Saturday, June 22, 2013

THAMANI YA KISWAHILI

              THAMANI YA KISWAHILI

1.  Kinywa ninakifungua, Kiswahili kukisifu,
     Kama walotangulia, wengi nao walisifu,
     Wasomi wanofwatia, idadi yao rufufu,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

2.  Lugha ina zake sifa, kuzaliwa na kukua,
     Lugha inaweza kufa, duniani kupotea,
     Yaweza pata kifafa, popote kuangukia,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

3.  Kiswahili kimekua, ulayani kimefika,
     China wanakitumia, redioni chasikika,
     Vitabuni chavutia, chaitangaza Afrika,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

4.  Kiswahili ni adhimu, kwa wazawa Tanzania,
     Kiswahili ni muhimu, kwa taifa tunajua,
     Nguvu yake ya kudumu, wasojua zingatia,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

5.  Wasomi wanabukua, vyuoni kwa ushindani,
     Thamani wanaijua, kutunza utamaduni,
     Namba yao yazidia, Kiswahili ki’ damuni,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

6.  Kiswahili chapotea, shuleni hata nyumbani,
     Wazawa twapuuzia, twachukulia utani,
     Uchafu tunakitia, Kiswahili ki’ jaani,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

7.  Kapteni kuwa chanzo, lugha kuizalilisha,
     Kuyapuzia mafunzo, ni umma kuupotosha,
     Kiswahili kiwe mwanzo, mbali kitatufikisha,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

8.  Taifa twanyea kambi, Kiswahili kukibeza,
     Tena twaifanya dhambi, utamaduni kupoteza,
     Lugha twaivisha kumbi, ndani lugha imeoza,
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

9.  Tumekuwa kumbakumba, kila lugha twakwapua,
     Tuuacheni ushamba, Kiswahili chatufaa,
     Za kigeni funga kamba, Kiswahili kitang’aa
     Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

10. Kiswahili rangi mbili, nyeupe nayo nyeusi,
      Si hakika bali real, si nafasi ni space,
      Lugha imefika mbali, kwa wazawa ukakasi,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

11. Kiswahili kinalia, mipaka kimewekewa,                      
      Nguvu yake yapungua, za kigeni kutumiwa,
      Msamiati wapotea, lugha kudharauliwa,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

12. Naja na kwao wachache, wavivu wa kufikiri,
      Wanenayo wayaache, mawazo yao sifuri,
      Kiswahili kama mche, kwa ajira ni tajiri,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

13. Tazameni kwa wachina, kichina hakijachina,
      Ng’huung’haa ya wachina, kwenye tenda twawaona,
      Iweje sisi kuchina, kipi kinachotubana?
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

14. Lugha yetu tuienzi, bila shaka tutatoka,
      Kiswahili ni kurunzi, mbele yetu chamulika,
      Tuitumie wajenzi, taifa kulisimika,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

15. Kusahau ni vizuri, lakini si kwa kupanga,
      Harufu zote ni nzuri, na nzi ananiunga,
      Zawadi huwa na siri, ufanano kuujenga,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

16. Waja ninatia nanga, mengine kuyasikia,
      Kutoka kwao malenga, lugha hii waijua,
      Tamashani nilopanga, hapa natamatishia,
      Wavuvi wote wa pweza, mwambani hukutanika.

                                                                        KAPELE HARRY-0763891415
                                                                        kapeleh@yahoo.com

No comments: