Sunday, August 18, 2013

WANAKUSUBIRI

                                           

WANAKUSUBIRI

Pumzi kali watoa, ishara ya kumaliza,
Nguvu zinakuishia, miguu  unaburuza,
Mengi unajiwazia, kufika utaweza?
Wanakusubiri!

Wanakusubiri wote, wazee pia vijana,
Wanakumezea mate, kwa uchu wanaonana,
Wanasubiri upite, wabaki kuulizana,
Wanakusubiri!
WANAKUSUBIRI

Jirani akusubiri, kushindwa akuwazia,
Mawazoye ya hatari, mashimo kakuchimbia,
Safari yako si shwari, miba kakutegea,
Wanakusubiri!

Kizee chenye tunguli, kwa hamu kimetulia,
Chajiuliza maswali, vipi kitakuondoa,
Na usiku hakilali, kukuua chawazia,
Wanakusubiri!

Rafikizo hawapendi, kukuona ukishinda,
Wamekiunda kikundi, kwa visu wanakuwinda,
Wameiandaa gundi, wamekupimia sanda,
Wanakusubiri!

Wakuu wanaumia, vyeo utajawapoka,
Kushinda wamepania, upupu watakupaka,
Kwa waganga wakuendea, kwawe wanaangaika,
Wanakusubiri!

Bibi yako kachukia, zawadi kakwandalia,
Taji ataitumia, ukichaa kukutia,
Kikao kakukalia, penye nia pana njia,
Wanakusubiri!

Shangazi naye kafura, mate chini kayatema,
Kaburi amelichora, pembe nne utazama,
Ameibadili sura, kwa bidii ajituma,
Wanakusubiri!

Ni baba na yeye mama, kwa heri wanasubiri,
Mwana wao umesoma, kwa shida nazo hatari,
Matunda watayachuma, mwisho wa yako safari,
Wanakusubiri!  
                                                                                    
                                                                                                             hkapele@gmail.com


No comments: