NADHARIA YA TAFSIRI NA
UKALIMANI
Imehaririwa na
Kapele. H
©
2014
Karibu tena mdau na mpenzi
wa lugha ya kiswahili leo ningependa kwapamoja tuogelee katika bahari ya kiswahili, yenye kina na upana wa
kutosha. Katika uwanja huu ni vema tuanze na dhana ya Tafsiri ambapo wataalamu
mbalimbali watatuongoza kupata dhana iliyokamulika.
Mshindo (2010:2), anaanza kwa kutoa historia ya
dhana kufasiri “kietimolojia dhana kufasiri imetokana na neno la kiatini
translatio lenye maana ya kupeleka upande wa pili au kuleta upande wa pili.
Mtaalamu huyu anajaribu kufasili dhana hii kuwa kufasiri ni kufafanua maana ya
matini moja na kutayarisha baadaye matini nyingine inayowiana nayo, ambayo
huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe ule ule uliomo katika matini ya
awali kwa kutumia lugha nyingine.
Newmark (2003:5), anaeleza kuwa kufasiri ni kuweka
maana ya matini moja katika lugha nyengine kwa namna ambayo mwandishi
amekusudia matini hiyo iwe.
Catford (1965:20), anafasili
tafsiri kuwa ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja
(lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka lugha nyingine
(lugha lengwa).
Mwansoko(1996), tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa
mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Mawazo kati ya lugha
chanzi na lugha lengwa sharti yawiane na wala haiwezekani mawazo ya matini hizo
mbili kuwa sawa kabisa. Pia tafsiri hii imeelezwa na Mwansoko na
wenzake(2013:1), kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi
kutoka lugha moja hadi nyingine.
Brislin (1976), ni dhana inayorejelea uhamishaji wa
mawazo na habari kutoka lugha moja (chanzi) hadi lugha nyingine (lengwa); ama
lugha hizo zimeandikwa au hazijaandikwa; ama lugha hizo zina othografia
zilizosanifiwa au hazina ama lugha mojawapo au zote mbili ni za kiishara.
Pinchuck (1977), anaeleza kuwa tafsiri ni mfanyiko
tendani wa kutafuta ulinganifu wa lugha lengwa kwa usemi wa lugha chanzi.
Nida na Taber (1969), wanasema kuwa kutafsiri hujihusisha na
kuhamisha ujumbe katika lugha lengwa ambao ni linganifu kutokana na ule wa
lugha chanzi kwa kuzingatia maana na mtindo.
LUGHA
CHANZI/ MATINI CHANZI
Hii ni lugha/matini ambayo
imetumia lugha ya kwanza na ambayo haijatafsriwa. Mfano. Lugha chanzi yaweza
kuwa Kiswahili, kiingereza, kijapani n.k, Pia kwa ufupi inaweza kuitwa (LC).
LUGHA/MATINI
LENGWA
Hii ni lugha ambayo
inapatikana baada ya matini kutafsiriwa. Pia inaweza kuitwa (LL).
Kutokana na fasili hizi za
wanazuoni mbalimbali inawezekana kabisa kupata maana ya tafsri kwa kuunganisha
ama kusahihisha mapungufu yaliyomo katika fasili hizo. Hebu tazama fasili,
tafsiri ni matini inayopatikana kutokana na mchakato wa kuhawilisha mawazo yae
yale kutoka lugha chanzi na kupeleka mawazo hay ohayo katika lugha lengwa au ni
mchakato wa kuhawilisha mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
MAMBO
MUHIMU YANAYOPASWA KUZINGATIWA KATIKA TAFSIRI
Mawazo yanayoshughulikiwa lazima
yawe katika maandishi na si vinginevyo. Mawazo au ujumbe kati ya matini chanzi
na matini lengwa sharti yalingane. Katika hili kuna angalizo kubwa kwamba
mawazo haya si lazima yawe sawa bali yanatakiwa yalingane.
Hali ya mawazo ya matini
chanzi na matini lengwa kutokuwa sawa kwake kunaweza kusababishwa na sababu
zifuatazo. Tofauti za kiisimu, Tofauti za kiutamaduni, Tofauti za kihistoria, Tofauti
za maendeleo ya sayansi na teknolojia, na Tofauti za kimazingira.Mwansoko
ameshatajwa (2013). Newmark anaendelea kueleza juu ya mambo muhimu ya
kuzingatia kuhusu tafsiri ni pamoja na dhamiri yake, maana yake, athari yake,
mfumo wake, na dhima yake ( dhamiri ya mtunzi wa matini chanzi ni ipi, hivyo ni
wazi kuwa kuyatambua mawazo ya mtunzi wa matini chanzi ni vigumu lakini ndio
kazi ya tafsiri hiyo, kuhusu maana ya matini ni vema kuisoma matini kasha
ukaielewa maana iliyomo ndani yake ndipo ukaanza kazi ya kuitafsiri matini
lengwa, pia athari ya matini kwa wasomaji wake athari hiyo yaweza kuwa ya kiutamaduni,
kiuchumi, kimazingira, kisiasa n.k,
MAMBO
MUHIMU YANAYORAHISISHA KAZI YA TAFSIRI
Muktadha au mazingira
asilia, mtafsiri anapaswa kuongozwa na muktadha makhsusi. Katika muktadha
sharti utamaduni utangulie ndipo siasa na mamlaka vifuate.
Kanuni za sarufi za lugha
husika. Katika kutafsiri kanuni ama kaida sharti zibuniwe, zibadilike, na
kufuatwa. Lefevere
(1998), kufasiri ni mchezo wa lugha unaojumuisha kaida ambazo zinabuniwa na
mchezo wenyewe lakini ambazo zenyewe haziwezi kuwa mchezo wenyewe. Pia kufasiri
ni kufuata kaida, kubadilisha kaida, kujenga kaida na kubuni kaida ambazo kwa
upande wake zinaongeza uchangamano ndani na nje ya uga wake.
Maandishi ama tahajia ya
lugha husika ama lengwa. Maana ya maneno yaliyomo katika matini. Jambo hili
limetiliwa mkazo na mwanazuoni Newmark katika fasili yake ya tafsiri kuwa,
mtaalamu anapaswa kuzingatia maana ya maneno yaliyomo katika matini, kama
ilivyokusudiwa iwe na mwandish chanzi.
Maana ya nahau na misemo.
Kuna maana tofautitofauti za misemo kutoka jamii moja na jamii nyingine. Si
kila maana ya msemo wa Kiswahili unaweza kupatika katika lugha ya kiingereza.
Hivyo ni muhimu sana kuzingatia maana na misemo kutoka katika lugha lengwa.
Matumizi ya vituo na mikato
katika kutenga desmali. Ni muhimu kuzingatia vituo na mikato katika kutenga
desmali kwani alama hizi mbili zina matumizi tofauti hasa katika lugha ya
kiispania na hile ya kiingereza. Mfano, 1,000.01 kwa kiingereza ni sahihi
lakini kiispania sio sahihi kwani wao hutumia alama ya kituo ndipo ikafuata
alama ya makato kama inavyoonekana hapa, 1.000,01 hivyo ni muhimu sana
kuzingatia haya.
DHIMA YA TAFSIRI
Dhima au kazi ya tafsiri
imeweza kuelezwa na wanazuoni mbalimbali ambo kwa hakika hawakucheza mbali na
uga huu, wanazuoni hawa waliamua ndelea na kpambana vilivyo katika vita isiyo
na usawa bali ulinganifu. Mwansoko na wenzake (2013:1-3), wao wametaja na
kueleza dhima kuu nne za tafsiri ambapo wameanza na:
i.
Tafsiri kama njia ya mawasiliano.
ii.
Tafsiri kama nyenzo ya kueneza utamaduni.
iii.
Tafsiri kama mbinu ya kujifunza lugha.
iv.
Tafsiri kama kiliwazo cha nafsi ya mfasiri.
v.
Tafsiri huweza kuziba mapengo ya kimsamiati
au kimaana katika lugha.
Pia Mshindo ametajwa
(2010:25-28), hatofautiani sana na mwansoko kwani naye pia ametaja na kufafanua
dhima za tafsiri kuwa ni:
i.
Tafsiri hutumika kama nyenzo ya mawasiliano.
ii.
Kufasiri ni kuuleza na kuueneza utamaduni wa
jamii.
iii.
Kufasiri ni nyenzo kuu ya kufundishia lugha.
iv.
Kufasiri ni kushajiisha tabia ya kusoma na
kutafiti.
v.
Kufasiri huziba mapengo ya kimsamiati au
kimaana baina ya lugha.
vi.
Kufasiri huwa kiliwazo
Wataalamu
hawatofautiani sana katika ufafanuzi wa dhima za tafsiri katika maisha ya kila
siku, japo tofauti zipo lakini si kubwa sana. Kuhusu suala la tafsiri kama njia
ya mawasiliano, waandishi hawa wanaeleza kuwa katika kufasiri kuna mawasiliano
changamano sana baina ya tamaduni. Katika maisha ya kila siku watu huwasiliana
kwa kutumia ujumbe uliofasiriwa kwa kufuata misingi ya kiutamaduni. Katika
kufanikisha mawasiliano baina ya jamii mbili tofauti ujumbe wa matini chanzi
hufasiriwa na kuwekwa katika matini lengwa. Hivyo mawazo ya matini chanzi
hutumika na watu wenye uwezo wa kutumia lugha ya matini lengwa. Utofauti wa
kutumia lugha tofauti duniani umesababisha tukio la kutafsiri. Mwansoko na
wenzake ameshatajwa (2013:2), wanaeleza kuwa kama njia ya mawasiliano miongoni
mwa mataifa mbalimbali, tafsiri inatumika kutolea maelezo ya biashara.
Tafsiri
kama nyenzo ya kunezea utamaduni, mwingiliano wa tamaduni za mataifa mbalimbali
zinaenezwa kwa kutumia tafsiri za matini. Nchi nyingi zinaeneza utamaduni wake
kupitia matini mbalimbali. Yapo matini yalitafsiriwa kutoka lugha chanzi ya
kiingereza na kuweka katika lugha lengwa yaani Kiswahili. Hivyo basi kutokana
na matini ya kingereza kufasiriwa na kutumika katika jamii ya waswahili, kupo
kuenea kwa utamaduni wa mwingereza katika jamii ya waswahili. Mfano mzuri ni
kitabu cha Mashimo ya Mfalme Sulemani, kilichofasiriwa na F. Johnson.
Kinaonesha wazi ni jinsi gani utamaduni wa mzungu ulivyoenezwa katika jamii ya
waafrika.
Tafsiri
kama nyenzo ya kufundishia lugha, ili kuweza kupata mawazo
au kuvijua vipengee vya lugha nyingine huna budi kutumia taaluma ya tafsiri ili
uweze kuyatambua mawazo yaliyomo katika lugha chanzi na kuipeleka katika lugha
lengwa. Mfano Mshindo, (2010:26), anaeleza kuwa katika miaka ya hamsini(50) na
sitini (60), Kiswahili kilitumika kufundishia lugha ya kiingereza katika skuli
za sekondari za Zanzibar. Mbinu iliyotumika ni wanafunzi kupewa miundo ya
Kiswahili na kuifasiri kwa kiingereza au kupewa miundo ya kiingereza aifasiri
kwa Kiswahili. kutokana na dhima hii ni muhimu sana kwa mfasiri kujifunza
miundo ya lugha zote mbili.
Kufasiri
ni kushaajiisha tabia ya kusoma na utafiti.
katika kazi hii ya kufasiri, mfasiri analazimika kukusanya kwa kusoma visawe vingi na miundo mingi ya lugha
zitakazo msaidia katika kazi yake ya kufasiri. Kusoma kunamsukuma mfasiri
kufanya utafikti wa kina juu ya visawe, utamaduni wa lugha lengwa na chanzi,
kukusanya misamiati. Kwa kufanya hivo mfasiri anakuwa na uwanja mpana wa
kuimudu kazi yake. Ikumbukwe tu kuwa hakuna hukumu ya kazi bila ya kuwa na data
sahihi, hivyo ili hukumu iweze kuwa sahihi mfasiri analazimika kufuata kanuni
za utafiti ili aweze kuwa na uhakika wa kazi yake.Mshindo ameshatajwa uk. 27,
anafafanua kwamba ukweli ni kwamba hakuna mfasiri ambaye hafanyi utafiti, japo
mdogo, katika shughuli ya kufasiri. Hulazimika kupekua katika nyaraka
mbalimbali ili kujua maana ya maneno, usuliwa mambo, na historia ya matukio.
Kufasiri
huziba mapengo ya ya kimsamiati au kimaana baina ya lugha,
maneno mengi hukumbwa na atahari za kiutamaduni, kiisimu, na kihali. Kutokana
na athari hizi mfasiri hulazimika kutafuta maana ya maneno yatakayoeleweka
vizuri kwa watumiaji wa lugha lengwa. Hii hutokana na utofauti wa matumizi
katika baadhi ya maneno ambayo ambayo katika jamii nyingine yana maana tofauti
na ile ya lugha chanzi. Mfano: Mshindo ameshatajwa anasema, katika mazingira ya
rushwa neno mchicha, ambalo maana iliyozoeleka ni aina ya mboga ya majani,
haliwezi kukidhi haja kwa maana hiyo iwapo mfasiri hakulifafanua katika tafsiri
yake na kumwezesha msomaji wake kuelewa kwamba katika muktadha huo lina maana
ya rushwa. Pia katika mazingira mengine neno wimbo husimama badala ya rushwa kwani
kuna baadhi ya watuhumiwa huambiwa kuwa ili uweze kuishinda kesi hii huna budi
kuimba wimbo wako.
Kufasiri kama kiliwazo,
katika kazi ya kufasiri wapo baadhi ya wafasiri ambao huifanya kazi kama
kiliwazo cha nafsi zao. Katika dhima hii kazi zinazoshughulikiwa ni kazi za
kishairi. Kufasiri huku si kwa lengo jingine lolote lile. Kwani kazi hizi huwa
kiliwazo cha mfasiri kwa sababu tu mfasiri huwa na amani hasa pale
anapofanikiwa kuifaisiri kazi ambayo ililikuwa inampa shida kubwa akili mwake.
Mara tu baada ya kukamilisha shughuli nzito hiyo mfasiri huifurahisha akilini
yake kwa kukubali kazi yake. Mwansoko na wenzake wametajwa, uk:3 wanaeleza wazi
kuwa tafsiri humfanya mfasiri aburudike na kuridhisha nafsi yake kadiri anavyotatua
matatizo yake ya kufasiri. Utafutaji wa visawe mwafaka katika lugha lengwa kwa
kawaida ni kazi ngumu, inayochosha na kuchusha. Hizi ni baadhi tu ya dhima pia
zinaweza kuongezeka zaidi ya hizi hii ni kutegemea na chanzo cha maandiko na
utafutaji wa msomaji hivy unaalikwa kutembelea uwanja wa fasiri ili uweze kutoa
mawazo yako.
HISTORIA FUPI YA TAFSIRI
Misri ni nchi inayopatika katika bara la Afrika, nchi hii kihistoria ndio nchi mama ya maendeleo yanayoonekana leo hii. Maendeleo haya hasa ni yale ya kiuchumi, kijami ina kisayansi. Ugunduzi wa mambo mengi yalitokea katika nchi hii ya Misri yalizifikia nchi nyingine kwa njia za tafsiri. Miaka 3,000 na zaidi kabla ya kuzaliwa kristo, ulitokea uvumbuzi wa mambo mengi. ugunduzi wa taaluma mbalimbali uliwasukuma wasomo wa Kiyunani kufika katika nchi ya Misri kwa lengo la kujifunza taaluma. Mnamo karne ya kumi na tisa (19), ili kuweza kuyapata maarifa Wayunani walilazimika kuijua kwanza lugha ya Wamisri, pia walitumia miaka mingi y asana kuishi Misri wakiisaka elimu. Kazi ya kuisaka elimu haikufanywa na kila Myunani bali wasomi wengi na maarufu waliamua kufanya hivyo. Mambo waliyojifunza huko waliyatafsri kwa lugha yao yaani Kiyunani, hivyo lugha ya Misri ilikuwa lugha chanzi na lugha ya Wayunani ilikuwa lugha lengwa.
Mwansoko na wenzake
(2013:4), wasema, wakati wa himaya ya Warumi hasa baada ya Ukristo kuenea huko
ulaya nzima, elimu hiyo ya zamani ilianza kupigwa vita kwa kudaiwa kuwa ilikuwa
ya “kipagani”, kipindi hiki kilipelekea zama za giza. Baada ya kuimarika kwa Uislamu
Mashariki ya Kati, Afrika ya Kaskazini na Hispania, wataalamu na wasomi wa
Kiislamu walisoma elimu ya Wayunani hasa ile ya kale. Walifanya kazi kubwa ya
kufasiri maandiko yale, lugha chanzi ikiwa ni Kiyunani na lugha lengwa ni
Kiarabu. Mara tu baada ya kazi kubwa ya kufasiri iliyofanywa na wafasiri
matokeo makubwa yalitokea na utamaduni mpya ulienea. Kutokea huku kwa maendeleo
makubwa katika nchi za Kiarabu kulisababisha uchumi wan chi za ulaya kuzidi
kudidimia. Karne ya kimi na mbili ikumbukwe kuwa ilikuwa na tukio la vita vya
msalaba, vita hivi vilihusisha pande mbili yaani Wakristo na Waislamu, wakati
wa vita hii wataalamu wengi toka ulaya walishuhudia maendeleo makubwa sana
katika nchi za Kiarabu. Wataalamu hao waliamua kuchukus vitabu na kuenda navyo
kwa nia ya kufasiri, ili waweze kupata maarifa ya Waarabu na siri kubwa ya
maendeleo. Karne ya kumia na tano (15), ulaya ilianza kupata maendeleo makubwa
yaliyoifanya ulaya kutoka katika zama za giza zilizosababishwa na imani zao
potofu. Kipindi hiki kiliifanya ulaya kuingia katika mfumko wa elimu na
maarifa.
Mfano wa vitabu vingi
vilivyo fasiriwa vilishika kasi sana ambapo maandishi yaliyosheheni mawazo ya
wataalamu mbalimbali. Mawazo haya ya vitabun yalifasiriwa kwa lengo la
kuwafikia wasomaji awa nchi za ulimwengu wa tatu.
Karne ya ishirini (20), ni
kipindi ambacho kinaonesha kuenea na kukua kwa tafsiri hasa kwa wingi wa
maandiko mengi kutafsiriwa. Ni katika kipindi hiki mikataba mingi ya kitaifa
kati ya mashirika ya umma nay ale ya binafsi ilifasiriwa na kuleta urahisi
mkubwa mawazo kuwafikia watu mbalimbali.
Tafsri nchini Tanzania,
ilichelewa kuingia, kwani ni katika karne ya 13, utenzi wa Hamziya uliweza
kutafsiriwa kutoka lugha ya Kiarabu (chanzi), na kupelekwa katika Kiswahili
(lengwa), katika karne ya (19), vitabu vingi vilifasiriwa na Wamisionari na
vingi kati ya hivyo vilikuwa vyenye maudhui ya kidini na hasa dini ya Kikristo
(Biblia), vitabu vya fasihi vilivyofasiriwa ni pamoja na Safari ya Gulliver,
Hadithi za Allen Quartermain, Robinson Kruso na Kisiwa ckake.
Baada ya uhuru vitabu kama
vile Julius Kaizali, Mabepari wa Venasi vilifasiriwa na kwa lengo la kufikisha
mawazo kwa waswahili wengine. Mfasiri akiwa ni Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere. Matokeo ya fasiri hizi yanaifanya Tanzania kuwa na hazina kubwa ya
mawazo mbalimbali. Mawazo haya yalipatikana kutoka katika lugha nyingi zikiwemo
zile za Kiarabu, Kifaransa, Kifini, Kijerumani, Kikorea na Kiingereza.
Pia yapo mashirika
yanayofanya kazi ya kufasiri hususani shirika la uchapishaji wa lugha za
kigeni, shirika la uchapishaji wa la maendeleo na mashirika mengine mengi.
kasoro katia taaluma ya tafsiri haikwepeki. Kwani sifa ya matini mbili yaani
chanzi na lengwa sharti zilingane tu, na wala si kuwa sawa. Hivyo ni wito kwa
wazawa kufasiri vitabu vya maarifa ya sayansi kama ilivyo katika kazi fasihi.
Shukrani za pekee kwa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam (TUKI), Shirika la Habari la
Tanzania. Pia pongezi hizi ziwafikie Chama cha WAFASIRI kilichoanzishwa mwaka
1981, kwa kusimamia haki na maslahi ya Wafasiri.
NADHARIA
YA TAFSIRI
Nadharia ya tafsiri ni
maelekezo kuntu juu ya vipengee anuwai vya kifasiri vinavyopaswa kuzingatiwa na
kila mfasiri akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Kila kitu hapa duniani huwa na
mwanzo wake hivyo hivyo nadharia ya tafsiri ina mwanzo wake ambao unasheheni sababu
nyingi za kuanzishwa kwake. Newmark (1982:4-5), anataja sababu kuu tatu za
kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri, sababu hizo zinafafanuliwa kama ifuatavyo:
Mosi, ni
kuwepo kwa makosa mengi, hasa yale ya kimuundo, kimaumbo na kimsamiati. Katika
taaluma hii ya tafsiri ni vigumu sana kuipata kazi iliyotafsiriwa isiyokuwa na
makosa. Kwa hali yoyote hile mfasiri huogelea katika makosa, ingawa anaweza
kufanya jitihada za kupunguza baadhi ya makosa.
Pili,
idadi kubwa na inayozidi kuongezeka kwa asasi zinazojishughulisha na kazi ya
tafsiri. Hapa nchini Tanzania asasi kama vile Baraza la Kiswahilila Taifa,
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Shirika la Habari La Tanzania na mashirika
ya watu binafsi, kama vile KIU na ILOS, na vyombo vyote vya habari.
Tatu, ni
mfumko wa istilahi katika taaluma mbalimbali, hasa sayansi na teknolojia, haja
ya kuzisanifisha ili kuwezesha tafsiri baina ya lugha moja na nyingine
kufanyika kwa ufanisi zaidi. Yapo baadhi ya masomo ambayo kila siku misamiati
mipya inaundwa hivyo basi kutokana uibuzi huu wa misamiati mipya huifanya kazi
ya tafsiri kuwa na mapungufu mengi.
Kama ilivyo katika mimea na
wanyama kutegemea katika kulisha jambo ambalo wanasayansi wanaliita mlishano
yaani simba hutegemea nyama kutoka kwa wanyama wengine, ambao wanategemea
kupata chakula kutokana na nyasi na nyasi hutegemea mbolea kutoka kwa wanyama,
basi hata nadharia ya tafsiri hutegemeana kama si kuhusiana kwa ukaribu na
taaluma nyingine kama vile: Mwansoko na wenzake (2013), wanaanza kwa kusema
kuwa tafsiri ni sehemu ya taaluma ya lugha ijulikanayo kama isimu tumizi. Kwa
upande mwingine, ni sehemu ya isimu linganishi na katika ismu huchuliwa kama
sehemu ya semantiki, yaani elimumaana.
Nadharia ya tafsiri
inahusiana kwa karibu sana na isimu linganishi, imbayo kwa kiasi
kikubwa hujishughulisha na kulinganisha vipengele vya kiisimu vya lugha mbili
au zaidi pamoja na kuchunguza mbinu za uzalishaji. Katika kipengele hiki
mfasiri hupata faida ya kuelewa mifumo ya lugha nyingi na namna lugha hizo
zinavyotumia zana za kiisimu katika kuwasilisha taarifa anuwai.
Pia nadharia ya tafsiri
inahusiana na isimu jamii, taaluma hii huchunguza hasa mahusiano ya lugha na
jamii anuwai inayotumia lugha husika. Katika kuchunguza mahusihano taaluma hii
uchunguza rejesta za kijamii za lugha na matokeo hasi na chanya ya mwingiliano
uliopo baina ya lugha mbili zinazotofautiana kiutamaduni. Hivyo ni wajibu na
jukumu la mfasiri kujua tofauti hizi za kiutamaduni na kuzizingatia katika kazi
ya kufasiri.
Vilevile nadharia ya tafsiri
inahusiana na semantiki ambayo ni elimumaana, kwa kawaida kinachofasiriwa ni
mawazo ua maana ya matini na wala sio maneno pwekepweke. Kutokana na taaluma
hii kuchunguza maana ni muhimu kwa mfasiri kuijua vizuri taaluma hii ili iwe
msingi kwake wa kufasiri matini mbalimbali. Fasiri huendana na kujua maana za
maneno, hali ambayo humfanya mfasiri awe na kamusi mbalimbali ili aweze kubaini
maana mbalimbali za maneno. Taaluma hii pia humsaidi mfasiri kugundua kuwa
maana hazitokani na maneno pwekepweke, ili awezekuchagua maneno kuendana na
muktadha.
Elimumtindo ni
taaluma nyingine inayohusiana kwa karibu kabisa na nadharia ya tafsiri, kwani
taaluma hii hushughulikia uainishaji wa mitindo ya lugha na mikitadha ya
matumizi yake. Elimu hii hufanya mfasiri abaini mitindo mbalimbali ya matini
chanzi, mtindo huo wa matini chanzi hupelekwa kwa tafsiri katika matini lengwa.
Ingawa taaluma hii inahusiana na taaluma hizi pia upo uhusiano wa nadharia hii
ya tafsiri na:
Uhakiki matini,
katika uhakiki wa matini mfasiri hufanya tathimini ya kina juu ya matini husika
kabla ya kutoa hukumu ya ubora wa matini chanzi kabla ya kuitafakari na
hatimaye kuifasiri. Mfasiri huakiki vipengele mbalimbali kama vile kipengele
cha utamaduni, mazingira n.k
Mantiki, mfasiri
husafiri katika uga wa mawazo ya kina ambayo humfanya atambue ukweli na usahihi
wa kauli zilizomo kwenye matini chanzi. Taaluma hii humfanya mfasiri kuchambu
kauli zenye uvulivuli na kuzirekebisha kabla ya kazi ya kufasiri.
Mwisho nadharia ya tafsiri
inahusiana na taaluma ya falsafa inayosisitiza zaidi katika
kutafuta maana za maneno kutokana na matumizi yake halisi katika matini
inayohusika. TUKI, (2012) wanaeleza falsafa kuwa ni elimu ya asili, maana na
sababu za mambo au vitu.
Marejeo
Mshindo,H.B (2010), Kufasiri na Tafsiri,Chuo kikuu cha
Chukwani, Zanzibar.
Mwansoko H.J.M, na wenzake
(2013), Kitangulizi cha Tafsiri Nadharia
na Mbinu, TUKI, Dar es Salaam.
Taasisi ya taaluma za lugha
za Kiswahili (2011), Kioo cha Lugha, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dar es
Salaam.
11 comments:
Nice
Safi sana
Somo zuri
Hakika somo hili lafaa kabisa
Hakika somo hili lafaa kabisa
Somo zuri Sana limenifanya nimepata uelewa zaidi kuhusu tafsiri na ukaliman
Nimepata ufahamu mwingi. Shukurani kwa kazi hii nzuri.
Hakika nimejufunza Mambo mengi kupitia nukuu hizi
Well
Somo zuri ila umejikita zaidi katika taaluma ya tafsiri; hivyo ungejaribu kuangalia pia kwenye taaluma ya ukalimani.
Wow. I'm impressed
Post a Comment