa
             taarifa]
           [+paji la uso]
           [+enda kuelekea juu ya kitu]
           [+weka mbegu au mche katika ya ardhi ili ikue]

Kutokana na mifano hiyo hapo juu ni dhahiri kuwa kwa kutumia nadharia hii ya urejeleo ni vigumu kufasili maana ya maana kwa kuwa neno paa, panda na kaa hurejelea fahiwa nyingi.

Nadharia ya urejeleo haifanyi kazi kwenye maneno yenye uhusiano wa kipolisemia (Holm na Karlgren, 1995:3). Polisemia ni maneno ambayo yana uhusiano kimaana, na mara nyingi maana ya maneno huwa imepanuka kadri ya mpito wa wakati. Mfano wa maneno kama vile;
Kichwa [+ cha binadamu]
              [+ kama kiongozi]
Jicho      [+ la sindano]
              [+la binadamu]
mguu     [+wa binadamu]
              [+wa gari]

Kutokana na mifano ya maneno hayo hapo juu, nadharia ya urejeleo haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kipolisemia. Kwa sababu waasisi wa nadharia ya urejeleo wanadai kuwa katika urejeleo lazima kuwe na kirejelewa kimoja na jina moja tu, lakini maneno yenye uhusiano wa kipolisemia huwa na kirejelewa zaidi ya kimoja ambavyo huweza kurejelea maana tofautitofauti.

Maneno kama vielezi, na vihusishi yanakosa maana katika nadharia hii (Filp, 2008:20). Kwa mujibu wa wanaurejeleo maana ya neno ni kitu kinachorejelewa na neno husika, kwa msingi huu maneno ni majina ambayo hutaja vitu. Aidha dhana hii inaonesha kuwa maneno yasiyokuwa nomino kama vile vielezi na vihusishi hayana maana, jambo ambalo halina ukweli. Hii ni kwa sababu lugha yoyote inajumuisha aina mbalimbali za maneno na si majina tu.

Nadharia hii haiwezi pia kufafanua maana katika kiwango cha sentensi, ambapo sentensi ni tungo inayojitosheleza kimaana, kimsingi huhusisha na mtendaji, neno sentensi haliwezi kufafanuliwa na kupata urejeo sentensi.kwa mfano (a) Mwalimu anafundisha darasani
(b) Juma anapika ugali
Katika sentensi hizi urejeleo wa maana ya sentensi nzima hauwezi kupatikana.


Aidha nadharia ya uelekezi ni dira ambayo waasisi wake wanadai kuwa, njia nzuri ya kufafanua maana ya kitu au dhana ni kusonta kwa kidole kile kinachorejelewa (uelekezi kwa kutumia kidole) (Matinde, 2012:252). Ni muhimu kuelewa  kuwa kalamu ni nini, na mbuzi nini na kuelewa kuwa umelenga kalamu nzima na mbuzi mzima na wala si sehemu tu ya kitu. Hivyo basi nadharia hii ya uelekezi inapata ugumu wa kufasili maana ya maana kama ifuatavyo;

Baadhi ya maneno katika lugha hayawezi kufafanuliwa kwa kusonta kidole ( uelekezi kwa kutumia kidole), mfano usingizi, urafi, njaa, hekima na busara. Kwani unaposonta kidole tumboni tunaweza kupata fahiwa mbalimbali kama vile njaa, shibe, ujauzito, minyoo na utumbo.

Pia nadharia hii ni ya kidhahania kwani huakisi tu kuwa anaye elekezwa anaufahamu au maarifa awali kuhusu kile kinachorejelewa. Mfano inatuwia vigumu kumfafanua ng’ombe kwa kusonta kidole kwa mtu asiyekuwa na maarifa ya awali ya ng’ombe kuwa anasifa zipi.

Aidha sababu za kiutamaduni huweza kuleta ugumu katika matumizi ya nadharia hii katika ufasiri na ufafanuzi wa kile kinachorejelewa. Mfano sehemu nyingi nchini Kenya neno mchele hurejelea uliopikwa na ambao haujapikwa, tofauti na Tanzania ambapo neno mchele hurejelea usiopikwa tu, na mchele uliopikwa huitwa wali. Hivyo ni vigumu kufafanua maana ya maana kwa kutumia nadharia hii ya uelekezi.

Nadharia vijenzi semantiki ni nadharia inayopambanua leksimu au vinyambo vilivyo katika kikoa kimoja cha maana kwa kutumia seti isiyo na ukomo (Baron, 1972). Kwa kigezo hiki sifa za leksimu hupambanuliwa kwa kutumia alama ya kujumlisha (+) inayodokeza uwepo wa sifa hiyo na alama ya kutoa (-) inayodokeza kutokuwepo kwa sifa tajwa. Aidha sifa bainifu za leksimu moja huitofautisha na leksimu nyingine.

Kutokana na matumizi ya mbinu ya uwili kinzani kutofaa katika leksimu ambavyo vijenzi vyake havibainishiki kwa urahisi, maana ya maana bado ni tata. Alama kinzani (+ na -) haviwezi kuwa na uzito katika aina zote za maneno kama vile vihusishi na vinganishi vinapotumiwa kufasili maana ya maneno husika. Kwa mfano ni rahisi kufasili neno mvulana kwa kutumia kijenzi MTU, MTU MZIMA na ME kwa kutumia alama + au lakini ni vigumu kubaini vijenzi semantiki katika kufasili kiunganishi kwa.  

Pia kutokuwepo kwa vigezo vya uteuzi wa vijenzi, kunatatiza fasili ya maana kwa kuzingatia nadharia ya vijenzi semantiki. Nadharia hii haiweki wazi sana kilichozingatiwa katika kuteua vijenzi husika wakati wa kufasili leksimu mbalimbali. Kwa mfano kijenzi ME kinatumiwa katika ufafanuzi wa leksimu zinazohusu binadamu na udugu. Jambo hili linatatiza na kuibua hisia zisizo na jibu la haraka kama kusahaulika kwa kijenzi KE, ni mfumo dume au la. Aidha matumizi ya vijenzi mlalo na mfuatano katika fasili za udugu hauzingatii umbali au ukaribu. Kwa mfano ndugu wa tumbo moja (kaka au dada) si lazima wafuatane kwa karibu.

Vile vile hakuna ukomo wa vijenzi katika fasili ya leksimu, pamoja na nadharia hii kufanikiwa kubainisha vikoa maana katika lugha, hakuna uthibiti wa idadi ya vijenzi vinavyotumika. Leksimu moja katika lugha inaweza kuwa na idadi tofauti ya vijenzi semantiki ukilinganisha na neno jingine katika lugha ile ile. Kwa mfano neno mvulana linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi [MTU], [MTU MZIMA] na [ME], wakati neno kaka linapambanuliwa kwa kutumia vijenzi semantiki [ME], [MZAZI], [MLALO] na [MFUATANO]. Tofauti hii ya vijenzi semantiki kutoka neno moja na jingine inazua uvulivuli wa kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia ya vijenzi semantiki.

Aidha uwepo wa orodha ya vijenzi semantiki vya jumla vinavyotumiwa katika kufasili vinyambo vya lugha mahususi unakosa uthibitisho. Hii inatokana na ukweli kwamba kila lugha ina kanuni zake mahususi. Hivyo, ujumla unaosisitizwa na wanadharia ya vijenzi semantiki ni wa kutiliwa shaka kwani lugha inaweza kutofautiana na lugha nyingine katika vijenzi-semantiki kutokana na utamaduni wa jamii husika.


Nadharia ya dhana au taswira iliasisiwa na wataalumu wa isimu ambao ni Sapir na Desassure (Ogden na Richards, 1923). Ambapo msingi wake mkuu unaeleza kuwa maneno ya kiambo ni dhana au taswira inayoibuliwa na kiambo hicho akilini mwa mwanalugha wakati kiambo hicho kinapotumika. Kwa mujibu wa nadharia hii maana ya neno, kisemo na sentensi hujengeka akilini mwa msikilizaji au mzungumzaji. Kwa mfano tunaweza kuwa na NENODHANA. Nadharia ya dhana huhusisha moja kwa moja maana na wazo, taswira au hisi badala ya kuhusisha maana na kitu moja kwa moja. Pia husaidia kutoa majibu ya vinyambo visivyoweza kurejerewa kama vile: Mungu, shetani, upepo, njaa, usingizi, upendo na furaha, kwa kuwa nadharia ni wazo kuu linalomwongoza mtu ama jamii kutenda jambo fulani, ni dhahiri kuwa nadharia ya dhana humwongoza mwanalugha kuhusisha maana na wazo, taswira au hisi. Kutokana na upungufu wa nadharia hii upo utata au ugumu wa kufasili maana ya maana kwa sababu;

Dhana ya picha au taswira si bainifu na haiwezi kuchunguzika na kutabiri chochote. Huwezi kutabiri maana ya neno wala kufanya utafiti wa aina moja. Kwa sababu maana ya kiashiria hutokana na picha au taswira zinazojengeka akilini mwa mwanalugha. Hivyo maana ya maana inabaki kuwa telezi kwa kuwa kila kiashiria kinajengewa maana kulingana na picha iliyojengeka akilini mwa mwanalugha. Kwa mfano, kiashiria kiti kinaweza kujengewa picha tofauti akilini mwa mwanalugha kulingana na mazingira au uzoefu wa mwanalugha huyo. Kielelezo kifuatacho kinaonesha ni kwa namna gani picha ya kiti inaweza kuwa na maana mbalimbali kulingana na picha ya mwanalugha aliyoijenga akilini mwake.
Kiashiria                                        Taswira au picha
KITI                                              - kiti cha ofisini
                                                       - kiti cha kinyozi
                                                       - kiti cha umeme
Picha kama hizi zinajengwa na mwanalugha huku akiwa anafahamu kuwa kiti ni kifaa kilichotengenezwa kwa kutumia mbao, kwa ajili ya mtu mmoja kuketi, kina miguu minne, kina sehemu ya egemeo la nyuma. Ugumu wa kufasili maana ya maana unakuja pale mwanalugha anapokuwa na picha au taswira ya kiti chenye mguu mmoja na kile chenye miguu mitatu. Pia kiashiria nyumba kinaweza kuwa mfano wa kiashiria chenye kujengewa picha tofauti tofauti akilini mwa mwanalugha. Ikiwa nyumba ni jengo ambalo limekusudiwa kukaliwa na watu. Utata unakuja pale mtu anayejua kuwa banda ni nyumba ambayo hutumika kuwekea vitu au wanyama.

Aidha, picha za akilini ni dhahania ya kutosha kuweza kuwakilisha maana za nomino au vitenzi vya kawaida. Dhana anayoijenga mtu akilini mwake haiwezi kufumbata maana ya kitu halisi. Kwa mfano, mtu anaposikia neno mbuzi, dhana itakayojengwa inaweza kuwa dhana ya kiumbe mnyama, kiumbe hai, kifaa cha kukunia nazi, kiumbe mwenye miguu minne. Maana inayojengwa hutegemea zaidi ukomo wa fikra zake. Aidha utofauti katika uwezo wa kujenga dhana akilini juu ya leksimu fulani unapunguza maana ya kitu kinachojengewa dhana.

Hakuna picha ya jumla ya mguso katika nadharia ya dhana au taswira, kwani kila mwanalugha hujenga picha akilini mwake kulingana na imani yake, uzoefu wake, na mazingira yake (Holm na Karlgren, 1995:6). Katika majina au nomino dhahania mwanalugha hawezi kuvigusa viashiria ila huvijengea picha viashiria hivyo akilini mwake kama vile kiashiria shetani hakina mguso. Hakiwezi kuonekana wala kushikika bali mwanalugha hujenga picha akilini mwake kuwa kiashiria shetani kina maana ya kiumbe mwenye pembe ndefu, mbaya wa sura, kiumbe wa kutisha, tena mtoa roho za watu ambaye kwa hakika ni laghai lakini pia shetani kama kiumbe anaweza kujengewa picha na mwanalugha kuwa ni mtu yeyote mwenye matendo mabaya. Kutokana na ujengaji wa picha au dhana akilini mwa mwanalugha inakuwa vigumu kueleza maana ya maana kutokana na ujenzi tofauti wa picha katika akili ya mwanalugha.
  
Pia ugumu wa kueleza maana ya maana unakuja pale tu ambapo nadharia ya dhana inadai kwamba kila kinyambo kina husiana na taswira wakati si kila kinyambo kinahusiana na taswira (Holm na Karlgren, 1995:3). Kwa mfano, kinyambo kama vile ingawa, lakini na japokuwa havina taswira ambayo mwanalugha anaweza kuijenga akilini mwake. Hivyo basi kutokana na ugumu huu wa baadhi ya vinyambo kukosa taswira kunakuwa na utata wa kueleza maana ya maana kwa kutumia nadharia ya dhana au taswira na kuifanya maana ya maana kubaki kuwa dhana telezi tu.
 
Haiwezi kuelezea vinyambo viwili kuwa vyaweza kuwa visawe. Taswira au dhana inayojengwa akilini kuhusishwa na kinyambo kimoja tu haiwezi kukubalika kwani inaweza kuvitenga visawe kwani si kila dhana inawakilishwa na neno moja tu (Matinde 2012:256). Kwa mfano badala ya kusema nyati mwanalugha mwingine anaweza kusema mbogo, chumvi kuwa munyu, dagaa kuwa kauzu, tembo kuwa ndovu.  Uwepo wa visawe unadhihirisha udhaifu wa nadharia hii katika kufasili maana ya maana kwani taswira au picha ya akilini si kigezo toshelevu cha uchanganuzi na ufasiri wa maana. Hii ni kwa sababu kila mzawa wa lugha huwa na picha tofauti kuhusu maneno, vitu, dhana au hali mbalimbali.

Pia, nadharia hii haiwezi kuelezea maana ya sentensi au nahau, kwa kuwa maana ya kinyambo haipatikana katika leksimu tu na wala si utungo mrefu kama vile nahau na sentensi. Nahau ifuatayo inaweza kutumika kama mfano kuntu wa hoja hii. “amekula chumvi nyingi” katika hali ya kawaida ni vigumu mtu kujenga maana ya dhana hiyo kama hana uelewa wa wazo. Kwa maana hiyo dhana atakayoijenga itahusiana na chumvi moja kwa moja, wakati maana ya nahau hii ni kuishi miaka mingi.

Nadhria ya kichocheo-mwitikio iliasisiwa na wanasaikolojia Skinner na Watson, wao wanadai kuwa maana ya neno au dhana husika hufafanuliwa katika hatua tatu ambazo ni kichocheo, tamko na mwitiko (Holm na Karlgren, 1995:4). Hivyo nadharia hii inaeleza kuwa maana ya umbo la kiisimu linalotamkwa na msemaji hutokana na mwitiko wa msikilizaji. Kwa hiyo nadharia hii huchukulia kuwa maana ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Pia maana ya tamko huwa katika muundo wa kitendo –uneni kama inavyooneshwa hapa chini.
Kichocheo …→ (mwitiko…kichocheo) …→ mwitiko

Tamko     ……………… Jibu la msikilizaji.

Kwa mfano; Musa ameamua kuvuta sigara chumbani, kuna harufu nzito inayotokana na moshi wa sigara. Hali hii inamlazimu Juma kutoa tamko; fungua madirisha yote. John na Kulwa wakaitikia kwa kufungua madirisha na yule mvuta sigara akazima sigara yake. Hivyo basi katika hali hii kichocheo cha tamko la Juma ni harufu ya moshi wa sigara, kiitikio ni John na Kulwa kufungua madirisha na mvuta sigara kuzima sigara. Kwa hiyo maana ya usemi inabainishwa na mwitiko wa John, Kulwa na mvuta sigara.

Udhaifu wa nadharia hii ya kichocheo-mwitiko ni kwamba, kichocheo kimoja kinaweza kusababisha utokeaji wa viitikio viwili au zaidi. Kwa mfano mvua imeanza kunyesha, mama anawaamrisha watoto waingie ndani. Watoto wanaitikia kwa kukimbia kwenda ndani ya nyumba.
           Kichocheo……………………mvua
           Tamko………………….ingia ndani
           Kiitikio ……………….watoto kuingia ndani ya nyumba upesi.
Katika mfano wetu huu viitikio vinaweza kuwa; watoto kuchukua ndoo na sufuria na kuanza kuteka maji, kuingia ndani na kuchukua miavuli, kuingia ndani na kukoka moto (Matinde, 2012:259).

Maneno mengi katika lugha hayataji vitu vinavyoonekana, kwa hiyo basi maneno hayo hayawezi kusababisha mwitikio wa msikilizaji. Mfano wa maneno hayo ni kama vile njaa, busara, upendo, uchoyo na huruma (Alston, 1967). Hii ni kwa sababu maneno dhahania hayawezi kuelezwa kwa kutumia nadharia hii.

Pia wakati mwingine wanalugha hawaitiki maneno kwa vitu vinavyowakilisha maneno hayo (Holm na Karlgren, 1995:4). Hii ina maana kuwa kujenga maana ya kinyambo kwa kutumia nadharia ya kichocheo mwitiko inalazimisha upekee wa vinyambo au maneno husika. Ukweli ni kwamba wanajamii huitikia vitu vinavyowakilisha maneno hayo.

Aidha semi nyingi sana katika lugha hazidhibitiwi na kichocheo katika muktadha peke yake. Kwa mantiki hii nadharia ya kichocheo mwitiko inakosa mashiko kwani wakati mwingine mtu anaweza kuulizwa swali na asijibu au akajibu kinyume kabisa na swali. Kwa mfano ni kawaida kwa Mtanzania kusema nakuja wakati anaonekana anakwenda.

Nadharia ya masharti – ukweli husisitiza dhana ya ukweli katika ujasiri wa maana, hivi kwamba maana sharti iwe ya kweli na ukweli huo ubainishwe bayana. Nadharia hii iliasisiwa na wanamantiki na wanafalsafa, kisha ikafafanuliwa na wanaisimu.
Mfano (a) Ukweli wa kihistria
i/ Muungano wa Tanzania na Zanzibar 1964
           ii/ Rais wa kwanza wa Tanzania ni J. K.Nyerere
          (b) Ukweli wa maarifa ya kiulimwengu
Ukweli huu hutokana na uhalisia wa kiulimwengu ambao kila mwanajamii anakuwa nao. Mfano shairi huundwa na beti, mistari, vina na mizani au mwanamke hujifungua.
       
(a)ukweli wa kiisimu
Ukweli huu hubainishwa kupitia mfuatano wa maneno katika sentensi na usahihi wa mfuatano huo.
      i ) Hadija aliolewa na Kanyansa (sahihi)
      ii) Kanyansa aliolewa na Hadija ( si sahihi)

Nadharia hii hushughulikia sentensi arifu tu, kwa kuwa ndizo hutoa kauli ambazo zinaweza kuwa kweli au si kweli. Hivyo ni vigumu kubashiri maana ya sentensi swalifu na amrishi kwa maswali na amri haviwezi kubainisha ukweli au si kweli. Vilevile ni vigumu nadharia hii kutumiwa kubainisha ukweli au wigo wa sentensi tendezi, kwani sentensi tendezi hazielezi matukio. Kwa mfano; Ninakubali kuwa yeye si jambazi. Katika sentensi hiyo ni vigumu kuamini au kutoamini ukweli wa kauli hiyo. Sentensi moja au zaidi huweza kuibua seti nyingi za masharti ukweli hali ambayo huifanya nadharia hii kuwa na mzunguko usiokikomo katika ufasiri na ufafanuzi wa maana.

Nadharia hii hutegemea zaidi maarifa ya kiulimwengu imani, mielekeo na tajiriba pana kuhusu kila tungo. Sentensi inayodokeza maarifa ya kiulimwengu ni ya kijumla kuhusu taaluma mbalimbali kama vile; maji hayana rangi- itakuwa kweli endapo tu maji hayatakuwa na rangi. Hivyo basi ukweli huu ni wa kiulimwengu kwa sababu kila mwanajamii anakuwa nao.

Nadharia ya masharti-ukweli hujikita zaidi katika maswala ya taaluma ya mantiki na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana. Hii ni kwa sababu tu nadharia hii inajikita zaidi katika kujua maana ya neno. Kwa mfano nini maana ya kifo na ukweli ni nini. Hivyo basi kutokana na mifano hiyo hapo juu nadharia hii huenda mbele zaidi na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana.

Nadharia ya utendaji au matumizi ilianzishwa ili kutatua upungufu uliojitokeza katika nadharia zilizotangulia. Nadharia hii inasema kwamba si sahihi kuangalia maana ya neno au kisemo kuwa si kitu ambacho kinajitosheleza. Msisitizo upo wa maana ya neno hupatikana katika utumizi uliotumika, kwani neno halina maana moja. Mwasisi wa nadharia hii ni Ludwing Wittgenstein, yeye aliona nadharia hii itatoa upungufu ulijitokeza katika nadharia zilizopita (Matinde, 2012:260). Katika kitabu cha Philosophical Investigation (1963) anasema ni kosa kubwa kuangalia kama kitu au kiumbile kamili. Hivyo alipendekeza kuwa maana ya neno iangaliwe kwa kuzingatia muktadha wa neno au kisemo jinsi kilivyotumika. Kwa maana hiyo maana au kisemo ni matokeo au athari inayopatikana.

Neno moja huweza kuwa na maana nyingi kutokana na muktadha au kutokana na matumizi yake. Kwa kuangalia muktadha wa jamii kuna baadhi ya maneno ambayo huwa na maana katika jamii fulani. Kwa mfano matumizi ya tumsifu Yesu kristo huendana na muktadha wa ibada au waumini wawili hasa wa kikatoriki. Usemi huu utakapotumiwa msikitini utazua utata wa imani za kidini.

Pamoja na  ugumu uliopo katika kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali zilizojadiliwa na wataalamu wengi, kila nadharia ina ubora na mapungufu yake katika kufasili maana ya maana katika kiwango cha neno na sentensi. Kwa hiyo maaana ya maana inabaki kuwa dhana telezi kutokana na utata wa kufasili dhana hii. Ni vema tafiti mbalimbali ziendelee kufanyika ili kuziba pengo la  ugumu wa kufasili maana ya maana.

                                                   MAREJEO
Alston, W. P. (1967) Meaning The Encyclopedia of philosophy, vol 5 Macmillan  and  Free press,
                                PaulEdwards, Editor in Chief, (pp.233-241), imesomwa tarehe 11/04/2014 saa 22:00
                                kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Baron, J. (1972) Semantic Components and Conceptual development, Elsevier imesomwa tarehe 11/04/2014
                                saa 22:15 kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Bloomfield, W. L. P. (1983) Language, LondonNew york.

Filp, H (2008) What is Semantics, What is Meaning, imesomwa tarehe 11/04/2014, saa 20:00 kutoka
                                www.sciencedirect.com/science/article.

Habwe, J. na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.

Holm, P. and Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning and Different perspective on information System,
                                Stockholm University, Marburg.

Lyons, J. (1981) Language; Meaning and Context, Fontana Paperbacks.

Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,
                               Serengeti Education publishers (T) LTD, Mwanza.

Mdee, S. J. na wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21: Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne
                               Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi.

Sengo, T. S. Y.M (2009) Fasihi za Kinchi, The Regestered Trustees of Al Amin Education and Research
                               Academy, Dar es Salaam.

Wamitila, K. W, (2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia, Kenya Focus Publications LTD, Nairobi.




Friday, April 18, 2014

TEMA MATE TUMCHAPE

Nani mtani jembe?
Nyumba ya mlevi mmoja nje kuna shimo kubwa la maji bila mfuniko. Siku moja karudi usiku kalewa toooop mambo yakawa hivi:
MUME: fungua mlango!
MKE: leo sifungui! Nimechoshwa na ulevi wako.
MUME: kama hufungui najitupa kwenye shimo nife                kabisa.
MKE. Kufa huna faida yoyote duniani.
MUME: kachukua jiwe kubwa kalitupa kwenye                     shimo dubwi!
MKE kajifunga kanga, kafungua mlango. Ghafla                 mume kaingia ndani na kumfungia mke nje.
MKE: Nifungulie la sivyo nitapiga kelele majirani                waje.
MUME: Piga kelele na wakija uwambie unatoka                       wapi usiku huu na kanga moja.

                  Nani jembe hapo, mume au mke? 
Tuma ujumbe wa kufurahisha  0763891415, ili watu wacheke.

VISIMA VYA SHAABAN ROBERT

VISIMA
VYA
SHAABAN ROBERT

Na nianze kwa salaamu, salamu ni yangu jadi,
Pokea zangu salamu, usitie ukaidi,
Nyote kwangu ni muhimu, hakuna aliyezidi,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Hapa nitapaanzia, pengine kuelekea,
Tega sikio sikia, akilini kuyatia,
Moja mbili naingia, tayari kukuambia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha kwanza kufikirika, kisa mwana mfalume,
Mkuu mwana kataka, si binti bali kidume,
Waganga wakaitika, kwa kasi kama umeme,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Wakatoka wa kusini, magharibi wakafika,
Hata wa kasikazini, kipenga kiliwafika,
Mashariki sikioni, ngoma zilitetemeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Uponyaji kwa kafara, baraza lilitamka,
Ujinga kweli hasara, nchi iliharibika,
Waganga waso busara, miti mifugo kufyeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shujaa Utubusara, akili alitumia,
Kuiondoa hasara, nchi ilokusudia,
Hakuyataka madhara, kama yaliyotokea,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha pili ni cha Adili, mgawo kisa kikuu,
Kisima chao ahali, na mambo yao makuu,
Wema kweli ni asali, twairamba wajukuu,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Dunia kamwe si mbaya, wala haina makucha,
Binadamu tu wabaya, twasemana kutwa kucha,
Wema hushinda ubaya, Adili hakuuacha,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Busara kubwa kichwani, haina katu faida,
Kama hauna moyoni, wema na njema ibada,
Utatoswa baharini, ndugu acha ya husuda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Adili kashinda vita, kwa kutenda yalo mema,
Wema kwako nauleta, uwe baba naye mama,
Tenda pasi na kusita, imara mja simama,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha tatu binti Saadi, wasifu chaelezea,
Hiki kweli ni samadi, kipandwacho kinamea,
Giza linapokuzidi, kuchwa kuna karibia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti aliuza vyungu, mjini akaingia,
Maisha yale machungu, binti alivumilia,
Alitaka cha uvungu, kuimba aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti alikuwa mwema, kwa watu wa rika zote,
Mema aliyoyachuma, yalifika nchi zote,
Siti kaacha alama, hakutenda kwa kitete,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maisha kweli matendo, nini mja umetenda?
Singizi zaole vundo, waloshinda wametenda,
Epuka kuwekwa kando, kapambane tayashinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Rangi haina nafasi, katika kufanikiwa,
Mshipi utie tasi, kijana hujachelewa,
Hakuna jambo jepesi, liwezalo kimbiliwa,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti hakuwa Mtanga, watu wote tambueni,
Siti alitangatanga, mwisho yuko vitabuni,
Siti alitoa mwanga, nyayoze tufuateni,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maji ya kisima hiki, matamu nakuambia,
Utamu haufichiki, Shabani katwandikia,
Jitenge na unafiki, heri itakufikia,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Nne ni maisha yake, humo ninaogelea,
Alitupenda wenzake, tawasifu katwachia,
Tuzifate nyayo zake, wema kuushangilia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kayamimina, Robert kasisitiza,
Alimpenda Amina, hata katika jeneza,
Alipenda wake wana, Shabani hakujikweza,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Alichapa zake kazi, kwa makini na stadi,
Aliheshimu wazazi, hakutenda ukaidi,
Aliwapenda wakazi, alitimiza ahadi,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Penzi bora katangaza, katika yake diwani,
Kisima chatuliwaza, mitungi kutwa vichwani,
Umpendaye  utamwaza, siku zote maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kitu azizi, mja hilo litambue,
Usiitende ajizi, mwenzio mtamkie,
Mambo uyaweke wazi, wabukuzi wabukue,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Kisima kusadikika, njiani alikichimba,
Kwa wema katualika, wema ni la kwetu shamba,
Wavua pweza huvuka, katika wao mwamba,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siku ya watenzi wote, shabani aliandika,
Bara visiwani kote, watenzi walizinduka,
Hawakuzicheza kete, siku wakaiitika,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

K’elelezo cha fasili, ni ubora wa Shabani,
Kimebaini vivuli, kweli ndoa ni kanuni,
Ameiandika kweli, fumbo kuu maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shabani taa angavu, nani asiyeijua,
Shabani mvumilivu, vitabu katwandikia,
Shabani bwana shupavu, popote aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Utubora mkulima, kilimo alihimiza,
Alirudi himahima, mjini alikubeza,
Imara alisimama, uchumi kaukweza,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Shaabani liandika, jitu jinga ni hasara,
Usiweke ushirika, hilo halina busara,
Zinduka dada kaka, badili zako fikra,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Nitatia umakini, visimavye  kuvilinda,
Sintotia ufitini, mbegu bora kuipanda,
Aliimba ufukweni, kiswahili kukilinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

                                                            Kapele harry, simu 0763891415/hkapele@gmail.com

Monday, March 31, 2014

TUNZO YA USHAIRI

Malengo ya shindano hili ni: kumkumbuka mwanzilishi wa Tunzo hii, Marehemu Gerard Belkin,
kuuenzi mchango wa mtunzi na mwalimu mashuhuri wa Tanzania, Professor Ebrahim Hussein, na
kukuza fasihi na lugha ya Kiswahili kwa kuibua na kuendeleza vipaji vya watunzi.
Shindano litafungwa 30 Mei 2014. Washindi watatangazwa mwezi wa Agosti. Mshindi wa
kwanza atapata zawadi ya 2,000,000 /=. Mshindi wa pili atapata 1,300,000 /= na mshindi wa
tatu atapata 700,000 /=.

MASHARTI
1. Hili ni shindano la utunzi wa ushairi katika lugha ya Kiswahilitu.
2. Kwa mwaka huu, tungo zitakazoshindanishwa ni za aina mbili tu:  mashairi na nyimbo.
   Tenzi/Tendi na kazi za kinathari, kama riwaya au tamthilia, hazitahusika.
3. Kila mshiriki awasilishe mswada MMOJA tu wenye tungo TATU tu.
4. Tungo ziwe ni za mtunzi mwenyewe.
5. Tungo ziwe  mpya kabisa. Yaani, zisiwe zimepata kuchapishwa au kutiwa katika CD au
    kanda; kuchezwa jukwaani, redioni au katika televisheni, au kusambazwa kupitia katika
    mitandao.
6. Bahari zitakazoshindanishwa ni: Kundi A: Mashairi(ya Kimapokeo au Huru-masivina); B.
    Nyimbo:Za kimapokeo, k.m. Taarabu, au za Bongo fleva.
7. Kila utungo wa kimapokeo uzingatie kanuni za kijadi za utunzi, na usipungue beti 10 au
    kuzidi beti 15. Utungo wa wimbo, pamoja na kuzingatia kanuni zinazohusika, usipungue
    beti 3 wala kuzidi beti 10.
8. Utungo huru usipungue mishororo (mistari) 3 wala kuzidi mishororo 50.
9. Kila mshiriki awasilishe tungo za bahari au aina moja tu katika makundi A na B.
10. Mtunzi atachagua mwenyewe mada na maudhui ya utungo wake.
11. Tungo ziheshimu miiko ya kijamii na kimaadili.

MAELEKEZO MENGINE
1. Kila mshiriki aambatanishe ukurasa wenye maelezo mafupi yenye kuzingatia yafuatayo:
• Jina lake kamili, wasifu na sifa zake kwa ufupi (umri, jinsi, kazi, utunzi wake)
• Anwani ya posta/makazi, anwani-pepe, na namba ya simu ya mkononi
• Maelezo kuwa mswada ni kwa ajili ya Shindano la Ushairi la Ebrahim Hussein
2. Tungo zichapwe kwa kompyuta, upande mmoja wa karatasi, kwa kutumia herufi za ukubwa
   wa pointi 12, na kuacha nafasi moja na nusu baina ya mistari.
3. Tarehe ya mwisho ya kupokea miswada ni: 30/5/2014, saa 10 alasiri.
4. Miswada inaweza kuwasilishwa kwa mkono, kwa njia ya posta au kwa barua-pepe.
• Miswada itakayoletwa kwa mkono iwasilishwe katika ofisi ya Tuzo iliyoko katika jengo la
   TPH Bookshop, Mtaa wa Samora Na. 24, Dar es Salaam.
• Miswada  itakayowasilishwa  kwa  njia  ya  barua-pepe  itumwe  kwenye  anwani-pepe
   ifuatayo: tunzoushairi@gmail.com
• Miswada itakayoletwa kwa njia ya posta itumwe kwenye anwani ya posta ifuatayo:
  Mratibu, Shindano la Ushairi la Ebrahim Hussein, Mkuki na Nyota Publishers Limited,
  S.L.P. 4246, Dar es Salaam
  Kwa maelezo zaidi tembelea Tovuti yetu: www.ushairi.com au piga simu: 0652 02 82 07

Monday, March 24, 2014

NADHARIA YA TAFSIRI NA UKALIMANI

NADHARIA YA TAFSIRI NA UKALIMANI
                                                                                                                                         Imehaririwa na Kapele. H                               
                                        © 2014
Karibu tena mdau na mpenzi wa lugha ya kiswahili leo ningependa kwapamoja tuogelee katika  bahari ya kiswahili, yenye kina na upana wa kutosha. Katika uwanja huu ni vema tuanze na dhana ya Tafsiri ambapo wataalamu mbalimbali watatuongoza kupata dhana iliyokamulika.

Mshindo (2010:2), anaanza kwa kutoa historia ya dhana kufasiri “kietimolojia dhana kufasiri imetokana na neno la kiatini translatio lenye maana ya kupeleka upande wa pili au kuleta upande wa pili. Mtaalamu huyu anajaribu kufasili dhana hii kuwa kufasiri ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadaye matini nyingine inayowiana nayo, ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe ule ule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine.
Newmark (2003:5), anaeleza kuwa kufasiri ni kuweka maana ya matini moja katika lugha nyengine kwa namna ambayo mwandishi amekusudia matini hiyo iwe.
Catford (1965:20), anafasili tafsiri kuwa ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka lugha nyingine (lugha lengwa).

Mwansoko(1996), tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Mawazo kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yawiane na wala haiwezekani mawazo ya matini hizo mbili kuwa sawa kabisa. Pia tafsiri hii imeelezwa na Mwansoko na wenzake(2013:1), kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.

Brislin (1976), ni dhana inayorejelea uhamishaji wa mawazo na habari kutoka lugha moja (chanzi) hadi lugha nyingine (lengwa); ama lugha hizo zimeandikwa au hazijaandikwa; ama lugha hizo zina othografia zilizosanifiwa au hazina ama lugha mojawapo au zote mbili ni za kiishara.

Pinchuck (1977), anaeleza kuwa tafsiri ni mfanyiko tendani wa kutafuta ulinganifu wa lugha lengwa kwa usemi wa lugha chanzi.

Nida na Taber (1969), wanasema kuwa kutafsiri hujihusisha na kuhamisha ujumbe katika lugha lengwa ambao ni linganifu kutokana na ule wa lugha chanzi kwa kuzingatia maana na mtindo.

LUGHA CHANZI/ MATINI CHANZI
Hii ni lugha/matini ambayo imetumia lugha ya kwanza na ambayo haijatafsriwa. Mfano. Lugha chanzi yaweza kuwa Kiswahili, kiingereza, kijapani n.k, Pia kwa ufupi inaweza kuitwa (LC).

LUGHA/MATINI LENGWA
Hii ni lugha ambayo inapatikana baada ya matini kutafsiriwa. Pia inaweza kuitwa (LL).
Kutokana na fasili hizi za wanazuoni mbalimbali inawezekana kabisa kupata maana ya tafsri kwa kuunganisha ama kusahihisha mapungufu yaliyomo katika fasili hizo. Hebu tazama fasili, tafsiri ni matini inayopatikana kutokana na mchakato wa kuhawilisha mawazo yae yale kutoka lugha chanzi na kupeleka mawazo hay ohayo katika lugha lengwa au ni mchakato wa kuhawilisha mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.

MAMBO MUHIMU YANAYOPASWA KUZINGATIWA KATIKA TAFSIRI
Mawazo yanayoshughulikiwa lazima yawe katika maandishi na si vinginevyo. Mawazo au ujumbe kati ya matini chanzi na matini lengwa sharti yalingane. Katika hili kuna angalizo kubwa kwamba mawazo haya si lazima yawe sawa bali yanatakiwa yalingane.

Hali ya mawazo ya matini chanzi na matini lengwa kutokuwa sawa kwake kunaweza kusababishwa na sababu zifuatazo. Tofauti za kiisimu, Tofauti za kiutamaduni, Tofauti za kihistoria, Tofauti za maendeleo ya sayansi na teknolojia, na Tofauti za kimazingira.Mwansoko ameshatajwa (2013). Newmark anaendelea kueleza juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu tafsiri ni pamoja na dhamiri yake, maana yake, athari yake, mfumo wake, na dhima yake ( dhamiri ya mtunzi wa matini chanzi ni ipi, hivyo ni wazi kuwa kuyatambua mawazo ya mtunzi wa matini chanzi ni vigumu lakini ndio kazi ya tafsiri hiyo, kuhusu maana ya matini ni vema kuisoma matini kasha ukaielewa maana iliyomo ndani yake ndipo ukaanza kazi ya kuitafsiri matini lengwa, pia athari ya matini kwa wasomaji wake athari hiyo yaweza kuwa ya kiutamaduni, kiuchumi, kimazingira, kisiasa n.k,

MAMBO MUHIMU YANAYORAHISISHA KAZI YA TAFSIRI
Muktadha au mazingira asilia, mtafsiri anapaswa kuongozwa na muktadha makhsusi. Katika muktadha sharti utamaduni utangulie ndipo siasa na mamlaka vifuate.
Kanuni za sarufi za lugha husika. Katika kutafsiri kanuni ama kaida sharti zibuniwe, zibadilike, na kufuatwa. Lefevere (1998), kufasiri ni mchezo wa lugha unaojumuisha kaida ambazo zinabuniwa na mchezo wenyewe lakini ambazo zenyewe haziwezi kuwa mchezo wenyewe. Pia kufasiri ni kufuata kaida, kubadilisha kaida, kujenga kaida na kubuni kaida ambazo kwa upande wake zinaongeza uchangamano ndani na nje ya uga wake.
Maandishi ama tahajia ya lugha husika ama lengwa. Maana ya maneno yaliyomo katika matini. Jambo hili limetiliwa mkazo na mwanazuoni Newmark katika fasili yake ya tafsiri kuwa, mtaalamu anapaswa kuzingatia maana ya maneno yaliyomo katika matini, kama ilivyokusudiwa iwe na mwandish chanzi.

Maana ya nahau na misemo. Kuna maana tofautitofauti za misemo kutoka jamii moja na jamii nyingine. Si kila maana ya msemo wa Kiswahili unaweza kupatika katika lugha ya kiingereza. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia maana na misemo kutoka katika lugha lengwa.
Matumizi ya vituo na mikato katika kutenga desmali. Ni muhimu kuzingatia vituo na mikato katika kutenga desmali kwani alama hizi mbili zina matumizi tofauti hasa katika lugha ya kiispania na hile ya kiingereza. Mfano, 1,000.01 kwa kiingereza ni sahihi lakini kiispania sio sahihi kwani wao hutumia alama ya kituo ndipo ikafuata alama ya makato kama inavyoonekana hapa, 1.000,01 hivyo ni muhimu sana kuzingatia haya.

DHIMA YA TAFSIRI
Dhima au kazi ya tafsiri imeweza kuelezwa na wanazuoni mbalimbali ambo kwa hakika hawakucheza mbali na uga huu, wanazuoni hawa waliamua ndelea na kpambana vilivyo katika vita isiyo na usawa bali ulinganifu. Mwansoko na wenzake (2013:1-3), wao wametaja na kueleza dhima kuu nne za tafsiri ambapo wameanza na:
i.              Tafsiri kama njia ya mawasiliano.
ii.            Tafsiri kama nyenzo ya kueneza utamaduni.
iii.           Tafsiri kama mbinu ya kujifunza lugha.
iv.           Tafsiri kama kiliwazo cha nafsi ya mfasiri.
v.            Tafsiri huweza kuziba mapengo ya kimsamiati au kimaana katika lugha.

Pia Mshindo ametajwa (2010:25-28), hatofautiani sana na mwansoko kwani naye pia ametaja na kufafanua dhima za tafsiri kuwa ni:
i.              Tafsiri hutumika kama nyenzo ya mawasiliano.
ii.            Kufasiri ni kuuleza na kuueneza utamaduni wa jamii.
iii.           Kufasiri ni nyenzo kuu ya kufundishia lugha.
iv.           Kufasiri ni kushajiisha tabia ya kusoma na kutafiti.
v.            Kufasiri huziba mapengo ya kimsamiati au kimaana baina ya lugha.
vi.           Kufasiri huwa kiliwazo

Wataalamu hawatofautiani sana katika ufafanuzi wa dhima za tafsiri katika maisha ya kila siku, japo tofauti zipo lakini si kubwa sana. Kuhusu suala la tafsiri kama njia ya mawasiliano, waandishi hawa wanaeleza kuwa katika kufasiri kuna mawasiliano changamano sana baina ya tamaduni. Katika maisha ya kila siku watu huwasiliana kwa kutumia ujumbe uliofasiriwa kwa kufuata misingi ya kiutamaduni. Katika kufanikisha mawasiliano baina ya jamii mbili tofauti ujumbe wa matini chanzi hufasiriwa na kuwekwa katika matini lengwa. Hivyo mawazo ya matini chanzi hutumika na watu wenye uwezo wa kutumia lugha ya matini lengwa. Utofauti wa kutumia lugha tofauti duniani umesababisha tukio la kutafsiri. Mwansoko na wenzake ameshatajwa (2013:2), wanaeleza kuwa kama njia ya mawasiliano miongoni mwa mataifa mbalimbali, tafsiri inatumika kutolea maelezo ya biashara.

Tafsiri kama nyenzo ya kunezea utamaduni, mwingiliano wa tamaduni za mataifa mbalimbali zinaenezwa kwa kutumia tafsiri za matini. Nchi nyingi zinaeneza utamaduni wake kupitia matini mbalimbali. Yapo matini yalitafsiriwa kutoka lugha chanzi ya kiingereza na kuweka katika lugha lengwa yaani Kiswahili. Hivyo basi kutokana na matini ya kingereza kufasiriwa na kutumika katika jamii ya waswahili, kupo kuenea kwa utamaduni wa mwingereza katika jamii ya waswahili. Mfano mzuri ni kitabu cha Mashimo ya Mfalme Sulemani, kilichofasiriwa na F. Johnson. Kinaonesha wazi ni jinsi gani utamaduni wa mzungu ulivyoenezwa katika jamii ya waafrika.

Tafsiri kama nyenzo ya kufundishia lugha, ili kuweza kupata mawazo au kuvijua vipengee vya lugha nyingine huna budi kutumia taaluma ya tafsiri ili uweze kuyatambua mawazo yaliyomo katika lugha chanzi na kuipeleka katika lugha lengwa. Mfano Mshindo, (2010:26), anaeleza kuwa katika miaka ya hamsini(50) na sitini (60), Kiswahili kilitumika kufundishia lugha ya kiingereza katika skuli za sekondari za Zanzibar. Mbinu iliyotumika ni wanafunzi kupewa miundo ya Kiswahili na kuifasiri kwa kiingereza au kupewa miundo ya kiingereza aifasiri kwa Kiswahili. kutokana na dhima hii ni muhimu sana kwa mfasiri kujifunza miundo ya lugha zote mbili.

Kufasiri ni kushaajiisha tabia ya kusoma na utafiti. katika kazi hii ya kufasiri, mfasiri analazimika kukusanya kwa  kusoma visawe vingi na miundo mingi ya lugha zitakazo msaidia katika kazi yake ya kufasiri. Kusoma kunamsukuma mfasiri kufanya utafikti wa kina juu ya visawe, utamaduni wa lugha lengwa na chanzi, kukusanya misamiati. Kwa kufanya hivo mfasiri anakuwa na uwanja mpana wa kuimudu kazi yake. Ikumbukwe tu kuwa hakuna hukumu ya kazi bila ya kuwa na data sahihi, hivyo ili hukumu iweze kuwa sahihi mfasiri analazimika kufuata kanuni za utafiti ili aweze kuwa na uhakika wa kazi yake.Mshindo ameshatajwa uk. 27, anafafanua kwamba ukweli ni kwamba hakuna mfasiri ambaye hafanyi utafiti, japo mdogo, katika shughuli ya kufasiri. Hulazimika kupekua katika nyaraka mbalimbali ili kujua maana ya maneno, usuliwa mambo, na historia ya matukio.

Kufasiri huziba mapengo ya ya kimsamiati au kimaana baina ya lugha, maneno mengi hukumbwa na atahari za kiutamaduni, kiisimu, na kihali. Kutokana na athari hizi mfasiri hulazimika kutafuta maana ya maneno yatakayoeleweka vizuri kwa watumiaji wa lugha lengwa. Hii hutokana na utofauti wa matumizi katika baadhi ya maneno ambayo ambayo katika jamii nyingine yana maana tofauti na ile ya lugha chanzi. Mfano: Mshindo ameshatajwa anasema, katika mazingira ya rushwa neno mchicha, ambalo maana iliyozoeleka ni aina ya mboga ya majani, haliwezi kukidhi haja kwa maana hiyo iwapo mfasiri hakulifafanua katika tafsiri yake na kumwezesha msomaji wake kuelewa kwamba katika muktadha huo lina maana ya rushwa. Pia katika mazingira mengine neno wimbo husimama badala ya rushwa kwani kuna baadhi ya watuhumiwa huambiwa kuwa ili uweze kuishinda kesi hii huna budi kuimba wimbo wako.

Kufasiri kama kiliwazo, katika kazi ya kufasiri wapo baadhi ya wafasiri ambao huifanya kazi kama kiliwazo cha nafsi zao. Katika dhima hii kazi zinazoshughulikiwa ni kazi za kishairi. Kufasiri huku si kwa lengo jingine lolote lile. Kwani kazi hizi huwa kiliwazo cha mfasiri kwa sababu tu mfasiri huwa na amani hasa pale anapofanikiwa kuifaisiri kazi ambayo ililikuwa inampa shida kubwa akili mwake. Mara tu baada ya kukamilisha shughuli nzito hiyo mfasiri huifurahisha akilini yake kwa kukubali kazi yake. Mwansoko na wenzake wametajwa, uk:3 wanaeleza wazi kuwa tafsiri humfanya mfasiri aburudike na kuridhisha nafsi yake kadiri anavyotatua matatizo yake ya kufasiri. Utafutaji wa visawe mwafaka katika lugha lengwa kwa kawaida ni kazi ngumu, inayochosha na kuchusha. Hizi ni baadhi tu ya dhima pia zinaweza kuongezeka zaidi ya hizi hii ni kutegemea na chanzo cha maandiko na utafutaji wa msomaji hivy unaalikwa kutembelea uwanja wa fasiri ili uweze kutoa mawazo yako.

HISTORIA FUPI YA TAFSIRI

Misri ni nchi inayopatika katika bara la Afrika, nchi hii kihistoria ndio nchi mama ya maendeleo yanayoonekana leo hii. Maendeleo haya hasa ni yale ya kiuchumi, kijami ina kisayansi. Ugunduzi wa mambo mengi yalitokea katika nchi hii ya Misri yalizifikia nchi nyingine kwa njia za tafsiri. Miaka 3,000 na zaidi kabla ya kuzaliwa kristo, ulitokea uvumbuzi wa mambo mengi. ugunduzi wa taaluma mbalimbali uliwasukuma wasomo wa Kiyunani kufika katika nchi ya Misri kwa lengo la kujifunza taaluma. Mnamo karne ya kumi na tisa (19), ili kuweza kuyapata maarifa Wayunani walilazimika kuijua kwanza lugha ya Wamisri, pia walitumia miaka mingi y asana kuishi Misri wakiisaka elimu. Kazi ya kuisaka elimu haikufanywa na kila Myunani bali wasomi wengi na maarufu waliamua kufanya hivyo. Mambo waliyojifunza huko waliyatafsri kwa lugha yao yaani Kiyunani, hivyo lugha ya Misri ilikuwa lugha chanzi na lugha ya Wayunani ilikuwa lugha lengwa.

Mwansoko na wenzake (2013:4), wasema, wakati wa himaya ya Warumi hasa baada ya Ukristo kuenea huko ulaya nzima, elimu hiyo ya zamani ilianza kupigwa vita kwa kudaiwa kuwa ilikuwa ya “kipagani”, kipindi hiki kilipelekea zama za giza. Baada ya kuimarika kwa Uislamu Mashariki ya Kati, Afrika ya Kaskazini na Hispania, wataalamu na wasomi wa Kiislamu walisoma elimu ya Wayunani hasa ile ya kale. Walifanya kazi kubwa ya kufasiri maandiko yale, lugha chanzi ikiwa ni Kiyunani na lugha lengwa ni Kiarabu. Mara tu baada ya kazi kubwa ya kufasiri iliyofanywa na wafasiri matokeo makubwa yalitokea na utamaduni mpya ulienea. Kutokea huku kwa maendeleo makubwa katika nchi za Kiarabu kulisababisha uchumi wan chi za ulaya kuzidi kudidimia. Karne ya kimi na mbili ikumbukwe kuwa ilikuwa na tukio la vita vya msalaba, vita hivi vilihusisha pande mbili yaani Wakristo na Waislamu, wakati wa vita hii wataalamu wengi toka ulaya walishuhudia maendeleo makubwa sana katika nchi za Kiarabu. Wataalamu hao waliamua kuchukus vitabu na kuenda navyo kwa nia ya kufasiri, ili waweze kupata maarifa ya Waarabu na siri kubwa ya maendeleo. Karne ya kumia na tano (15), ulaya ilianza kupata maendeleo makubwa yaliyoifanya ulaya kutoka katika zama za giza zilizosababishwa na imani zao potofu. Kipindi hiki kiliifanya ulaya kuingia katika mfumko wa elimu na maarifa.

Mfano wa vitabu vingi vilivyo fasiriwa vilishika kasi sana ambapo maandishi yaliyosheheni mawazo ya wataalamu mbalimbali. Mawazo haya ya vitabun yalifasiriwa kwa lengo la kuwafikia wasomaji awa nchi za ulimwengu wa tatu.

Karne ya ishirini (20), ni kipindi ambacho kinaonesha kuenea na kukua kwa tafsiri hasa kwa wingi wa maandiko mengi kutafsiriwa. Ni katika kipindi hiki mikataba mingi ya kitaifa kati ya mashirika ya umma nay ale ya binafsi ilifasiriwa na kuleta urahisi mkubwa mawazo kuwafikia watu mbalimbali.

Tafsri nchini Tanzania, ilichelewa kuingia, kwani ni katika karne ya 13, utenzi wa Hamziya uliweza kutafsiriwa kutoka lugha ya Kiarabu (chanzi), na kupelekwa katika Kiswahili (lengwa), katika karne ya (19), vitabu vingi vilifasiriwa na Wamisionari na vingi kati ya hivyo vilikuwa vyenye maudhui ya kidini na hasa dini ya Kikristo (Biblia), vitabu vya fasihi vilivyofasiriwa ni pamoja na Safari ya Gulliver, Hadithi za Allen Quartermain, Robinson Kruso na Kisiwa ckake.
Baada ya uhuru vitabu kama vile Julius Kaizali, Mabepari wa Venasi vilifasiriwa na kwa lengo la kufikisha mawazo kwa waswahili wengine. Mfasiri akiwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Matokeo ya fasiri hizi yanaifanya Tanzania kuwa na hazina kubwa ya mawazo mbalimbali. Mawazo haya yalipatikana kutoka katika lugha nyingi zikiwemo zile za Kiarabu, Kifaransa, Kifini, Kijerumani, Kikorea na Kiingereza.

Pia yapo mashirika yanayofanya kazi ya kufasiri hususani shirika la uchapishaji wa lugha za kigeni, shirika la uchapishaji wa la maendeleo na mashirika mengine mengi. kasoro katia taaluma ya tafsiri haikwepeki. Kwani sifa ya matini mbili yaani chanzi na lengwa sharti zilingane tu, na wala si kuwa sawa. Hivyo ni wito kwa wazawa kufasiri vitabu vya maarifa ya sayansi kama ilivyo katika kazi fasihi. Shukrani za pekee kwa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam (TUKI), Shirika la Habari la Tanzania. Pia pongezi hizi ziwafikie Chama cha WAFASIRI kilichoanzishwa mwaka 1981, kwa kusimamia haki na maslahi ya Wafasiri.  

 NADHARIA YA TAFSIRI

Nadharia ya tafsiri ni maelekezo kuntu juu ya vipengee anuwai vya kifasiri vinavyopaswa kuzingatiwa na kila mfasiri akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Kila kitu hapa duniani huwa na mwanzo wake hivyo hivyo nadharia ya tafsiri ina mwanzo wake ambao unasheheni sababu nyingi za kuanzishwa kwake. Newmark (1982:4-5), anataja sababu kuu tatu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri, sababu hizo zinafafanuliwa kama ifuatavyo:

Mosi, ni kuwepo kwa makosa mengi, hasa yale ya kimuundo, kimaumbo na kimsamiati. Katika taaluma hii ya tafsiri ni vigumu sana kuipata kazi iliyotafsiriwa isiyokuwa na makosa. Kwa hali yoyote hile mfasiri huogelea katika makosa, ingawa anaweza kufanya jitihada za kupunguza baadhi ya makosa.

Pili, idadi kubwa na inayozidi kuongezeka kwa asasi zinazojishughulisha na kazi ya tafsiri. Hapa nchini Tanzania asasi kama vile Baraza la Kiswahilila Taifa, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Shirika la Habari La Tanzania na mashirika ya watu binafsi, kama vile KIU na ILOS, na vyombo vyote vya habari.

Tatu, ni mfumko wa istilahi katika taaluma mbalimbali, hasa sayansi na teknolojia, haja ya kuzisanifisha ili kuwezesha tafsiri baina ya lugha moja na nyingine kufanyika kwa ufanisi zaidi. Yapo baadhi ya masomo ambayo kila siku misamiati mipya inaundwa hivyo basi kutokana uibuzi huu wa misamiati mipya huifanya kazi ya tafsiri kuwa na mapungufu mengi.

Kama ilivyo katika mimea na wanyama kutegemea katika kulisha jambo ambalo wanasayansi wanaliita mlishano yaani simba hutegemea nyama kutoka kwa wanyama wengine, ambao wanategemea kupata chakula kutokana na nyasi na nyasi hutegemea mbolea kutoka kwa wanyama, basi hata nadharia ya tafsiri hutegemeana kama si kuhusiana kwa ukaribu na taaluma nyingine kama vile: Mwansoko na wenzake (2013), wanaanza kwa kusema kuwa tafsiri ni sehemu ya taaluma ya lugha ijulikanayo kama isimu tumizi. Kwa upande mwingine, ni sehemu ya isimu linganishi na katika ismu huchuliwa kama sehemu ya semantiki, yaani elimumaana.

Nadharia ya tafsiri inahusiana kwa karibu sana na isimu linganishi, imbayo kwa kiasi kikubwa hujishughulisha na kulinganisha vipengele vya kiisimu vya lugha mbili au zaidi pamoja na kuchunguza mbinu za uzalishaji. Katika kipengele hiki mfasiri hupata faida ya kuelewa mifumo ya lugha nyingi na namna lugha hizo zinavyotumia zana za kiisimu katika kuwasilisha taarifa anuwai.

Pia nadharia ya tafsiri inahusiana na isimu jamii, taaluma hii huchunguza hasa mahusiano ya lugha na jamii anuwai inayotumia lugha husika. Katika kuchunguza mahusihano taaluma hii uchunguza rejesta za kijamii za lugha na matokeo hasi na chanya ya mwingiliano uliopo baina ya lugha mbili zinazotofautiana kiutamaduni. Hivyo ni wajibu na jukumu la mfasiri kujua tofauti hizi za kiutamaduni na kuzizingatia katika kazi ya kufasiri.

Vilevile nadharia ya tafsiri inahusiana na semantiki ambayo ni elimumaana, kwa kawaida kinachofasiriwa ni mawazo ua maana ya matini na wala sio maneno pwekepweke. Kutokana na taaluma hii kuchunguza maana ni muhimu kwa mfasiri kuijua vizuri taaluma hii ili iwe msingi kwake wa kufasiri matini mbalimbali. Fasiri huendana na kujua maana za maneno, hali ambayo humfanya mfasiri awe na kamusi mbalimbali ili aweze kubaini maana mbalimbali za maneno. Taaluma hii pia humsaidi mfasiri kugundua kuwa maana hazitokani na maneno pwekepweke, ili awezekuchagua maneno kuendana na muktadha.

Elimumtindo ni taaluma nyingine inayohusiana kwa karibu kabisa na nadharia ya tafsiri, kwani taaluma hii hushughulikia uainishaji wa mitindo ya lugha na mikitadha ya matumizi yake. Elimu hii hufanya mfasiri abaini mitindo mbalimbali ya matini chanzi, mtindo huo wa matini chanzi hupelekwa kwa tafsiri katika matini lengwa. Ingawa taaluma hii inahusiana na taaluma hizi pia upo uhusiano wa nadharia hii ya tafsiri na:

Uhakiki matini, katika uhakiki wa matini mfasiri hufanya tathimini ya kina juu ya matini husika kabla ya kutoa hukumu ya ubora wa matini chanzi kabla ya kuitafakari na hatimaye kuifasiri. Mfasiri huakiki vipengele mbalimbali kama vile kipengele cha utamaduni, mazingira n.k


Mantiki, mfasiri husafiri katika uga wa mawazo ya kina ambayo humfanya atambue ukweli na usahihi wa kauli zilizomo kwenye matini chanzi. Taaluma hii humfanya mfasiri kuchambu kauli zenye uvulivuli na kuzirekebisha kabla ya kazi ya kufasiri.

Mwisho nadharia ya tafsiri inahusiana na taaluma ya falsafa inayosisitiza zaidi katika kutafuta maana za maneno kutokana na matumizi yake halisi katika matini inayohusika. TUKI, (2012) wanaeleza falsafa kuwa ni elimu ya asili, maana na sababu za mambo au vitu.


  

                                                     Marejeo
Mshindo,H.B (2010), Kufasiri na Tafsiri,Chuo kikuu cha Chukwani, Zanzibar.
Mwansoko H.J.M, na wenzake (2013), Kitangulizi cha Tafsiri Nadharia na Mbinu, TUKI, Dar es Salaam.

Taasisi ya taaluma za lugha za Kiswahili (2011), Kioo cha Lugha, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.