Monday, September 2, 2013

KAULI MBIU - CHAWAKAMA


 KAULI MBIU (CHAWAKAMA)
      KIGALI-RWANDA (2013)

Kipenga nakipuliza, uwanjani naingia,
Salamu natanguliza, nawaomba kupokea,
Amani naitangaza, karibu mja tulia,
Pongezi kwa chawakama, kongamano kulipanga,

Karibu wa mashariki, karibu nanyi wa kati,
Kiswahili tukilaki, tukiweke katikati,
Hata kama hukitaki, ndugu upige saluti,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Kwa kuimba nitaimba, nitaimba Kiswahili,
Kurumba nitakirumba, nitarumba Kiswahili,
Kwa Kiswahili taamba, sauti ifike mbali,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Kiswahili nakipamba, kwazo rangi na maua,
Nawajuza vuta kamba, Kiswahili ndio njia,
Za kigeni kwenu kamba, mwilini zang’ang’ania,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Maendeleo hayaji, lugha yetu kuisusa,
Tutabaki waombaji, mazuri kutoyagusa,
Aibu yake mwombaji, kwa kitambo humtesa,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Kiswahili kinalia, mipaka kimewekewa,                            
Nguvu yake yapungua, za kigeni kutumiwa,
Msamiati potea, lugha kudharauliwa, 
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Tuwatazame wachina, katika tenda rufufu,
Kichina hakijachina, lugha yao ni tukufu,
Ujuzi wanajuzana, wachina sawa mkufu,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Tanzania zindukeni, Kenya sasa amkeni,
Uganda changamkeni, Rwanda nanyi pulikeni,
Enyi kati hongereni, Burundi jivunieni
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Wasomi tuzindukeni, kulala tukuacheni,
Tujiulize  kwanini, tongotongo zi usoni,
Tu kituko kwa wageni, ombaomba mstarini,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Tujichunguze wenyewe, tatizo tunalo sisi,
Tumfano wake mwewe, tamaa zetu za fisi,
Kila kitu tukwapuwe, meno yana ukakasi,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Naja na kwao wachache, wavivu wa kufikiri,
Wanenayo wayaache, mawazo yao sifuri,
Kiswahili kama mche, kwa ajira ni tajiri,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Lugha yetu tuienzi, bila shaka tutatoka,
Kiswahili ni kurunzi, mbele yetu chamulika,
Tuitumie wajenzi, bara letu kusimika,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

Waja ninatia nanga, mengine kuyasikia,
Kutoka kwao malenga, lugha hii waijua,
Yalomuhimu kulonga, hapa natamatishia,
Kiswahili yetu tunu, johari ya Afrika.

                                               Mawasiliano:   hkapele@gmail.com
                                                                      www.harrykapele.blogspot.com
                                                                      +255763891415
                                                                       









No comments: