Ndugu zangu
wapendwa, salamu nazitoa kwenu ninyi nyote zikiniacha mimi ndugu yenu nikiwa
katika hali ya kufikiria kwa nini tuko hapa? Salaam ziwafikieni nyote mlioko
shambani mkitafuta riziki kwa kutumia jembe la mkono, mkilima katika shamba
lenye miba mingi, mkitokwa jasho sehemu karibu zote za miili yenu, na kuliramba
jasho litiririkalo kutoka vichwani mwenu, pia salaamu ziwafikie wafugaji ambao
kutwa nzima mnazunguka na mifugo yenu porini huku mkitafuta marisho na maji ya
kuwapa ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda wenu uhai. Lakini haya yote mnayakosa
kwa sababu hali ya mazingira yetu ya asili imebadirika na kuwa ya UTANDAWAZI,
Salaam nyingine
za dhati nazituma kwa waalimu wote, madaktari, wafanyakazi bandarini,
wajasiliamali, bila kuwa sahau wadogo zangu wanaoshinda katika masazo ya watu
warukao kutwa nzima na midege yenye raha duniani, salaamu hizi ziwafikie akina
mama wote mkiwa katika wadi ambazo hazina utofauti na jela, mwisho ningependa
kuwapa salaamu za upendo ndugu zangu ambao kutwa wanawindwa mithili ya digidigi
na viungo vyao kuwa vyanzo vya mapato ya wajinga wachache ambao wanalirudisha
nyuma taifa changa lenye zaidi ya miaka arobaini.
Hapana wa mwisho
ni hawa watoto ambao wazazi wao wametangulia mbele ya haki ama walitupwa jalalani
na wazazi ambao walizitia nywele zao kemikali na kuziharibu akili zao na kuwa
bora ya kichaa anayeandika namba za usajili za kila gari inayo katisha mbele
yake. Watoto hawa waliokolewa kwa kuokotwa na kuokolewa kutoka katika midomo ya
nguruwe, na mbwa koko ambao kutwa nzima wanacheza jalalani. Kwa pamoja nasema
Salaamu.
Ndugu zangu
labda nianze kwa kusema “HERI KULIMIA NG’OMBE ULIYECHAGULIWA NA MTU
KWA LENGO LA KWENDA KULIMA SHAMBA UKWENI NA NG’OMBE HUYO AKALALA SHAMBANI, KULIKO
KULIMIA NG’OMBE ULIYEMCHAGUA MWENYEWE KUTOKA KATIKA ZIZI LENYE NG’OMBE WENGI WENYE AFYA NJEMA AKALALA
SHAMBANI TENA UKWENI.”
Hapana! Hapana!
Hapana! Narudia tena hapana, hatutoruhusu tena kaka ukatutie aibu ukweni ni
heri kulimia mbuzi hawa labda tutaweza kulimaliza shamba hata kama
ni kwa muda mrefu tutamaliza kulima.
Ndugu zangu
ajali iliyotokea mwanzo haikuwa na mshindo kama hii iliyotokea leo asubuhi,
kwani mshindo wake umesikika mbali kwani hata jirani anashangaa, hebu nikuulize
swali ni vipi dereva aliyesababisha ajali kubwa iliyouwa watoto zaidi ya sitini
kati ya wale mia waliokuwa wakisafiri kwenda katika nchi ya ujuzi kwa lengo la
kusaka taaluma ambayo ingewafanya wajitegemee baadaye na kuwa kizazi bora apewe
tena usukani na kuliongoza gari hilo huku dereva huyu akiwa amefungwa majeraha
na madakitari bingwa kutoka nje ya nchi ya watu weusi? Dereva aliyekatika mkono
harafu anang’ang’ania gari? Eti jamani
swali hili jibu twalijua?
Kweli asiyeona
akioneshwa haoni, kwa huzuni tuumalizeni msiba matanga tuyaanueni maana hatuwezi
kujua nini akifanyacho kobe pindi awapo kimya
ndani ya jumba lake
huku miguu na kichwa
chake vikiwa ndani labda tusuburi jibu. Maana tuliyemkabidhi silaha ndiye
huyu anayegeuka na kutujeruhi
anayetuuzia kuni zetu, anayetuuzia maji yetu, anayetuuzia ardhi yetu,
anayetuuzia urithi wetu ndiye huyu anayecheka nasi wakati wa kulia kwetu ni
vipi kijana kuoga na kuvaa nguo safi
pindi uendapo kumposa binti wa jirani ilihali hali yako inafahamika, ni heri
yule aliyesema akipata nauli mjini kwa mjomba atakwenda kuliko sisi tulioko
huku tunywao maji yaliyochanganyika na kemikali kutoka katika migodi waliyopewa
wageni, tulao mlenda na kulala, tulimao na bei tukapangiwa, tuingiao baharini
na kuhatarisha maisha yetu kwa kucheza na mamba, tufikapo ufukweni mwatusubiri kwa bei chini, tuwakumbatiao watoto wachanga
ambao wanalia kwa uchungu wakiwatafuta matiti ya mama zao katika vifua vya wanaume maana sisi
hatutaki kusafiri. Tulichoka katika safari tuliyosafiri jana dereva akiwa huyu!
Huyu!, hebu watazame bibi zangu wale hawana hamu ya kusafiri tena kwenda
kumuuona mjukuu wao aliyezaliwa, nashangaa hata babu zangu walio mkabidhi mkuki
dereva huyu siku yake ya kwanza kukabidhiwa gari aliendeshe salaama na
alifikishe salaama hawataki tena kupanda gari la dereva waliye mwamini.
Zaidi ni hawa mama zangu wanaotoa machozi mabichi
yaliyosababishwa na dhuruma na mwedo wa kasi aliokuwa nao dereva huyu katili
ambaye mara nyingi mwendo kasi wake hushangiliwa na wapiga debe wachache ambao
hutudagaya kuwa gari hili ni zuri halina tatizo, lina nafasi za kutosha maji na
chakula tutavikuta humo, ikiwa wao hawasafiri na hubakia kituoni hapo, na
kuanza kutoa sifa kama zilezile katika gari jingine. Mama zangu walishuhudia watoto wa wanawake wenzao
wakigongwa na kusagwasagwa kama mawe mgodini na huyu dereva msifika, mimi na
hawa wote tumeamua kupiga hatua mbilimbele kuelekea magerezani ambako wapo
ndugu zetu waliofungwa bila hatia, kuiamuru makama iwaachie huru ili waweze
kufanya kazi za kimaendeleo kuliko kula chakula ambacho wake zao walioachwa
wakiwa wajawazito wakilima na kuipinda
migongo yao iliyo wabeba watoto waliodhoofika kwa kukosa lishe bora.
Kwa pamoja
tunasema watoke! Watoke! Watoke! Watoke wawe huru kwani babu zetu waliokufa
wakipigania ardhi yetu wameamua kutuunga mkono, wanasiasa waliouliwa kwa hila
wameamua kuwa mbele yetu na maandamano makubwa yatafanywa na watoto wachanga
siku yao ya
watoto Duniani. Watoto wameayaona maovu yenu enyi tembo mnao angusha miti
katika mbuga yenye amani, wameona wizi muufanyao katika rasilimali za nchi yao
ambayo kila kukicha mwasimama majukwaani na kupayuka “WATOTO NI TAIFA LA KESHO”
hivyo tulitunze na kulilinda, watoto wamechoka na elimu ya kishenzi
inayotolewa, wanashangaa ni kwanini nyote mlioko madarakani mnajua kusoma,
kuhesabu na kuandika lakini wao kila kukicha wanaandikwa magazetini tena
magazeti yasiyo na uhuru wa habari ooh! ufahulu umeshuka, tuunde tume, tufanye
tafiti, watoto wamefanya tafiti na kugundua kuwa tume hasifundishi, tafiti
zimetosha maana karatasi na vifaa vinavyotumika kufanyia tafiti ni heri
zitumike kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Watoto wanayo
michezo na burudani nyingi za asili ambazo walikuwa wakicheza wakati wa
mbalamwezi, michezo iliyowafanya wakawa na miili kakamavu, hawakuwabana mama
zao majikoni pindi waandaapo chakula. watoto walicheza kwa pamoja tena kwa
umoja, walijifunza malezi hata kabla ya kuwa walezi, mama aliigiza umama na
baba aliigiza ubaba watoto waliigiza utoto yote hayo yalifanyika katika familia
iliyoundwa na mama mtoto, baba mtoto, na watoto. Ikumbukwe kuwa hakuna
aliyewafundisha bali walirithi toka kizazi kimoja hadi kingine. Kutokana na
mambo yote yaliyowakera watoto hawa wameamua kuandika barua na wanaomba isomwe
na kila ajuaye kusoma wakiwemo kaka, dada, mama, baba, mjomba, shangazi, bibi,
babu na ndugu jamaa na marafiki wote.
BARUA YA
WATOTO KWA WAZAZI
Wapendwa
baba na mama zetu, salaam.
Salaam zetu
ziwafikie wazazi wetu baba na mama, mkiona vema mzifikishe kwa babu na bibi,
kama babu na bibi zetu watazipokea basi wazifikishe kwa mizimu yetu
iliyotuachia imani zetu, na mizimu yetu izifikishe salaamu hizi mahali aishipo
Mungu wa miungu asante,
Dhumuni la barua
hii ni kuwataarifu kuwa kutokana na
kishindo cha ajali iliyotokea siku
chache zilizopita na kuwaangamiza kaka zetu na dada zetu waliokuwa na nia njema
ya kuusaka ujuzi wa kitaaluma lakini cha kushangaza tunaona tume zinaandaliwa
na mapesa mengi yanatolewa kwa ajali ya kamati teule ya mtendaji mkuu wa
kijijji chetu. Sisi watoto wenu tumeamua kwa pamoja na kwa moyo umoja kuingia barabarani
kumshinikiza dereva aliyeshikilia usukani aachie ngazi ili gari letu liendeshwe
na sisi wenyewe watoto mliodhani hatuyaoni yanayotendeka humu kijijini. Katika
maandalizi ya siku yetu ya watoto duniani tumeamua tusile wali, soda, kuku,
chips, nyama ya ng’ombe, nyama mbuzi, vileo, na mayai toka ughaibuni yanayoandikiwa
pesa nyigi wakati sisi tu vibogoyo! wala hatutonyonya maziwa ya mama zetu yaliyojaa
uchungu wa maisha usababishwa na dereva
katili tuliyemshuhudia tukiwa tu katika matumbo yenu.
Wazazi wetu
katika sikukuu hiyo tutahitaji kuona vipaji kutoka miongoni mwetu kwani ngoma
zetu zimeeharibiwa na utamaduni toka nje sasa mwacheza viduku, mwaimba kwa
kufoka, mwalilia mapenzi badala ya kuhiza maendeleo mimi Kirundumusi ni shuhuda
wa hayo myatendayo mchana kweupe na usiku pia, sisi watoto kwa macho yetu
wenyewe macho yenye kujaa ukungu mkidhani hatuyaoni matendo juani, tuliyaona
hayo na tumeamua kubadilika na katika risara tutakayo isoma mbele ya mgeni wetu
rasmi si risala kama zenu mlizozoea kuimba rushwa, ufisadi, huduma za jamii, na
kuwahurumia watoto na wamama wajawazito kwa kuandika jumbe fupi katika simu
zenu za gharama na kuomba misaada ya vyadarua toka nchi za magharibi. Katika
risala yetu tutazungumzia sera ya lugha ya kiswahili ambayo ndio muhimili wa
maendeleo ya taifa letu watoto, sera itakayokuwa tofauti na yenu mnayoburuzwa
kwa kukariri lugha msizozijua, pia tutahakikisha sisi watoto tunaurudisha mfumo
wa elimu mlio upuuza na kuanza kuwaburuza kaka na dada zetu waliopata ajali
pasipo wao kuhiari, sisi tutahakikisha mfumo wa KKK tatu unarudishwa kwa
wajinga wasiojua unaitwa KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU.
Wenu wanenu
tuliotoroka katika matumbo yenu yaliyo jaa majipu ya maumivu, hasira, kisasi,
huzuni, kwa pamoja tunasema tumeaua! tumeamua! kupambana hatutayaogopa mabomu
ya machozi, kama ni risasi za moto sisi pia tu
moto hivyo dawa ya moto ni moto na hivyo vitoa moshi twavijua vizuri kwani
dalili ya moto ni moshi.
Na, kapele harry, simu 0763891415
Blog, www.kapeleh.blogspot.com
No comments:
Post a Comment