Monday, March 24, 2014

NADHARIA YA TAFSIRI NA UKALIMANI

NADHARIA YA TAFSIRI NA UKALIMANI
                                                                                                                                         Imehaririwa na Kapele. H                               
                                        © 2014
Karibu tena mdau na mpenzi wa lugha ya kiswahili leo ningependa kwapamoja tuogelee katika  bahari ya kiswahili, yenye kina na upana wa kutosha. Katika uwanja huu ni vema tuanze na dhana ya Tafsiri ambapo wataalamu mbalimbali watatuongoza kupata dhana iliyokamulika.

Mshindo (2010:2), anaanza kwa kutoa historia ya dhana kufasiri “kietimolojia dhana kufasiri imetokana na neno la kiatini translatio lenye maana ya kupeleka upande wa pili au kuleta upande wa pili. Mtaalamu huyu anajaribu kufasili dhana hii kuwa kufasiri ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadaye matini nyingine inayowiana nayo, ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe ule ule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine.
Newmark (2003:5), anaeleza kuwa kufasiri ni kuweka maana ya matini moja katika lugha nyengine kwa namna ambayo mwandishi amekusudia matini hiyo iwe.
Catford (1965:20), anafasili tafsiri kuwa ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka lugha nyingine (lugha lengwa).

Mwansoko(1996), tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Mawazo kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yawiane na wala haiwezekani mawazo ya matini hizo mbili kuwa sawa kabisa. Pia tafsiri hii imeelezwa na Mwansoko na wenzake(2013:1), kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.

Brislin (1976), ni dhana inayorejelea uhamishaji wa mawazo na habari kutoka lugha moja (chanzi) hadi lugha nyingine (lengwa); ama lugha hizo zimeandikwa au hazijaandikwa; ama lugha hizo zina othografia zilizosanifiwa au hazina ama lugha mojawapo au zote mbili ni za kiishara.

Pinchuck (1977), anaeleza kuwa tafsiri ni mfanyiko tendani wa kutafuta ulinganifu wa lugha lengwa kwa usemi wa lugha chanzi.

Nida na Taber (1969), wanasema kuwa kutafsiri hujihusisha na kuhamisha ujumbe katika lugha lengwa ambao ni linganifu kutokana na ule wa lugha chanzi kwa kuzingatia maana na mtindo.

LUGHA CHANZI/ MATINI CHANZI
Hii ni lugha/matini ambayo imetumia lugha ya kwanza na ambayo haijatafsriwa. Mfano. Lugha chanzi yaweza kuwa Kiswahili, kiingereza, kijapani n.k, Pia kwa ufupi inaweza kuitwa (LC).

LUGHA/MATINI LENGWA
Hii ni lugha ambayo inapatikana baada ya matini kutafsiriwa. Pia inaweza kuitwa (LL).
Kutokana na fasili hizi za wanazuoni mbalimbali inawezekana kabisa kupata maana ya tafsri kwa kuunganisha ama kusahihisha mapungufu yaliyomo katika fasili hizo. Hebu tazama fasili, tafsiri ni matini inayopatikana kutokana na mchakato wa kuhawilisha mawazo yae yale kutoka lugha chanzi na kupeleka mawazo hay ohayo katika lugha lengwa au ni mchakato wa kuhawilisha mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.

MAMBO MUHIMU YANAYOPASWA KUZINGATIWA KATIKA TAFSIRI
Mawazo yanayoshughulikiwa lazima yawe katika maandishi na si vinginevyo. Mawazo au ujumbe kati ya matini chanzi na matini lengwa sharti yalingane. Katika hili kuna angalizo kubwa kwamba mawazo haya si lazima yawe sawa bali yanatakiwa yalingane.

Hali ya mawazo ya matini chanzi na matini lengwa kutokuwa sawa kwake kunaweza kusababishwa na sababu zifuatazo. Tofauti za kiisimu, Tofauti za kiutamaduni, Tofauti za kihistoria, Tofauti za maendeleo ya sayansi na teknolojia, na Tofauti za kimazingira.Mwansoko ameshatajwa (2013). Newmark anaendelea kueleza juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu tafsiri ni pamoja na dhamiri yake, maana yake, athari yake, mfumo wake, na dhima yake ( dhamiri ya mtunzi wa matini chanzi ni ipi, hivyo ni wazi kuwa kuyatambua mawazo ya mtunzi wa matini chanzi ni vigumu lakini ndio kazi ya tafsiri hiyo, kuhusu maana ya matini ni vema kuisoma matini kasha ukaielewa maana iliyomo ndani yake ndipo ukaanza kazi ya kuitafsiri matini lengwa, pia athari ya matini kwa wasomaji wake athari hiyo yaweza kuwa ya kiutamaduni, kiuchumi, kimazingira, kisiasa n.k,

MAMBO MUHIMU YANAYORAHISISHA KAZI YA TAFSIRI
Muktadha au mazingira asilia, mtafsiri anapaswa kuongozwa na muktadha makhsusi. Katika muktadha sharti utamaduni utangulie ndipo siasa na mamlaka vifuate.
Kanuni za sarufi za lugha husika. Katika kutafsiri kanuni ama kaida sharti zibuniwe, zibadilike, na kufuatwa. Lefevere (1998), kufasiri ni mchezo wa lugha unaojumuisha kaida ambazo zinabuniwa na mchezo wenyewe lakini ambazo zenyewe haziwezi kuwa mchezo wenyewe. Pia kufasiri ni kufuata kaida, kubadilisha kaida, kujenga kaida na kubuni kaida ambazo kwa upande wake zinaongeza uchangamano ndani na nje ya uga wake.
Maandishi ama tahajia ya lugha husika ama lengwa. Maana ya maneno yaliyomo katika matini. Jambo hili limetiliwa mkazo na mwanazuoni Newmark katika fasili yake ya tafsiri kuwa, mtaalamu anapaswa kuzingatia maana ya maneno yaliyomo katika matini, kama ilivyokusudiwa iwe na mwandish chanzi.

Maana ya nahau na misemo. Kuna maana tofautitofauti za misemo kutoka jamii moja na jamii nyingine. Si kila maana ya msemo wa Kiswahili unaweza kupatika katika lugha ya kiingereza. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia maana na misemo kutoka katika lugha lengwa.
Matumizi ya vituo na mikato katika kutenga desmali. Ni muhimu kuzingatia vituo na mikato katika kutenga desmali kwani alama hizi mbili zina matumizi tofauti hasa katika lugha ya kiispania na hile ya kiingereza. Mfano, 1,000.01 kwa kiingereza ni sahihi lakini kiispania sio sahihi kwani wao hutumia alama ya kituo ndipo ikafuata alama ya makato kama inavyoonekana hapa, 1.000,01 hivyo ni muhimu sana kuzingatia haya.

DHIMA YA TAFSIRI
Dhima au kazi ya tafsiri imeweza kuelezwa na wanazuoni mbalimbali ambo kwa hakika hawakucheza mbali na uga huu, wanazuoni hawa waliamua ndelea na kpambana vilivyo katika vita isiyo na usawa bali ulinganifu. Mwansoko na wenzake (2013:1-3), wao wametaja na kueleza dhima kuu nne za tafsiri ambapo wameanza na:
i.              Tafsiri kama njia ya mawasiliano.
ii.            Tafsiri kama nyenzo ya kueneza utamaduni.
iii.           Tafsiri kama mbinu ya kujifunza lugha.
iv.           Tafsiri kama kiliwazo cha nafsi ya mfasiri.
v.            Tafsiri huweza kuziba mapengo ya kimsamiati au kimaana katika lugha.

Pia Mshindo ametajwa (2010:25-28), hatofautiani sana na mwansoko kwani naye pia ametaja na kufafanua dhima za tafsiri kuwa ni:
i.              Tafsiri hutumika kama nyenzo ya mawasiliano.
ii.            Kufasiri ni kuuleza na kuueneza utamaduni wa jamii.
iii.           Kufasiri ni nyenzo kuu ya kufundishia lugha.
iv.           Kufasiri ni kushajiisha tabia ya kusoma na kutafiti.
v.            Kufasiri huziba mapengo ya kimsamiati au kimaana baina ya lugha.
vi.           Kufasiri huwa kiliwazo

Wataalamu hawatofautiani sana katika ufafanuzi wa dhima za tafsiri katika maisha ya kila siku, japo tofauti zipo lakini si kubwa sana. Kuhusu suala la tafsiri kama njia ya mawasiliano, waandishi hawa wanaeleza kuwa katika kufasiri kuna mawasiliano changamano sana baina ya tamaduni. Katika maisha ya kila siku watu huwasiliana kwa kutumia ujumbe uliofasiriwa kwa kufuata misingi ya kiutamaduni. Katika kufanikisha mawasiliano baina ya jamii mbili tofauti ujumbe wa matini chanzi hufasiriwa na kuwekwa katika matini lengwa. Hivyo mawazo ya matini chanzi hutumika na watu wenye uwezo wa kutumia lugha ya matini lengwa. Utofauti wa kutumia lugha tofauti duniani umesababisha tukio la kutafsiri. Mwansoko na wenzake ameshatajwa (2013:2), wanaeleza kuwa kama njia ya mawasiliano miongoni mwa mataifa mbalimbali, tafsiri inatumika kutolea maelezo ya biashara.

Tafsiri kama nyenzo ya kunezea utamaduni, mwingiliano wa tamaduni za mataifa mbalimbali zinaenezwa kwa kutumia tafsiri za matini. Nchi nyingi zinaeneza utamaduni wake kupitia matini mbalimbali. Yapo matini yalitafsiriwa kutoka lugha chanzi ya kiingereza na kuweka katika lugha lengwa yaani Kiswahili. Hivyo basi kutokana na matini ya kingereza kufasiriwa na kutumika katika jamii ya waswahili, kupo kuenea kwa utamaduni wa mwingereza katika jamii ya waswahili. Mfano mzuri ni kitabu cha Mashimo ya Mfalme Sulemani, kilichofasiriwa na F. Johnson. Kinaonesha wazi ni jinsi gani utamaduni wa mzungu ulivyoenezwa katika jamii ya waafrika.

Tafsiri kama nyenzo ya kufundishia lugha, ili kuweza kupata mawazo au kuvijua vipengee vya lugha nyingine huna budi kutumia taaluma ya tafsiri ili uweze kuyatambua mawazo yaliyomo katika lugha chanzi na kuipeleka katika lugha lengwa. Mfano Mshindo, (2010:26), anaeleza kuwa katika miaka ya hamsini(50) na sitini (60), Kiswahili kilitumika kufundishia lugha ya kiingereza katika skuli za sekondari za Zanzibar. Mbinu iliyotumika ni wanafunzi kupewa miundo ya Kiswahili na kuifasiri kwa kiingereza au kupewa miundo ya kiingereza aifasiri kwa Kiswahili. kutokana na dhima hii ni muhimu sana kwa mfasiri kujifunza miundo ya lugha zote mbili.

Kufasiri ni kushaajiisha tabia ya kusoma na utafiti. katika kazi hii ya kufasiri, mfasiri analazimika kukusanya kwa  kusoma visawe vingi na miundo mingi ya lugha zitakazo msaidia katika kazi yake ya kufasiri. Kusoma kunamsukuma mfasiri kufanya utafikti wa kina juu ya visawe, utamaduni wa lugha lengwa na chanzi, kukusanya misamiati. Kwa kufanya hivo mfasiri anakuwa na uwanja mpana wa kuimudu kazi yake. Ikumbukwe tu kuwa hakuna hukumu ya kazi bila ya kuwa na data sahihi, hivyo ili hukumu iweze kuwa sahihi mfasiri analazimika kufuata kanuni za utafiti ili aweze kuwa na uhakika wa kazi yake.Mshindo ameshatajwa uk. 27, anafafanua kwamba ukweli ni kwamba hakuna mfasiri ambaye hafanyi utafiti, japo mdogo, katika shughuli ya kufasiri. Hulazimika kupekua katika nyaraka mbalimbali ili kujua maana ya maneno, usuliwa mambo, na historia ya matukio.

Kufasiri huziba mapengo ya ya kimsamiati au kimaana baina ya lugha, maneno mengi hukumbwa na atahari za kiutamaduni, kiisimu, na kihali. Kutokana na athari hizi mfasiri hulazimika kutafuta maana ya maneno yatakayoeleweka vizuri kwa watumiaji wa lugha lengwa. Hii hutokana na utofauti wa matumizi katika baadhi ya maneno ambayo ambayo katika jamii nyingine yana maana tofauti na ile ya lugha chanzi. Mfano: Mshindo ameshatajwa anasema, katika mazingira ya rushwa neno mchicha, ambalo maana iliyozoeleka ni aina ya mboga ya majani, haliwezi kukidhi haja kwa maana hiyo iwapo mfasiri hakulifafanua katika tafsiri yake na kumwezesha msomaji wake kuelewa kwamba katika muktadha huo lina maana ya rushwa. Pia katika mazingira mengine neno wimbo husimama badala ya rushwa kwani kuna baadhi ya watuhumiwa huambiwa kuwa ili uweze kuishinda kesi hii huna budi kuimba wimbo wako.

Kufasiri kama kiliwazo, katika kazi ya kufasiri wapo baadhi ya wafasiri ambao huifanya kazi kama kiliwazo cha nafsi zao. Katika dhima hii kazi zinazoshughulikiwa ni kazi za kishairi. Kufasiri huku si kwa lengo jingine lolote lile. Kwani kazi hizi huwa kiliwazo cha mfasiri kwa sababu tu mfasiri huwa na amani hasa pale anapofanikiwa kuifaisiri kazi ambayo ililikuwa inampa shida kubwa akili mwake. Mara tu baada ya kukamilisha shughuli nzito hiyo mfasiri huifurahisha akilini yake kwa kukubali kazi yake. Mwansoko na wenzake wametajwa, uk:3 wanaeleza wazi kuwa tafsiri humfanya mfasiri aburudike na kuridhisha nafsi yake kadiri anavyotatua matatizo yake ya kufasiri. Utafutaji wa visawe mwafaka katika lugha lengwa kwa kawaida ni kazi ngumu, inayochosha na kuchusha. Hizi ni baadhi tu ya dhima pia zinaweza kuongezeka zaidi ya hizi hii ni kutegemea na chanzo cha maandiko na utafutaji wa msomaji hivy unaalikwa kutembelea uwanja wa fasiri ili uweze kutoa mawazo yako.

HISTORIA FUPI YA TAFSIRI

Misri ni nchi inayopatika katika bara la Afrika, nchi hii kihistoria ndio nchi mama ya maendeleo yanayoonekana leo hii. Maendeleo haya hasa ni yale ya kiuchumi, kijami ina kisayansi. Ugunduzi wa mambo mengi yalitokea katika nchi hii ya Misri yalizifikia nchi nyingine kwa njia za tafsiri. Miaka 3,000 na zaidi kabla ya kuzaliwa kristo, ulitokea uvumbuzi wa mambo mengi. ugunduzi wa taaluma mbalimbali uliwasukuma wasomo wa Kiyunani kufika katika nchi ya Misri kwa lengo la kujifunza taaluma. Mnamo karne ya kumi na tisa (19), ili kuweza kuyapata maarifa Wayunani walilazimika kuijua kwanza lugha ya Wamisri, pia walitumia miaka mingi y asana kuishi Misri wakiisaka elimu. Kazi ya kuisaka elimu haikufanywa na kila Myunani bali wasomi wengi na maarufu waliamua kufanya hivyo. Mambo waliyojifunza huko waliyatafsri kwa lugha yao yaani Kiyunani, hivyo lugha ya Misri ilikuwa lugha chanzi na lugha ya Wayunani ilikuwa lugha lengwa.

Mwansoko na wenzake (2013:4), wasema, wakati wa himaya ya Warumi hasa baada ya Ukristo kuenea huko ulaya nzima, elimu hiyo ya zamani ilianza kupigwa vita kwa kudaiwa kuwa ilikuwa ya “kipagani”, kipindi hiki kilipelekea zama za giza. Baada ya kuimarika kwa Uislamu Mashariki ya Kati, Afrika ya Kaskazini na Hispania, wataalamu na wasomi wa Kiislamu walisoma elimu ya Wayunani hasa ile ya kale. Walifanya kazi kubwa ya kufasiri maandiko yale, lugha chanzi ikiwa ni Kiyunani na lugha lengwa ni Kiarabu. Mara tu baada ya kazi kubwa ya kufasiri iliyofanywa na wafasiri matokeo makubwa yalitokea na utamaduni mpya ulienea. Kutokea huku kwa maendeleo makubwa katika nchi za Kiarabu kulisababisha uchumi wan chi za ulaya kuzidi kudidimia. Karne ya kimi na mbili ikumbukwe kuwa ilikuwa na tukio la vita vya msalaba, vita hivi vilihusisha pande mbili yaani Wakristo na Waislamu, wakati wa vita hii wataalamu wengi toka ulaya walishuhudia maendeleo makubwa sana katika nchi za Kiarabu. Wataalamu hao waliamua kuchukus vitabu na kuenda navyo kwa nia ya kufasiri, ili waweze kupata maarifa ya Waarabu na siri kubwa ya maendeleo. Karne ya kumia na tano (15), ulaya ilianza kupata maendeleo makubwa yaliyoifanya ulaya kutoka katika zama za giza zilizosababishwa na imani zao potofu. Kipindi hiki kiliifanya ulaya kuingia katika mfumko wa elimu na maarifa.

Mfano wa vitabu vingi vilivyo fasiriwa vilishika kasi sana ambapo maandishi yaliyosheheni mawazo ya wataalamu mbalimbali. Mawazo haya ya vitabun yalifasiriwa kwa lengo la kuwafikia wasomaji awa nchi za ulimwengu wa tatu.

Karne ya ishirini (20), ni kipindi ambacho kinaonesha kuenea na kukua kwa tafsiri hasa kwa wingi wa maandiko mengi kutafsiriwa. Ni katika kipindi hiki mikataba mingi ya kitaifa kati ya mashirika ya umma nay ale ya binafsi ilifasiriwa na kuleta urahisi mkubwa mawazo kuwafikia watu mbalimbali.

Tafsri nchini Tanzania, ilichelewa kuingia, kwani ni katika karne ya 13, utenzi wa Hamziya uliweza kutafsiriwa kutoka lugha ya Kiarabu (chanzi), na kupelekwa katika Kiswahili (lengwa), katika karne ya (19), vitabu vingi vilifasiriwa na Wamisionari na vingi kati ya hivyo vilikuwa vyenye maudhui ya kidini na hasa dini ya Kikristo (Biblia), vitabu vya fasihi vilivyofasiriwa ni pamoja na Safari ya Gulliver, Hadithi za Allen Quartermain, Robinson Kruso na Kisiwa ckake.
Baada ya uhuru vitabu kama vile Julius Kaizali, Mabepari wa Venasi vilifasiriwa na kwa lengo la kufikisha mawazo kwa waswahili wengine. Mfasiri akiwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Matokeo ya fasiri hizi yanaifanya Tanzania kuwa na hazina kubwa ya mawazo mbalimbali. Mawazo haya yalipatikana kutoka katika lugha nyingi zikiwemo zile za Kiarabu, Kifaransa, Kifini, Kijerumani, Kikorea na Kiingereza.

Pia yapo mashirika yanayofanya kazi ya kufasiri hususani shirika la uchapishaji wa lugha za kigeni, shirika la uchapishaji wa la maendeleo na mashirika mengine mengi. kasoro katia taaluma ya tafsiri haikwepeki. Kwani sifa ya matini mbili yaani chanzi na lengwa sharti zilingane tu, na wala si kuwa sawa. Hivyo ni wito kwa wazawa kufasiri vitabu vya maarifa ya sayansi kama ilivyo katika kazi fasihi. Shukrani za pekee kwa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam (TUKI), Shirika la Habari la Tanzania. Pia pongezi hizi ziwafikie Chama cha WAFASIRI kilichoanzishwa mwaka 1981, kwa kusimamia haki na maslahi ya Wafasiri.  

 NADHARIA YA TAFSIRI

Nadharia ya tafsiri ni maelekezo kuntu juu ya vipengee anuwai vya kifasiri vinavyopaswa kuzingatiwa na kila mfasiri akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Kila kitu hapa duniani huwa na mwanzo wake hivyo hivyo nadharia ya tafsiri ina mwanzo wake ambao unasheheni sababu nyingi za kuanzishwa kwake. Newmark (1982:4-5), anataja sababu kuu tatu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri, sababu hizo zinafafanuliwa kama ifuatavyo:

Mosi, ni kuwepo kwa makosa mengi, hasa yale ya kimuundo, kimaumbo na kimsamiati. Katika taaluma hii ya tafsiri ni vigumu sana kuipata kazi iliyotafsiriwa isiyokuwa na makosa. Kwa hali yoyote hile mfasiri huogelea katika makosa, ingawa anaweza kufanya jitihada za kupunguza baadhi ya makosa.

Pili, idadi kubwa na inayozidi kuongezeka kwa asasi zinazojishughulisha na kazi ya tafsiri. Hapa nchini Tanzania asasi kama vile Baraza la Kiswahilila Taifa, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Shirika la Habari La Tanzania na mashirika ya watu binafsi, kama vile KIU na ILOS, na vyombo vyote vya habari.

Tatu, ni mfumko wa istilahi katika taaluma mbalimbali, hasa sayansi na teknolojia, haja ya kuzisanifisha ili kuwezesha tafsiri baina ya lugha moja na nyingine kufanyika kwa ufanisi zaidi. Yapo baadhi ya masomo ambayo kila siku misamiati mipya inaundwa hivyo basi kutokana uibuzi huu wa misamiati mipya huifanya kazi ya tafsiri kuwa na mapungufu mengi.

Kama ilivyo katika mimea na wanyama kutegemea katika kulisha jambo ambalo wanasayansi wanaliita mlishano yaani simba hutegemea nyama kutoka kwa wanyama wengine, ambao wanategemea kupata chakula kutokana na nyasi na nyasi hutegemea mbolea kutoka kwa wanyama, basi hata nadharia ya tafsiri hutegemeana kama si kuhusiana kwa ukaribu na taaluma nyingine kama vile: Mwansoko na wenzake (2013), wanaanza kwa kusema kuwa tafsiri ni sehemu ya taaluma ya lugha ijulikanayo kama isimu tumizi. Kwa upande mwingine, ni sehemu ya isimu linganishi na katika ismu huchuliwa kama sehemu ya semantiki, yaani elimumaana.

Nadharia ya tafsiri inahusiana kwa karibu sana na isimu linganishi, imbayo kwa kiasi kikubwa hujishughulisha na kulinganisha vipengele vya kiisimu vya lugha mbili au zaidi pamoja na kuchunguza mbinu za uzalishaji. Katika kipengele hiki mfasiri hupata faida ya kuelewa mifumo ya lugha nyingi na namna lugha hizo zinavyotumia zana za kiisimu katika kuwasilisha taarifa anuwai.

Pia nadharia ya tafsiri inahusiana na isimu jamii, taaluma hii huchunguza hasa mahusiano ya lugha na jamii anuwai inayotumia lugha husika. Katika kuchunguza mahusihano taaluma hii uchunguza rejesta za kijamii za lugha na matokeo hasi na chanya ya mwingiliano uliopo baina ya lugha mbili zinazotofautiana kiutamaduni. Hivyo ni wajibu na jukumu la mfasiri kujua tofauti hizi za kiutamaduni na kuzizingatia katika kazi ya kufasiri.

Vilevile nadharia ya tafsiri inahusiana na semantiki ambayo ni elimumaana, kwa kawaida kinachofasiriwa ni mawazo ua maana ya matini na wala sio maneno pwekepweke. Kutokana na taaluma hii kuchunguza maana ni muhimu kwa mfasiri kuijua vizuri taaluma hii ili iwe msingi kwake wa kufasiri matini mbalimbali. Fasiri huendana na kujua maana za maneno, hali ambayo humfanya mfasiri awe na kamusi mbalimbali ili aweze kubaini maana mbalimbali za maneno. Taaluma hii pia humsaidi mfasiri kugundua kuwa maana hazitokani na maneno pwekepweke, ili awezekuchagua maneno kuendana na muktadha.

Elimumtindo ni taaluma nyingine inayohusiana kwa karibu kabisa na nadharia ya tafsiri, kwani taaluma hii hushughulikia uainishaji wa mitindo ya lugha na mikitadha ya matumizi yake. Elimu hii hufanya mfasiri abaini mitindo mbalimbali ya matini chanzi, mtindo huo wa matini chanzi hupelekwa kwa tafsiri katika matini lengwa. Ingawa taaluma hii inahusiana na taaluma hizi pia upo uhusiano wa nadharia hii ya tafsiri na:

Uhakiki matini, katika uhakiki wa matini mfasiri hufanya tathimini ya kina juu ya matini husika kabla ya kutoa hukumu ya ubora wa matini chanzi kabla ya kuitafakari na hatimaye kuifasiri. Mfasiri huakiki vipengele mbalimbali kama vile kipengele cha utamaduni, mazingira n.k


Mantiki, mfasiri husafiri katika uga wa mawazo ya kina ambayo humfanya atambue ukweli na usahihi wa kauli zilizomo kwenye matini chanzi. Taaluma hii humfanya mfasiri kuchambu kauli zenye uvulivuli na kuzirekebisha kabla ya kazi ya kufasiri.

Mwisho nadharia ya tafsiri inahusiana na taaluma ya falsafa inayosisitiza zaidi katika kutafuta maana za maneno kutokana na matumizi yake halisi katika matini inayohusika. TUKI, (2012) wanaeleza falsafa kuwa ni elimu ya asili, maana na sababu za mambo au vitu.


  

                                                     Marejeo
Mshindo,H.B (2010), Kufasiri na Tafsiri,Chuo kikuu cha Chukwani, Zanzibar.
Mwansoko H.J.M, na wenzake (2013), Kitangulizi cha Tafsiri Nadharia na Mbinu, TUKI, Dar es Salaam.

Taasisi ya taaluma za lugha za Kiswahili (2011), Kioo cha Lugha, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.   

11 comments:

Unknown said...

Nice

Unknown said...

Safi sana

Unknown said...

Somo zuri

Fredii thywan said...

Hakika somo hili lafaa kabisa

Fredii thywan said...

Hakika somo hili lafaa kabisa

Unknown said...

Somo zuri Sana limenifanya nimepata uelewa zaidi kuhusu tafsiri na ukaliman

Unknown said...

Nimepata ufahamu mwingi. Shukurani kwa kazi hii nzuri.

Unknown said...

Hakika nimejufunza Mambo mengi kupitia nukuu hizi

Unknown said...

Well

Unknown said...

Somo zuri ila umejikita zaidi katika taaluma ya tafsiri; hivyo ungejaribu kuangalia pia kwenye taaluma ya ukalimani.

Unknown said...

Wow. I'm impressed